Jul 16, 2023 08:04 UTC
  • Sisitizo la Russia la kuheshimu umoja wa ardhi yote ya Iran

Mikhail Bogdanov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia na mwakilishi maalumu wa rais wa nchi hiyo katika masuala ya Asia Magharibi na Afrika, amesisitiza juu ya kuheshimiwa mamlaka na umoja wa ardhi yote ya Iran kama nchi rafiki. Bogdanov ameyasema hayo katika mkutano na Kazem Jalali, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Moscow.

Naibu waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ametoa kauli hiyo ukiwa ni mjibizo kwa habari zilizotangazwa kuhusiana na mkutano wa pamoja wa hivi karibuni wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na Russia, na kusisitiza juu ya misimamo thabiti ya nchi yake kuhusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni nchi rafiki na kwamba Moscow inaheshimu mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi yote ya Iran.
Kazem Jalali (kulia) na Mikhail Bogdanov walipokutana mjini Moscow

Sisitizo la Russia la kuheshimu umoja wa ardhi yote ya Iran limetolewa kufuatia hisia na mijibizo kadhaa iliyotolewa na kuonyeshwa na viongozi na vyombo vya habari vya Iran kutokana na msimamo iliochukua Moscow kuhusu visiwa vitatu vya Iran katika Ghuba ya Uajemi. Tehran imeshatangaza na kusisitiza mara kadhaa kuwa visiwa vitatu vya Bumousa na Tunb Kubwa na Ndogo ni sehemu isiyoweza kutenganishwa na ya milele ya ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kukemea madai yoyote yanayotolewa juu ya suala hilo. Kadhia ya visiwa hivyo vitatu ni moja ya sababu kuu za tofauti zilizopo kati ya Iran na Muungano wa Falme za Kiarabu, Imarati. Imarati inadai kuwa visiwa hivyo vitatu ni milki yake lakini hivi sasa vinakaliwa kwa mabavu na Iran. Lakini Iran inavitambua visiwa hivyo vitatu kuwa ni sehemu isiyoweza kutenganishwa na ardhi yake na inatupilia mbali dhana ya kufanya mazungumzo ya aina yoyote au usuluhishi wowote ule wa kimataifa juu ya suala hilo.

Mwishoni mwa mkutano wa sita wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi na Russia uliofanyika mjini Moscow Jumatatu ya tarehe 10 Julai kwa anuani ya Mazungumzo ya Kistratejia kati ya Russia na nchi hizo, ilitolewa taarifa ya pamoja, ambapo nchi hizo sita za Kiarabu na Russia ziligusia madai ya Imarati ya umiliki wa visiwa vitatu vya Tonb Kubwa na Ndogo na Bumoussa na kutangaza uungaji mkono wao kwa kile kilichotajwa kama juhudi za nchi hiyo za kutatua suala hilo kwa njia ya mazungumzo ya pande mbili na Iran au kupitia Mahakama ya Kimataifa. Kufuatiwa kutangazwa msimamo huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliwasilisha malalamiko rasmi kwa Russia, ambapo mbali na msimamo wa wazi kabisa uliotangazwa na Waziri wa Mambo ya Nje, balozi wa Russia mjini Tehran aliitwa Wizara ya Mambo ya Nje na kukabidhiwa hati ya malalamiko ya Tehran kwa maelezo yaliyomo kwenye taarifa ya mkutano wa Moscow. Nasser Kanani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, sambamba na kusisitiza kuwa yaliyomo katika taarifa ya pamoja ya nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na Russia kuhusiana na visiwa vitatu vya Iran hayakubaliki, alisema: "visiwa hivi vitabakia milele kuwa milki ya Iran; na kutolewa taarifa za aina hii kunakinzana na uhusiano wa kirafiki uliopo kati ya Iran na majirani zake".

Msimamo huu unaonyesha kuwa licha ya uhusiano wa karibu uliopo baina ya Iran na Russia pamoja na China, kila pale nchi hizo zinapochukua misimamo inayopingana na umoja wa ardhi yote ya Iran hususan katika muktadha wa kustawisha uhusiano na nchi za kandokando ya kusini ya Ghuba ya Uajemi, Tehran haitakuwa na kigugumizi katika kuchukua msimamo na kutoa jibu kali juu ya suala hilo. Nukta ya kutafakari hapa ni kwamba Imarati, ambayo haikupata tija yoyote ilipowasilisha malalamiko yake huko nyuma Umoja wa Mataifa, hasa kwa Baraza la Usalama la umoja huo mnamo mwaka 1980, sasa inajaribu kutafuta uungaji mkono wa madola makubwa kimataifa juu ya suala hilo. Bila shaka, na kwa kuzingatia nyaraka madhubuti ilizonazo Iran za kuthibitisha mamlaka yake ya kitaifa juu ya visiwa vya Bumousa na Tunb Kubwa na Ndogo, na hali ya mlingano wa nguvu kikanda ilivyo, uwezekano wa Imarati kufanikiwa katika kampeni yake hiyo ni finyu na mdogo mno. Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter: "Hakuna kutafadhalishana na mtu yeyote linapokuja suala la uhuru na mamlaka ya ardhi ya Iran."

Viongozi wa nchi wanachama wa GCC (picha ya maktaba)

Inavyoonekana, lengo la Russia na hata China pia, -ambayo hapo kabla, katika hatua inayofanana na hii iliunga mkono msimamo wa Imarati kuhusu visiwa hivyo vitatu kupitia taarifa ya pamoja iliyotoa na nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, wakati wa ziara aliyofanya rais wake Xi Jinping nchini Saudi Arabia-, ni kustawisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara na nchi hizo kwa kuonyesha kwa namna fulani zina misimamo inayolingana na ya Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi katika masuala ya Asia Magharibi na Ghuba ya Uajemi likiwemo la visiwa vitatu. Ali Akbar Velayati, Mshauri Mwandamizi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza katika makala fupi kuhusu haki ya Iran ya kumiliki visiwa vya Bumousa, Tunb Kubwa na Tunb Ndogo na kubainisha kwamba, uungaji mkono wa Russia kwa msimamo wa nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi umetokana na "urahisi wa kuamini mambo" na kuandika: "Russia imetumbukia kwenye shimo la mtego lilelile ililotumbukia China kitambo nyuma". Akilifafanua hilo Velayati ameandika: “maana yake ni wao kudhani kwamba kwa kutilia nguvu madai hayo yasiyohusu, watakuja kuwa na uhusiano mzuri wa kiuchumi na Imarati katika siku za usoni.” Huenda ni kwa kuzingatia jambo hilo na kufuatia mijibizo iliyotolewa na viongozi na vyombo vya habari vya Iran, ndipo Moscow ikaamua kurekebisha haraka kupitia naibu waziri wake wa mambo ya nje, msimamo ghalati na usio sahihi iliotoa kuhusiana na visiwa vitatu vya Iran.../

Tags