Hikma za Nahjul Balagha (33)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 33 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 33.
Wasikilizaji wapenzi mtakumbuka kuwa katika Hikma ya 31 ya Nahjul Balagha, Imam Ali (AS) ameelezea nguzo za imani. Kwa vile suala la imani na wajibu wa kufahamu vizuri na kiundani hikma hii kuna umuhimu mkubwa, tumeamua kuichambua hikma hiyo katika vipindi sita tofauti.
Kwenye sehemu hii ya 33 ya mfululizo huu ambayo ni sehemu ya tatu ya uchambuzi huo wa hikma ya 31 tutazungumzia nguzo ya uadilifu iliyotajwa na Imam Ali AS katika nguzo za imani kwenye Hikma ya 31 ya Nahjul Balagha.
Katika Hikma ya 31 ya Nahjul Balagha na baada ya Imam Ali AS kubainisha nguzo mbili za subira na yakini, anasema kuwa uadilifu ndiyo nguzo ya tatu ya imani.
Uadilifu maana yake ni kwamba kila kitu kiwekwe mahali pake panapostahiki, kwa namna ambayo kitu hicho kitaweza kupata sehemu yake ifaayo na inayostahiki ya kuwepo kwa ukamilifu wake katika sehemu hiyo bila ya kuingilia haki na nafasi za vitu vingine. Imam Ali AS anatoa ufafanuzi zaidi kuhusu hikma hiyo aliposema:
وَالْعَدْلُ مِنْهَا عَلَى أَرْبَعِ شُعَب: عَلى غَائِصِ الْفَهْمِ، وَغَوْرِ الْعِلْمِ، وَزُهْرَهِ الْحُکْمِ، وَرَسَاخَهِ الْحِلْمِ
Na uadilifu una matawi manne. Ufahamu wa kina, elimu ya kina, maamuzi sahihi na upole na subira katika hukumu.
Kwa hakika, anayetaka kuhukumu kwa haki, jambo la kwanza analopaswa kuwa nalo ni uelewa wa kina wa kile alichoamua kukitolea hukumu. Baada ya hapo, ni kupata maarifa na taarifa za kutosha na za kina kuhusu suala hilo ili aweze kutoa hukumu yake kwa uwazi na bila ya utata wowote na hatimaye aweze kuondoa vizuizi na vikwamishaji vyote vilivyopo kwa kutumia subira na uvumilivu.
Katika barua yake maarufu kwa Malik Ashtar (Barua ya 53 ya Nahjul Balagha), wakati Imam alipomtuma Malik Ashtar kuwa gavana wake nchini Misri, alimbainishia sheria zote zinazohusiana na serikali na haki za watu katika barua hiyo na kumtaka azitekeleze ndani ya mawanda na mapana yote ya serikali yake. Katika sehemu moja ya barua hiyo Imam anaorodhesha baadhi ya vielelezo na sifa maalumu wanazopaswa kuwa nazo mahakimu akisema: “Basi mchague aliye bora zaidi machoni pako miongoni mwa raia zako ili atoe hukumu miongoni mwa watu. Yule asiyewatia kwenye matatizo watu katika mambo yao mbalimbali, na ugomvi wa mahasimu na wanaofanyiana uadui usimpandishe hasira na kumfanya mkaidi, na wala asiwe ni mtu mwenye kushikilia makosa yake na kuteleza kwake, na wakati kosa lake linapombainikia wazi asiwe mgumu kulegeza kamba na kurudi kwenye ukweli. Mtu ambaye kumjia mara kwa mara watu wanaogombana hakumtii chembe ya uchofu na awe na subira na uvumilivu baada ya kubainika haki na katika maamuzi awe na msimamo imara zaidi kuliko wote na asitetereke kabisa.
Tab'an ni wajibu wetu tuseme hapa kwamba, maneno hayo ya Imam Ali AS hayawahusu tu mahakimu na majaji mahakamani, bali yanahusu hukumu zote za kijamii na maisha ya kimaada na kiroho ya wanadamu. Kwa maneno mengine ni kwamba, sisi sote, mahali popote tulipo, ni wajibu kufuata miongozo hiyo mitukufu na lazima tuwe waangalifu na tuonyeshe subira na uvumilivu wakati wa shida na baadhi ya wakati katika mitazamo isiyo ya haki tunayopambana nayo kutoka kwa baadhi ya watu.
Baada ya kubainisha matawi ya uadilifu kwa hikima na balagha kubwa, Imam Ali AS anaeleza athari za kila tawi akisema:
فَمَنْ فَهِمَ عَلِمَ غَوْرَ الْعِلْمِ; وَمَنْ عَلِمَ غَوْرَ الْعِلْمِ صَدَرَ عَنْ شَرَائِعِ الْحُکْمِ; وَمَنْ حَلُمَ لَمْ یُفَرِّطْ فِی أَمْرِهِ وَعَاشَ فِی النَّاسِ حَمِیداً
Mwenye kufikiri sawasawa; atapata ufahamu kwa kina wa elimu na yule anayepiga mbizi kwenye kina cha elimu na maarifa; huibuka juu akiwa ameshiba lulu za hukumu, na mwenye kujipamba kwa subira na uvumilivu hakumbwi na misimamo ya kuchupa mipaka katika mambo yake na ataishi kwa heshima kati ya watu.