Oct 08, 2023 10:30 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (31)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 31 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine ya Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha. Ni matumaini yetu mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni hikma ya 31.

Wasikilizaji wapenzi, katika hikma hii ya 31 ya Nahjul Balagha, Imam Ali (AS) anatufundisha na kutufafanulia nguzo za imani. Kwa kuzingatia umuhimu mkubwa wa suala la imani na wajibu wa kuifahamu vizuri hekima hii iliyojaa mafundisho mazuri, tumeamua kuizungumzia hika hii ya 31 katika vipindi sita vya mfululizo huu tukiwa na matumaini tutaweza sote kufaidika vya kutosha.

Sote tunajua kwamba hatua ya kwanza ya mtu kuwa Muislamu ni kumwamini Mungu Mmoja. Lakini imani si kutamka kwa maneno tu, bali ni lazima imani hiyo ijikite moyoni. Imani ya moyoni ndiyo ambayo inampa mwongozo mwanadamu katika maisha yake na ina jukumu muhimu la kumuonesha njia ya namna ya kuishi hapa duniani.  Kwa maneno mengine ni kuwa, hatua ya kwanza ya kuingia katika njia ya kuwa mtumwa wa Mwenyezi Mungu ni imani na mtu aliye na imani hiyo takatifu anaitwa muumini. Lakini Imani ni nini na imejengeka kwenye misingi na nguzo zipi?

 

Cha kuvutia hapa ni kwamba swali hilo pia aliulizwa Amirul-Muuminina Ali bin Abi Talib (AS). Katika Hikma hii 31 ya Nahjul Balagha, mtukufu huyo anatoa ufafanuzi wa kuvutia sana. Anatoa vielelezo kwa njia bora ya kiubunifu. Alipoulizwa kuhusu imani, Imam alisema:

الْإِیمَانُ عَلَى أَرْبَعِ دَعَائِمَ: عَلَى الصَّبْرِ وَ الْیَقِینِ وَ الْعَدْلِ وَ الْجِهَادِ.

"Imani imesimama juu ya nguzo nne, subira na yakini, na uadilifu na jihadi.

Imepokewa katika hadithi za maasumu kwamba uhusiano uliopo baina ya subra na imani ni uhusiano wa kichwa na mwili. Kwa kweli kichwa cha mwanadamu ndiyo nguzo kuu inayoongoza mwili mzima. Kama kichwa kitatenganishwa na mwili, haupiti muda ila mfumo mzima wa ufanyaji kazi wa mwili wa mwanadamu husimama. Subira na istiqama ina nafasi hiyo hiyo katika imani. Kama subira itaondoka, imani ya mwanadamu haiwezi kuendelea kuwepo kwa muda mrefu. Bila ya subira mwanadamu hawezi kabisa kuacha kutenda madhambi. Pia hawezi kuwa na istiqama mbele ya matatizo, masaibu na matatizo yasiyo na idadi ya maisha.

Subira ni moja ya mambo muhimu ya kumpelekea mtu kuingia peponi. Kwa mujibu wa aya ya 24 ya Surat al Ra’ad, Malaika watakapokwenda kwa watu wa peponi watawaambia: Assalamu Alaikum! Amani iwe juu yenu, kwa sababu ya mlivyosubiri! Basi ni mema mno malipo ya Nyumba ya Akhera

Naam, katika sehemu nyingine ya hikma hii ya 31, Imam Ali AS anaendelea kutoa ufafanuzi kuhusu imani akisema,

 فَمَنِ اشْتَاقَ إِلَى الْجَنَّةِ سَلَا عَنِ الشَّهَوَاتِ وَ مَنْ أَشْفَقَ مِنَ النَّارِ اجْتَنَبَ الْمُحَرَّمَاتِ وَ مَنْ زَهِدَ فِی الدُّنْیَا اسْتَهَانَ بِالْمُصِیبَاتِ وَ مَنِ ارْتَقَبَ الْمَوْتَ سَارَعَ [فِی] إِلَى الْخَیْرَاتِ:

Yeyote mwenye hamu ya kuingia peponi, hujiweka mbali na matamanio ya nafsi, na yeyote anayeogopa moto, hujiweka mbali na mambo ya haramu; na kila mwenye kuitaliki dunia, hayakuzi matatizo na masaibu; na yeyote aliye na yakini kuwa atakufa, hufanya haraka kutenda mema

Naam, kila ambaye ana hofu na moto wa jahannam anapaswa kujiweka mbali na mambo ya haramu na awe na subira na asimame imara kupambana na matamanio haramu ya nafsi yake. 

Yeyote asiyeghururishwa na maisha ya dunia, huyaona ni madogo tu masaibu na matatizo anayopambana nayo. Na kila mwenye yakini kuwa kuna siku atakufa, huwa hafanyi uvivu katika kutenda mema, bali huwa mwepesi sana kutenda mambo ya kheri.

Tags