Sep 09, 2023 02:18 UTC
  • Jumamosi, 09 Septemba 2023

Leo ni Jumamosi tarehe 23 Mfunguo Tano Safar 1445 Hijria mwafaka na tarehe 9 Septemba 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1451 iliyopita kulianza vita maarufu kwa jina la vita vya miaka saba kati ya madola mawili yaliyokuwa na nguvu ya Iran na Roma, baada ya mfalme Justinian wa Roma kuanzisha mashambulizi yaliyokuwa na lengo la kulikalia eneo la magharibi mwa Iran. Baada ya miaka saba ya vita mfalme wa Iran Anushirvan alimshinda mfalme Justinian wa Roma na hivyo mfalme huyo akalazimika kujiuzulu. Baada ya kujiuzulu mfalme Justinian mfalme Tiberius alishika mamlaka ya utawala wa Roma. Vita hivyo vilimalizika mwaka 579 baada ya Waroma kukubali kuilipa Iran gharama inayofikia sarafu za dhahabu elfu 45. ***

 

 

Katika siku kama hii ya leo miaka 195 iliyopita alizaliwa Leo Tolstoy, mwandishi na mwanafasihi raia wa Russia. Awali Tolstoy alijiunga na jeshi la Qaukasia na katika kipindi hiki ndipo alipoandika kitabu chake cha kwanza alichokupa jina la "Childhood". Mwandishi huyo wa Russia baadae alijiengua jeshini na kutumia muda wake wote kwa ajili ya kusoma na kuandika. Miongoni mwa vitabu muhimu vya mwandishi Leo Tolstoy ni "Vita na Amani", "Waqazaki" na "Hadji Murad." Tolstoy alifariki dunia mwaka 1910. ***

 

Miaka 144 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia msomi mkubwa na mtaalamu wa fiq'hi wa Kiislamu Sheikh Muhammad Baqir Agha Najafi Isfahani. Sheikh Agha Najafi alizaliwa mnamo mwaka 1234 Hijiria nchini Iran na baada ya kusoma elimu mbalimbali za kidini mjini Isfahan, alielekea Najaf huko Iraq kwa ajili ya kukamilisha masomo yake. Baada ya kurejea kutoka Najaf msomi huyo aliweka makazi yake mjini Isfahan na kujikita katika kufundisha na kuwalea wanafunzi sambamba na kuandika vitabu. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni pamoja na "Lubbul-Fiq'h" na "Lubbul-Usuul." ***

Sheikh Muhammad Baqir Agha Najafi Isfahani.

 

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita yaani tarehe 9 Septemba 1945, ulitiwa saini mkataba wa kusalimu amri vikosi vya Japan vilivyokuwa vimeidhibiti na kuikalia kwa mabavu China. Kwa mujibu wa mkataba huo askari milioni moja wa Japan waliweka chini silaha zao kwa amri ya Hirohito mfalme wa wakati huo wa Japan. Kwa utaratibu huo vita vya kihistoria kati ya China na Japan vikafikia tamati. ***

Mkataba wa kusalimu amri vikosi vya Japan

 

Katika siku kama ya leo 54 iliyopita  alifariki dunia Jalal Aal Ahmad, mwandishi na mkosoaji wa Kiirani. Aal Ahmad alizaliwa mwaka 1302 Hijria Shamsiya jijini Tehran. Mwaka 1325, Jalal al Ahmad alitunukiwa shahada ya fasihi ya Chuo Kikuu cha Tehran. Aliingia katika uwanja wa siasa wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na akaanza kuandika magazeti. Alijishughulisha na kuandika makala na ukosoaji na hadithi fupifupi. Jalal Aal Ahmad alikuwa hodari katika kuandika visa na hekaya fupifupi. ***

Jalal Aal Ahmad

 

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, aliaga dunia Mao Zedong kiongozi wa Uchina. Mao Zedong alizaliwa mwaka 1893 na mwaka 1921 aliunda chama cha Kikomonisti cha Uchina baada ya kuungwa mkono na wafuasi wa fikra zake. Mao alikuwa akisisitiza suala la kuwatetea na kuwalinda wanavijiji na kwa sababu hiyo ilipata uungaji mkono mkubwa wa wanavijiji wa Uchina. ***

Mao Zedong

 

Tags