Sep 26, 2023 08:22 UTC
  • Sura ya Al-Qamar, aya ya 9-22 (Darsa ya 970)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 970 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 54 ya Al-Qamar. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya tisa hadi ya 12 ya sura hiyo ambazo zinasema:

كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ فَكَذَّبُوا عَبْدَنَا وَقَالُوا مَجْنُونٌ وَازْدُجِرَ

Kabla yao, kaumu ya Nuhu (pia) walikadhibisha; walimkadhibisha mja wetu, na wakasema ni mwendawazimu, na akazuiwa (kwa maudhi na vitisho).

فَدَعَا رَبَّهُ أَنِّي مَغْلُوبٌ فَانتَصِرْ

Ndipo akamwomba Mola wake Mlezi akasema: Kwa hakika mimi nimeshindwa, basi ninusuru!

فَفَتَحْنَا أَبْوَابَ السَّمَاءِ بِمَاءٍ مُّنْهَمِرٍ

Basi tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayo miminika.

وَفَجَّرْنَا الْأَرْضَ عُيُونًا فَالْتَقَى الْمَاءُ عَلَىٰ أَمْرٍ قَدْ قُدِرَ

Na tukaipasua ardhi kwa chemchem, yakakutana maji kwa jambo lilio kadiriwa.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia hali ngumu na ya kutisha itakayowakabili wakanushaji wa haki Siku ya Kiyama. Aya hizi tulizosoma zinagusia baadhi ya adhabu zitakazowafika watu hao hapa duniani na kueleza kwamba, Nabii Nuh AS, kama walivyokuwa Mitume wengine, aliwalingania watu wake wito wa Tauhidi wa kumwamini na kumwabudu Mungu mmoja tu wa haki na akawaonyesha miujiza kadhaa kutihibitisha ukweli wa Utume wake, lakini wale ambao hawakuwa tayari kuikubali haki walimwita Mtume wao huyo mwendawazimu aliyeathiriwa na majini na kwamba akili yake pia imedumazwa. Makafiri hao walitoa vitisho kwa Nabii Nuh kwamba watampiga mawe na kumuua. Mbali na kumfanyia vitimbi na maudhi chungu nzima, waliuwekea kila aina ya vizuizi wito wa Mtume huyo ili yeye aache kufikisha ujumbe aliopewa na Mola wake na awaache wao kama walivyo waendelee na mambo yao. Ilipofikia hatua hiyo, Nabii Nuh AS alimwomba Allah amnusuru na shari ya wakadhibishaji hao wa haki. Na kwa kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa ameshatimiza dhima kwa watu hao na hawakuwa tayari kuifuata haki, aliwateremshia adhabu ya gharika kubwa na ya kutisha iliyosomba na kuangamiza kila kitu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuwaita Mitume wendawazimu ni miongoni mwa tuhuma zilizozoeleka katika zama zote za historia. Wapinzani watenda maovu wamejaribu sana kutumia silaha hiyo ili kuharibu shakhsia za Manabii hao wa Allah. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wanachopaswa kufanya waumini ni kutimiza wajibu wao; na hata pale wanapokuwa wameshindwa na maadui zao wasivunjike moyo wala kukata tamaa kwa sababu qudra na nguvu za Allah ziko juu ya nguvu zingine zote. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, mvua, ambayo ni dhihirisho la huruma na rehma za Allah, wakati mwingine huwa sababu ya watu kupatwa na ghadhabu na adhabu ya Mola.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 13 hadi ya 17 ya sura yetu ya Al-Qamar ambazo zinasema:

وَحَمَلْنَاهُ عَلَىٰ ذَاتِ أَلْوَاحٍ وَدُسُرٍ

 Na tukamchukua kwenye ile (safina) ya mbao na misumari.

تَجْرِي بِأَعْيُنِنَا جَزَاءً لِّمَن كَانَ كُفِرَ

Ikawa inakwenda kwa uangalizi wetu, kuwa ni malipo kwa (Mtume) aliyekuwa amekanushwa.

وَلَقَد تَّرَكْنَاهَا آيَةً فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ

Na bila ya shaka tuliiacha iwe ni Ishara. Lakini je, yupo anaye kumbuka? 

‏ فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ

Basi ilikuwaje adhabu yangu, na maonyo yangu!

وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ

Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur'ani iwe nyepesi kuikumbuka; basi je yupo anaye kumbuka?

Kabla Mwenyezi Mungu hajawateremshia adhabu watu wa kaumu ya Nuh, alimwamuru Mtume wake huyo achonge jahazi kubwa ili aweze kupakia ndani yake aina mbalimbali za wanyama pia na kuepusha vizazi vyao visije vikatoweka. Hiyo ilikuwa ishara kwamba, dhoruba na gharika kubwa ilikuwa inakuja kusomba na kuangamiza sehemu kubwa ya ardhi; vyenginevyo kusingekuwapo na haja ya kufanya hivyo. Ilipoanza gharika hiyo, kwa amri ya Mwenyezi Mungu, jahazi la Nabii Nuh AS lilianza kukata mawimbi na wote waliokuwa wameabiri ndani yake waliokoka, lakini makafiri wote waligharikishwa. Hatimaye baada ya maji kudidimia ardhini, waliokuwemo jahazini walishuka kutoka kwenye safina hiyo salama usalimini. Pamoja na hayo, mabaki ya jahazi hilo kubwa la Nuh AS yaliyojumuisha mbao na misumari, yaliendelea kubaki kwa irada ya Allah ili iwe alama ya qudra na uwezo wa Mola na ili wakanushaji wa haki wajue kwamba adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali, kwa hivyo wayahadhari mno maonyo wanayopewa na Mitume. Kusimuliwa kisa hiki ndani ya Qur'ani, bila shaka kumefanywa kwa madhumuni ya kutoa ukumbusho ili watu wapate ibra na mazingatio na waache kuifanyia haki ubishi na ukaidi. Katika aya ya mwisho tuliyosoma, imeelezwa kwamba Qur'ani imefanywa kuwa nyepesi. Na hilo halina shaka, kwamba namna utamkaji wa maneno ya Qur'ani ulivyo unaufanya usomaji wake uwe rahisi, lakini pia mwepesi na wa kuvutia. Muhtawa na yaliyomo kwenye aya zake pia yanajumuisha visa na mifano, inayoyafanya yanayozungumziwa ndani yake yawe rahisi kukubalika. Lakini pamoja na Qur'ani kuwa nyepesi, maneno yake ni mazito na madhubuti. Aidha, licha ya aya zake kuwa nyepesi, zimepangwa kwa namna ambayo, hata kama weledi na wajuzi wote wa elimu wataungana na kushirikiana pamoja, hawataweza katu kuleta maneno yanayoshabihiana na Qur'ani. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, anapotaka Allah, vipande vya miti na mbao huweza kumhifadhi mtu kwenye tufani na dhoruba kali, kama ambavyo Nabii Musa AS pia aliokolewa na fimbo ya mti kwenye tufani ya mawimbi ya Mto Nile. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mtu yeyote anayekufuru na kuonyesha utovu wa shukurani kwa neema ya uwepo wa Mitume, hufikwa na adhabu hapa duniani na huko akhera. Vilevile aya hizi zinatuonyesha kwamba, kama mwili wa Firauni ulivyoopolewa majini na kubakishwa, jahazi la Nuh AS pia lilibakishwa ili liwe ibra na mazingatio kwa watakaofuatia. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tufahamu kuwa Qur'ani ni kitabu chepesi na rahisi kufahamika, lakini pamoja na kuwa hivyo, hakuna mtu yeyote awezaye kuleta mfano wake, hata kama walimwengu wote watashirikiana pamoja katika jambo hilo.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 18 hadi ya 22 ya sura yetu ya Al-Qamar ambazo zinasema:

كَذَّبَتْ عَادٌ فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ

Kina A'di (pia) walikadhibisha. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu? 

إِنَّا أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ رِيحًا صَرْصَرًا فِي يَوْمِ نَحْسٍ مُّسْتَمِرٍّ

Hakika Sisi tuliwapelekea upepo mkali katika siku ya nuhsi iendeleayo,

تَنزِعُ النَّاسَ كَأَنَّهُمْ أَعْجَازُ نَخْلٍ مُّنقَعِرٍ

Ukiwang'oa watu kama vigogo vya mitende vilivyo ng'olewa.

فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ

Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu!

وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ

Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur'ani nyepesi kuikumbuka; basi je yupo anaye kumbuka?

Baada ya simulizi za yaliyoisibu kaumu ya Nabii Nuh AS, aya hizi tulizosoma zinazungumzia habari za kaumu ya A'adi. Nabii Hud AS ndiye aliyekuwa Mtume wa kaumu hiyo. Licha ya kuwapa maonyo na indhari watu wake hao, hawakuwa tayari kuacha maasi na maovu waliyokuwa wakiyafanya. Watu wa A'adi walikuwa wakimuudhi na kumfanyia stihzai kila mara Mtume wao Hud AS, na wakawa wanajivuna na kujigamba kwa kujaaliwa kuwa watu wenye nguvu na maumbo makubwa. Watu hao hawakuwa wakidhani kama itafika siku mji wao na maskani zao zitakuja kuvumiwa na upepo mkali na wa kutisha ambao utasambaratisha kwa kuvipeperusha na kuvivurumisha, viwiliwili vyao vya maungo makubwa na yenye nguvu huku na kule, mithili ya mitende iliyong'olewa mashina. Kimbunga hicho cha kutisha kiliendelea kwa muda wa juma zima na hakikusaza chochote, kuanzia nyumba za mji huo pamoja na wakazi wake. Mwenyezi Mungu SWT anarudia tena kuuliza, kwa nini hamupati ibra na kuonyeka kutokana na yaliyozisibu kaumu zilizopita, japokuwa kwa kukusimulieni ndani ya Qur'ani habari za watu wa kaumu hizo tumekurahisishieni njia ya kupatia nasaha na mawaidha kutokana na hatima iliyowafika watu hao? Baadhi ya tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, Mwenyezi Mungu ametimiza dhima kwa wanadamu kwa kuwapelekea Mitume wa kuwafikisha maonyo na indhari. Kwa hivyo wale wanaoamua kuikaidi na kuipinga haki wangojee kuona matokeo ya maovu na maasi wanayofanya. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kama yalivyo maji, upepo pia unafuata amri na irada ya Allah SWT; kwa hiyo kuna wakati huwa ni alama ya rehma za Mwenyezi Mungu, na wakati mwingine huwa ni wenzo wa adhabu kwa waovu. Atakapo Yeye Mola, upepo unaweza kuwa sababu ya uotaji na ukuaji wa kitu na unaweza pia kuwa wenzo wa maangamizi na uharibifu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, Qur'ani si kitabu cha taarikh na historia, lakini ili kuwapa watu mwongozo wa uongofu, imetaja simulizi za yaliyozipata baadhi ya kaumu na watu ili watu wote wapate mawaidha na kuacha kuikanusha na kuikadhibisha haki. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 970 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuwezeshe kuifanya Qur'ani mwongozo wa kila kitu katika maisha yetu na Siku ya Kiyama ije kuwa muombezi wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags