Sura ya Adh-dhaariyaat, aya ya 1-14 (Darsa ya 954)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 954. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 50 ya Qaaf, katika darsa hii tutaanza kutoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 51 ya Adh-Dhaariyaat. Sura hii iliteremshwa Makka na ina aya 60. Maudhui kuu za aya zake ni kuhusu asili ya uumbaji na Ma'adi, yaani kufufuliwa viumbe, ishara za Mwenyezi Mungu katika ulimwengu wa uumbaji, visa vya baadhi ya Mitume na hatima iliyozipata kaumu za watu waliopotoka na waliopotea. Baada ya utangulizi huo mfupi, sasa tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya mwanzo hadi ya sita ya sura hiyo ambazo zinasema:
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa Jina la Allah Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu
وَالذَّارِيَاتِ ذَرْوًا
Naapa kwa pepo zinazo tawanya (vitu),
فَالْحَامِلَاتِ وِقْرًا
Na naapa kwa mawingu mazito,
فَالْجَارِيَاتِ يُسْرًا
Na naapa kwa merikebu zinazo kwenda kwa wepesi.
فَالْمُقَسِّمَاتِ أَمْرًا
Na naapa kwa malaika wanao gawanya (mambo) kwa amri (ya Mwenyezi Mungu),
إِنَّمَا تُوعَدُونَ لَصَادِقٌ
Hakika mnayo ahidiwa bila ya shaka ni kweli,
وَإِنَّ الدِّينَ لَوَاقِعٌ
Na kwa hakika (siku ya) malipo bila ya shaka itatokea.
Sura hii kama zilivyo baadhi ya sura zingine za Qur’ani inaanza kwa viapo kadhaa: kiapo cha kwanza ni cha kuapiwa vitu vya maumbile kama mawingu na upepo ambavyo ni sababu za kunyesha mvua inayopelekea kuota mimea na miti na kupatikana uhai na maisha ya wanadamu katika maeneo mbalimbali ya sayari ya dunia. Kiapo cha pili ni kuapiwa merikebu na vipando vya baharini vinavyoelea majini; na kutokana na kuvuma kwa upepo, husafirisha abiria na bidhaa kutoka sehemu moja hadi nyingine ya dunia. Kiapo cha tatu cha aya hizo ni cha kuapiwa malaika ambao wana jukumu la kugawanya riziki za wanadamu ulimwenguni kote. Hakuna shaka maisha ya viumbe wanadamu, wanyama na mimea yanategemea kunyesha kwa mvua; nazo pepo zina mchango na nafasi muhimu katika kuyasukuma mawingu kutoka sehemu moja hadi nyingine, kuifanya hewa iwe na ukadiri na wastani na katika urutubishaji wa mimea. Merikebu, meli na majahazi, nazo pia zinatoa mchango muhimu katika maisha ya wanadamu. Ukweli ni kwamba njia za majini na baharini ndizo njia nyingi na pana zaidi, tena nyepesi na za gharama ndogo zaidi kwa ajili ya kusafirisha bidhaa na shehena nzito za mizigo kutoka sehemu moja hadi nyingine. Kwa hakika na yakini, viapo hivi vya Qur’ani tukufu vinabainisha qudra, tadbiri, hekima na uwezo wa Allah SWT katika uendeshaji wa masuala ya maisha ya wanadamu, ili wale wanaokanusha ufufuo wajue kwamba baada ya Mwenyezi Mungu kuuumba ulimwengu, hakuuacha tu vivi hivi, bali aliuwekea ghaya na lengo kuu maalumu; lengo ambalo litathibiti katika ulimwengu wa baada ya kifo; na ahadi ya kuthibiti kwake ilitolewa na Mitume kwa watu katika zama zote za historia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuapiwa vitu mbalimbali vya ulimwengu wa maumbile kama mawingu, upepo na mvua kunamshajiisha mwanadamu afanye ugunduzi wa kanuni za ulimwengu wa maumbile na hekima na utaratibu unaotawala katika uendeshaji wa ulimwengu huo. Kuvitambua vitu hivyo na kanuni zinazotawala katika uendeshaji wake ni utangulizi wa kumjua Allah SWT. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Mwenyezi Mungu Jalla Jalaaluh anauendesha ulimwengu huu kwa kutumia sababu na visababishi vikiwemo vya vitu vya kimaada na visivyo vya kimaada. Wa aidha aya hizi zinatutafakarisha kwamba, miongoni mwa mambo ya kustaajabisha ni kuona sisi wanadamu tunaamini ahadi tunazopewa na huyu na yule hata kama ni za ubabaishaji, lakini hatuiamini ahadi ya yakini na isiyo na chembe ya shaka tunayopewa na Allah SWT!!
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya saba hadi ya tisa ya sura yetu ya Adh-Dhaariyaat ambazo zinasema:
وَالسَّمَاءِ ذَاتِ الْحُبُكِ
Naapa kwa mbingu zenye umbile zuri na njia nyingi,
إِنَّكُمْ لَفِي قَوْلٍ مُّخْتَلِفٍ
Hakika nyinyi bila ya shaka mko (mnatangatanga) katika kauli inayo khitalifiana (juu ya Qur’ani).
يُؤْفَكُ عَنْهُ مَنْ أُفِكَ
Anageuzwa kutokana na haki mwenye kugeuzwa.
Katika mwendelezo wa yale yaliyozungumziwa kwenye aya zilizotangulia, aya hizi zinaanza kwa kuapia adhama ya mbingu; mbingu ambayo inabeba mamilioni ya galaksi na nyota; nyota ambazo katika giza la usiku hutoa mwangaza ulio mithili ya taa zing’arazo na zenye kupendeza zinazotandawaa na kusambaa kwenye anga ya mbingu. Lakini pamoja na yote hayo na pasi na kuzingatia tadbiri na irada ya Allah katika mbingu na ardhi, wale wakanushao asili ya uumbaji na maadi, yaani marejeo ya viumbe, wana shaka juu ya kuteremshwa wahyi kwa Mitume na hutafuta visingizio na vijisababu hivi na vile ili kuwatia ila na kasoro Manabii hao wa Allah na mafundisho waliyokuja nayo. Ni wazi kwamba wakadhibishaji hao si watu wenye mantiki madhubuti wala uthabiti wa itikadi, kwa hivyo misimamo yao ni ya kuyumbayumba na kauli zao ni zenye kugongana. Lakini kinyume na misimamo ya watu hao, njia ya haki ni moja na imesimama juu ya msingi wa mantiki wadhiha na ya wazi kabisa na misimamo imara na thabiti. Na hapana shaka kuwa, mtu yeyote atakayeitambua haki, kisha akaipinga na kuipa mgongo atakuwa amepotoka; na hatua yake hiyo itakuwa sababu ya kuselelea kwenye dhalala na upotofu mkubwa zaidi. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kauli za wanaokanusha maadi na kufufuliwa viumbe hazina hoja na mantiki madhubuti na ndio maana kauli zao hizo huwa ni za kutupatupa na wakati mwingine huwa na mikinzano na migongano. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, njia ya uongofu iliyonyooka ni moja tu, lakini njia za dhalala na upotofu ni nyingi mno. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tujue kwamba, mtelezo, kosa na dhambi moja ni utangulizi wa mtu kupotoka, kuteleza na kutumbukia kwenye lindi la madhambi mengine na kuifanya njia ya yeye kurudi kwenye haki iwe ngumu zaidi.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 10 hadi ya 14 ya sura yetu ya Adh-Dhaariyaat ambazo zinasema:
قُتِلَ الْخَرَّاصُونَ
Wazushi wameangamizwa.
الَّذِينَ هُمْ فِي غَمْرَةٍ سَاهُونَ
Ambao wameghafilika katika ujinga.
يَسْأَلُونَ أَيَّانَ يَوْمُ الدِّينِ
Wanauliza: Ni lini hiyo siku ya malipo?
يَوْمَ هُمْ عَلَى النَّارِ يُفْتَنُونَ
Hiyo ni siku watakayo adhibiwa Motoni.
ذُوقُوا فِتْنَتَكُمْ هَٰذَا الَّذِي كُنتُم بِهِ تَسْتَعْجِلُونَ
(Wataambiwa) onjeni adhabu yenu! Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyahimiza.
Aya hizi zinaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizotangulia na kueleza kwamba kauli za wakanushaji wa kufufuliwa viumbe zinatokana na dhana na makisio tu yasiyo na mashiko na uongo na uzushi wa watu hao waliozama kwenye lindi la ujinga na kujisahau, huku wenyewe wakijihisi na kujiona ni watu waliotaalamika na watambuzi wakubwa wa mambo. Moja ya masuali ambayo aghalabu ya wakanushaji wa maadi walikuwa wakiwauliza Mitume na waumini ni: hicho Kiyama kitatokea lini hasa? Watu hao walikuwa wakidhani, kwa kuwa waumini hawaujui wakati halisi wa kujiri kwa Kiyama, basi jambo hilo halipo. Hali ya kuwa hiyo ni hoja nyepesi mno, kwa sababu kutojua sisi ni wakati gani tetemeko la ardhi litatokea, si hoja ya kuthibitisha kwamba tukio hilo halitajiri. Ukweli ni kwamba, watu hao hawataamini kufufuliwa hadi siku watakapokuja kuuhisi ndani ya miili yao uchungu wa Moto wa Jahannamu; na kwa sasa hawataacha kuwakejeli na kuwafanya stihzai waumini kwa masuali hayo ya kipuuzi na yasiyo na maana. Baadhi ya tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, kauli za kifidhuli na zisizo na mantiki kuhusiana na dini, ambazo hazina mashiko ya kielimu bali zinatokana na dhana na makisio tu huwa sababu ya mtu kuwekwa mbali na rehma za Mwenyezi Mungu. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kwamba, kutokuwa na uelewa na ufahamu kamili wa baadhi ya hali, mazingira na matukio ya Siku ya Kiyama hakutupi kisingizio cha kutilia shaka asili ya maadi na kufufuliwa viumbe. Kama ambavyo baadhi ya watu hutumia kisingizio hicho kukanusha na kukadhibisha asili ya jambo hilo. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 954 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azijaze nyoyo zetu imani ya yakini juu ya Kiyama, imani ambayo itatuwezesha kufanya yale yanayomridhisha Yeye Mola wetu na kujiepusha na yale yanayomghadhibisha. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/