Aug 10, 2023 02:24 UTC
  • Alkhamisi, Agosti 10, 2023

Leo ni Alkhamisi tarehe 23 Mfunguo Nne Muharram 1445 Hijria mwafaka na tarehe 10 Agosti 2022.

Katika siku kama ya leo miaka 236 iliyopita aliaga dunia Allamah Mulla Muhammad Mahdi Naraqi, mwanazuoni na msomi mkubwa wa Kiislamu. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali nchini Iran, msomi huyo mkubwa alielekea Hauza ya Najaf nchini Iraq kwa lengo la kuzidisha elimu ya kidini na alipata elimu kwa walimu mashuhuri wa zama hizo. Baada ya hapo Allamah Mulla Mahdi Naraqi alianza kufanya utafiti, kufundisha na kuandika vitabu. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya Allamah Naraqi ni "Jamiul Sa'adat" na " Anisul Muwahhidin".

Allamah Mulla Muhammad Mahdi Naraqi

Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita, yalitiwa saini makubaliano yaliyojulikana kwa jina la The Treaty of Sèvres kati ya utawala wa Othmaniya uliokuwa umeshindwa katika Vita vya Kwanza vya dunia na waitifaki wake. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, utawala wa dola ya Othmaniya ulipoteza karibu asilimia 80 ya ardhi yake iliyokuwa ikiitawala, na kupunguza eneo ililokuwa ikilitawala kutoka kilomita mraba milioni tatu hadi kilomita mraba laki sita tu. Makubaliano hayo yalitambua rasmi makubaliano ya awali ya Ufaransa na Uingereza juu ya kugawana ardhi iliyokuwa ikitawaliwa na dola ya Othmania, ambapo Uingereza ilizitawala Iraq, Jordan na Palestina na Ufaransa nayo ilizitwaa na kuzidhibiti Syria na Lebanon. 

Siku kama ya leo miaka 86 iliyopita, vilianza vita vya miaka miwili kati ya Japan na China juu ya mzozo wa maeneo ya Yangtze na Canton ambayo yalikuwa maeneo ya kistratijia ya ardhi ya China. Canton ilikuwa bandari muhimu mno huko kusini mwa China ambayo Wachina walipigana vita vya miaka miwili kuilinda mbele ya uvamizi wa Wajapani. Hata hivyo na baada ya kupata hasara kubwa tarehe 25 Aprili 1939 bandari ya Canton ikatwaliwa na Japan. Utawala wa Japan uliendelea kujipanua katika ardhi ya China kwa kudhibiti maeneo mengine ya mashariki mwa nchi hiyo baada ya kuanza Vita vya Pili vya Dunia. Hata hivyo Wajapani walilazimika kurudi nyuma kutokana na mapambano makali ya wananchi wa China. 

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, kufuatia kushindwa kikamilifu Japan katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kwa mujibu wa maazimio ya Kongamano la Potsdam, maeneo ya kaskazini mwa Korea yalidhibitiwa na Jeshi Jekundu la Urusi ya Zamani. Kabla ya kushindwa Japan, maeneo hayo yalikuwa chini ya udhibiti wa nchi hiyo. Aidha baada ya siku chache maeneo ya kusini ya Korea yalidhibitiwa na Marekani. Kudhibitiwa maeneo ya kaskazini na kusini ya Korea ulikuwa utangulizi wa kugawanywa ardhi hiyo katika nchi mbili za Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini. 

Katika siku kama hii ya leo miaka 18 iliyopita, Haram ya maimamu wawili, Ali al Hadi na Hassan al Askakri (as) huko Samarra, nchini Iraq walikozikwa wajukuu hao wawili wa Mtume Muhammad (saw) iliharibiwa na Mawahabi wa Kitakfiri wenye mafungamano na al-Qaeda.

Magaidi wa kitakfiri, wakiongozwa na Abu Musab al Zarqawi, siku ya Jumatano, tarehe 23 ya Muharram 1427 mwendo wa saa 7:00 asubuhi, wakiwa wamevalia sare za askari wa Iraq, waliingia kwenye haram ya maimamu hao wawili na kuteka silaha za walinzi na pamoja na watumishi wa eneo hilo takatifu, na kulipua eneo hilo kwa kutumia milipuko ya TNT yenye uzito wa kilo 200. Nguvu ya mlipuko huu ilikuwa kubwa sana kiasi kwamba baadhi ya vifaa na jengo hilo nje vilirushwa umbali wa nusu kilomita.

Samarra

 

Tags