Sep 17, 2023 14:36 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (27)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 27 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama zilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha. Ni matumaini yetu mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 27.

امْشِ بِدَائِکَ مَا مَشَى بِکَ

Enenda na maumivu yako kwa namna yanavyoendana nawe.

Katika Hikma ya 27 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anatukumbusha kwenye kanuni muhimu ya afya na matibabu akisema: امْشِ بِدَائِکَ مَا مَشَى بِکَ Enenda na maumivu yako kwa namna yanavyoendana nawe. Maadamu inawezekana kuyabeba maumivu, fanya hivyo, nenda nayo, usisalimu amri.

Kama mnavyojua wapenzi wasikilizaji, maumivu ni ishara kwamba mfumo wa mwili umeshambuliwa na mwili sasa umo vitani katika kujihami mbele ya shambulio hilo. Baadhi ya wakati pambano hilo hujitokeza kwa sura ya homa, kichomvi, uvimbe na vitu kama hivyo.

Leo, imethibitishwa katika sayansi ya matibabu kwamba kila wakati mtu anapokuwa na maumivu hata kidogo tu anakimbilia kujitibu haraka, mfumo wa kujilinda na maradhi wa mwili wake huwa unapungua. Kwa kweli, Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu na mfumo wa asili ambao una uwezo mkubwa wa kukabiliana na magonjwa. Iwapo mtu atachunga vizuri kanuni za afya, lishe bora na kuupa mwili wake nafasi ya kujihami, basi huusaidia mwili wake huo kukabiliana na maradhi mengi. Fauka ya hayo ni kuwa, maradhi mengi huwa yana muda wake maalumu, muda wake huo ukiisha, maradhi hayo hupungua nguvu yenyewe kwa yenyewe.  

Baadhi ya wakati, mtu anapofanya haraka kula dawa, huuzowesha mwili wake kutegemea dawa muda wote na kukosa nguvu za kujihami, na wakati dawa hizo zinapouzoea mwili, hupoteza athari zake na mtu kulazimika kuongeza dozi kwa ugonjwa ambao huenda ungeweza kutibika bila ya hata kula dawa yoyote. Hivyo, ni wazi kwamba, mtu kufanya haraka kutumia dawa au kwenda kwa daktari hata kwa magonjwa madomadogo, kuna madhara kwake, badala ya kuwa na faida. Matumizi ya kiholela ya madawa ya kemikali huongeza madhara kwa mwili wa mwanadamu na kumpokonya kinga ya asili ya mwili. Imam Ali AS anasema katika barua ya 31 ya Nahjul Balagha kwamba: Ni dawa ngapi ambazo zenyewe huwa ugonjwa na si tiba. Tunapoyazingatia hayo tutazidi kuona uhumimu wa hikma za Imam Ali AS ndani ya Nahjuli Balagha. 

Wakati mtu anapokata tamaa, akasalimu amri mbele ya ugonjwa mdogo tu, huwa anazidisha ugonjwa huo ni kujikubaliasha kuwa hawezi kuvumilia. Huo wenyewe ni ugonjwa wenye madhara mengi. Lakini kama atasimama imara, akaanza kufanya kazi zake na kutoiruhusu akili yake iamini kuwa yu mgonjwa, hatua hiyo huleta athari kubwa na kuupa nguvu mwili ya kukabiliana na ugonjwa huo na kuushinda. Katika sehemu nyingine pia, Imam Ali AS amenukuliwa akisema, "Usilale kitandani maadamu unaweza kusimama kwa miguu yako kukabiliana na ugonjwa."

Tab'an inabidi tuzingatie hapa kwamba, maneno hayo hayana maana kuwa, mtu anapoumwa asiende kwa daktari au akwepe kula dawa, hapana, bali maana yake ni kuwa, mtu asifanye pupa ya kukimbilia kwa daktari na kula dawa hata ugonjwa mdogo tu. Dawa zenyewe zina madhara mengi ya pembeni. Kadiri mtu atakavyoweza kuachia mwili wake ujihami wenyewe ni bora kulikoni kuingiza ndani yake dawa za kemikali hata kwa magonjwa madogo sana.