Sep 17, 2023 16:21 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (79)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ili tuweze kwa pamoja kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu

 

Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 79 ya mfululizo huu kitamzungumzia Ayatullah Ali Qadhi. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Ilikuwa imepita miaka mingi ambapo Ayatullah Seyyid Hussein Qadhi alikuwa amemwomba Mwenyezi Mungu amjalie na kumruzuku mtoto wa kiume. Yeye, ambaye alikuwa mmoja wa maseyyid na masharifu wa Tabataba'i na wanachuoni mashuhuri wa Tabriz, alikwenda kwenye haram ya Imamu Husein (a.s.) kwa matumaini ya kutimiziwa haja yake na akamfanya Habib bin Mudhahir kama mwombezi wake mbele ya Mwenyezi Mungu kupitia kwa Imam Hussein (as).

Haukupita muda mrefu Mwenyezi Mungu akaikubali nadhiri yake kwa uombezi wa Seyyid al-Shuhadaa (a.s.) na akamruzuku Seyyid Husein mtoto wa kiume ambaye baadaye alikuja kuwa chanzo cha fahari na heshima kwa familia yake. Tarehe 13 Dhul-Hijjah 1285 Hijria mwafaka na 1868 Miladia ilikuwa siku ya kukumbukwa na maridhawa mno kwa Seyyed Hussain Qadhi na mkewe. Waliamua kumwita mtoto wao "Ali" na wakampeleka shuleni tangu utoto wake kujifunza Qur'an na mambo ya msingi. Seyyed Ali, ambaye alikuwa na akili, upeo na kipaji cha hali ya juu, alimaliza masomo yake ya msingi mapema zaidi kuliko watoto wa rika lake na akaingia Hawza ya Tabriz.

Mnamo mwaka 1308 Hijria sawa na 1890 Miladia akiwa na umri wa miaka 23, alifunga safari na kwenda katika Hawza ya Najaf Iraq na kuufanya mji huo kuwa makazi yake hadi mwisho wa maisha yake. Sambamba na kusoma masomo ya dini, pia alitilia maanani sana suala la kulea nafsi.

Tangu akiwa mdogo, alianza safari ya kulea nafsi kwa mujibu wa elimu ya irfani (kumtambua Mwenyezi Mungu) alipokuwa akisoma kwa baba yake, na alipoingia Najaf, alijisalimisha na kujikabidhi kwa Imamu Ali (as) ili amuonyeshe njia ambayo ndani yake kuna ridhaa za Mwenyezi Mungu na Imam alifanya hivyo. Imamu kwa upande wake kwa hakika alitekeleza haki ya baba kwa mwanawe kwa namna ambayo, Seyyid Ali Qadhi akiwa Najaf aliweza kustafidi vyema na uhudhuriaji wake wa masomo kwa walimu mahiri wa zama hizo na wakubwa na akaondokea kuwa mbobezi wa elimu ya irfan akiwa mashuhuri pia kwa makarama. Akiwa na umri wa miaka 27, alifikia daraja ya ijtihad na akaanza kuandika na kufundisha.

Seyyid Ali Qadhi alikuwa akishikamana na adabu za Sharia, kufanya mambo yanapendekezwa yaani mustahabu, na kuepuka yale yanayochukiza yaani makuruhu. Hii ndiyo sababu iliyomfanya ajumuishwe katika neema na mapenzi ya Mwenyezi Mungu na hivyo kufikia viwango vya juu vya irfani na kumtambua Mola Muumba na akakaribia hadhi ya mwanadamu mkamilifu.

 

 

Nafasi na daraja ambayo ilimpa uwezo wa kupenya katika nyoyo za wengine kwa vitendo na maneno yake na kuwaongoza kwenye njia sahihi. Aliwafundisha wanafunzi, ambao kila mmoja wao alifikia daraja za juu katika uwanja wa maadili na irfani. Watu kama Ayatullah Seyyid Muhammad Hussein Tabatabai, Ayatullah Muhammad Taqi Behjat, Sheikh Abbas Quchani na wengineo ni miongoni mwa wanafunzi.

Seyyid Ali Qadhi daima aliwahimiza wanafunzi wake kusoma falsafa na irfani ya kinadharia, na katu hakuwahi kutosheka na kufundisha kinadharia tu, bali alikuwa pamoja na wanafunzi wake kivitendo katika kupita hatua na marhala za kiirifani na kulea nafsi.

Kwake yeye haikuwa ikijalisha kama wanafunzi walikuwa mbele yake au la, kwa vyovyote vile, alikuwa anajua hali yao, aliangalia tabia na matendo yao, na kila inapobidi, alitoa ushauri wa kimaadili na kiirifani kwa kila mwanafunzi kwa faragha kulingana na hali ya kila mwanafunzi.

Allama Muhammad Hussein Tabatabai, mmoja wa wafasiri wakubwa wa zama hizi wa falsafa ya Mulla Sadra, anasema hivi kuhusu mwalimu wake, Ayatullah Qadhi: “Katika hali ya kawaida, alikuwa akipatikana kwa muda wa siku kumi au ishirini, marafiki walikuwa wakija na kuondoka, na kulikuwa kukipita mazungumzo baina yao na kisha ghafla moja alikuwa akitoweka na kwa siku kadhaa hakukuwa na habari yoyote kuhusiana na yeye; hakukuwa na habari zake  si nyumbani, wala shuleni, au msikitini huko Kufa.

Siku chache baadaye, alikuwa akionekana na kuendesha masomo na vikao vya faragha nyumbani na shuleni. Alikuwa namna hii na alikuwa na hali ya ajabu na ya kushangaza. Katika siku hizi, ustadhi huyu alikuwa akijishughulisha na kulea nafsi na alikuwa amefikia hatua ambayo inaweza kuelezwa kwamba alikuwa khalifa wa Mwenyezi Mungu na alikuwa akifanya kazi za makhalifa wa Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Seyyid Ali Qadhi alikuwa akiamini kwamba, ustahimilivu na subira katika kumtafuta na kumuendea Mwenyezi Mungu ni sababu ya kudiriki jina kuu la Mwenyezi Mungu na ni watu wastahiki tu ndio wanaoweza kufikia daraja ya kufahamu siri za Mola Muumba.

Ayatullah Qadhi alikuwa akizingatia mno suala la kuswali Sala wakati wa awali na alifungamana mno na jambo hilo.

 

Aidha mwanazuoni huyo alijifunga mno na suala la kusali Sala za usiku. Kwa mtazamo wake ni kwamba, kila kitu mukhtarasi wake ni katika Sala za usiku. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana alikuwa akiwanasihi na kuwasisitizia sana wanafunzi wake juu ya suala la kushikamana na Sala za usiku. Alikuwa akiwaambia: Kama mnataka dunia salini Sala za usiku, kama mnataka akhera basi salini pia Sala za usiku.

Alikuwa akipenda mno kusali na kufanya ibada katika misikiti ya Kufa na Sahla na alikuwa na chumba maalumu katika misikiti hiyo kwa ajili ya kufanya ibada na kumtaaradhia Mola wake Muumba.

Sifa nyingine muhimu aliyosifika nayo mwanazuoni huyu ni tabia njema, kutenda wema na hisani na maingiliano mazuri na watu aliyokuwa nayo ambayo ni ya kupigiwa mfano. Akiwa nyumbani alikuwa mpole sana kwa mkewe na wanawe na daima alikuwa akijichunga akichelea kwamba, ibada zake zisije kuikwaza familia yake.

Kuwa na makarama ni sifa nyingine aliyofahamika nayo Sayyid Ali Qadhi ambapo inanukuliwa kwamba, kuna wakati alikuwa akitoa habari ya matukio ya baadaye. Moja ya matukio aliyotabiri ni kutokea Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa uongozi wa Imam Khomeini.

Ayatullah Sheikh Abbas Qochani ambaye ni mmoja wa wanafunzi wa Sayyid Qadhi anasimulia kwamba: Tulipokuwa Najaf al-Ash'raf (Iraq) tulikuwa na vikao na Ayatullah Qadhi, na aghalabu watu walikuwa wakiingia kwa uratibu na sote tulikuwa tukifahamiana na kujuana. Katika kikao kimoja, ghafla aliingia Sayyid mmoja kijana ambaye sisi hatukuwa tukimfahamu. Mwalimu akakatisha mazungumzo yake na akaonyesha heshima na taadhima kubwa kwa Sayyid yule kijana na kumwambia: Sayyid Ruhullah! Ni lazima kusimama dhidi ya watawala madhalimu, ni lazima kusimama kidete ni lazima kupambana na ujahili. Hii ni katika hali ambayo, hakukuwa na habari zozote kuhusiana na Mapinduzi ya Iran. Tulishangazwa mno na maneno haya ya mwalimu wetu. Hata hivyo baada ya miaka mingi na baada ya kutokea Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran tulikuja kufahamu siku ile maneno ya mwalimu wetu yalikuwa na maana gani na kwa alionyesha heshima kwa Imam Khomeini.

Ayatullah Sayyid Ali Qadhi aliaga dunia 1946 Miladia akiwa na umri wa miaka 81 baada ya kuugua. Kaburi la mwanazuoni huyu linapatikana katika makaburi ya Wadi Salaam huko Najaf Iraq.

Wapenzi wasikilizaji, muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.

Asanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.