Nov 19, 2023 06:36 UTC
  • Palestina, Suala Kuu la Umma wa Kiislamu (2)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran na karibuni kusikiliza sehemu ya pili ya kipindi cha Palestina, Suala Kuu la Umma wa Kiislamu.

Katika kipindi cha leo tunakusudia kujadiliana nanyi kwa pamoja umuhimu wa suala la ardhi ya Palestina kwa ulimwengu wa Kiislamu na ni kwa nini suala hili linapaswa kupewa kipaumbele na kuchukuliwa kuwa dukuduku la pamoja la nchi za Kiislamu. Kama mnavyokumbuka tulizungunmzia katika kipindi kilichopita historia fupi ya ardhi ya Palestina na tukasema kuwa Palestina ni ardhi yenye historia kongwe ambayo inarejea nyuma maelfu ya miaka na kwamba katika kipindi hicho chote imekuwa ikishuhudia mapigano na mivutano kati ya makabila na jamii tofauti kutokana na nafasi yake muhimu ya kijografia, kiuchumi na ardhi yenye rutuba kwa ajili ya shughuli za kilimo. Pia tulisema kwamba hata kama wakazi wa kwanza wa ardhi hiyo walifika huko maelfu ya miaka iliyopita lakini kabila la kwanza kuishi katika ardhi hiyo lilikuwa kabila la Waarabu wa Kanaani ambao walihamia katika ardhi hiyo yapata miaka 3500 kabla ya kuzaliwa Isa Masih (as) au kwa jina jingine Yesu Kristo, wakitokea Bara Arabu ambapo walianzisha ustaarabu mpya na kujenga huko miji mingi. Tulisema pia katika kipindi kilichopita kuwa jina la sasa la Palestina lilitokana na jina la makabila ya kale yaliyoitwa Palest au Pulasti ambayo yaliwasili katika ardhi ya Palestina katika karne ya 13 kabla ya kuzaliwa Isa Masih (as). Walivutiwa na kisha kufuata dini na utamaduni wa Wakanaani na kuimarisha zaidi maendeleo ya ardhi hiyo. Sasa tunakuombeni tuendelee na kipindi hiki kutokea hapo, karibuni.


********************

Ardhi ya Palestina ni chimbuko la Manabii na Mitume tofauti wa Mwenyezi Mungu na kimsingi historia ya Palestina inaanza kwa jina la Manabii. Itikadi ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika ardhi hiyo ilianza kwa kuingia Nabii Ibrahim (as) katika ardhi ya Palestina. Nabii Ibrahim (as) ni miongoni mwa Mitume Ulul Azma au kwa maneno mengine Mitume Wakuu walioteremshiwa sheria na vitabu vya mbinguni, ambaye aliwasili katika ardhi ya Palestina kutokea Iraq, miaka 1900 kabla ya kuzaliwa Isa Masih (as). Kama tulivyotangulia kusema, Nabii Ibrahim ni miongoni mwa Mitume Wakuu ambao walipewa sheria, mafundisho matakatifu, azma na irada thabiti na kufanya juhudi kubwa kwa ajili ya kueneza mafundisho hayo na itikadi ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake. Nabii Ibrahim alikuwa kiongozi wa ibada ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa makabila ambayo ima yalikuwa yakiabudu masanamu au viumbe vingine vya angani kama mwezi na jua. Alipowasili katika ardhi ya Palestina aliishi katika mji wa sasa wa al-Khalil (Hebron).

Ibrahim (as) hakuwa tu kiongozi wa imani ya kumuabudu Mwenyzi Mungu mmoja, bali pia alikuwa mtu wa kwanza kugeuza mila ya kutoa watoto kafara. Kwa amri na mapenzi ya Mwenyezi Mungu, yeye na wafausi wake waliondoka katika mji wa Ur na kuhamia Kanaani. Alipokuwa akiishi Kanaani, alikutana na watu ambao walikuwa wakifuata mila na desturi zilizokuwa kinyume kabisa na imani ya kumwabudu Mwenyezi Mungu mmoja. Dini ya watu hao ilikuwa ni ya kuabudu masanamu ambapo moja ya masanamu hayo maarufu lilikuwa likiitwa "Baal" ambalo maana yake ni "mmiliki na bwana." Kwa itikadi yao huyo alikuwa mungu wa jua na pia sanamu la "Ashtar" au "Astarte" ambalo kwa mtazamo wao alikuwa mungu wa mwezi. Watu wa Kanaani pia walikuwa wakitoa kafara watoto wao kwa mmoja wa miungu yao hiyo aliyeitwa Molokh au Molak (Kilatini: Moloch au Molech) katika ibada isiyo ya kibinadamu. Molokh alionyeshwa kwa umbo la fahali mwenye pembe mbili zilizoinuliwa na wakati mwingine akiwa na mabawa mawili. Aliketishwa kwenye kiti cha enzi cha dhahabu na kunyoosha mikono yake mbele ili kupokea dhabihu ya mtoto aliyetolewa kafara. Sanamu hilo lilitengenezwa kwa chuma na wakati mwingine kwa shaba, ambapo wakati wa ibada ya kutolewa kafara mtoto, moto mkali uliwashwa chini ya jukwaa lililoketishwa sanamu hilo. Wapiga ngoma walipiga ngoma kwa sauti kubwa ili kuzuia sauti ya kilio na machungu ya mtoto aliyekuwa akipitia mateso makali, kuwatia huzuni na huruma watu waliokuwa pembeni yake.

Molokh

Alipowasili Palestina, Nabii Ibrahim (as) alikemea vikali ibada ya masanamu na kuwatahadharisha Wakanaani kutoa kafara watoto wao na kuwataka wamwabudu Mwenyezi Mungu mmoja. Hatimaye Nabii Ibrahim (as) aliaga dunia na kuzikwa katika mji wa al-Khalil. Mji huo umepewa jina hilo kutokana na kaburi la Nabii Ibrahim (as) kuwa katika mji huo mtakatifu.

Kaburi la Nabii Ibrahim (as) katika Msikiti wa Ibrahim katika mji wa al-Khalil

Nabii Ibrahim (as) alijaliwa mtoto wa kiume kwa jina Is'haq (as) kutoka kwa mke wake wa kwanza Bibi Sarah, na kabla ya hapo Ismail kutoka kwa mke wake wa pili Bibi Hajar. Miaka Mingi baada ya hapo Is'haq alijaliwa kupata mtoto kwa jina Ya'qoub (Yakobo) ambaye alipewa lakabu ya Israil (Israeli). Yaqoub alijaliwa kuwa na watoto 12 wa kiume ambao wote waliitwa Bani Israel kwa maana ya wana wa Israel. Mmoja wa watoto hao wa Nabii Ya'qoub ni Nabii Yusuf ambaye alipendwa sana na baba yake, Ya'qoub. Umakini na uzingatiaji mkubwa aliopewa Yusuf na baba yake pamoja na kutambua ndugu zake kwamba siku moja angechukua mamlaka ya kuwaongoza Waisraeli kwa amri ya Mwenyezi Mungu, ni mambo yaliyomfanya Yusuf kuonewa wivu na kuchukiwa na ndugu zake wengine. Walipanga njama ya kufunga na kumtupa kwenye kisima na kisha kumuuza kwa msafara wa Bani Ismail (wajukuu wa Nabii Ismail) ili kama walivyodhania, waweze kubadilisha mapenzi na irada ya Mungu, huku wakiwa wameghafilika na ukweli kwamba irada ya Mwenyezi Mungu haibadiliki kamwe.

Yusuf akapelekwa na msafara huo hadi Misri. Alipokuwa huko alivutiwa na mmoja wa watawala wa Misri na kupewa cheo muhimu huko. Wakati huo ambapo pia alikuwa ameteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Mtume, aliwalingania watu wa Misri na kuwataka wamwabudu Mwenyezi Mungu mmoja na kujitenga na ibada ya masanamu. Licha ya kukabiliwa na upinzani mkali na hasira ya makuhani wa mahekalu ya masanamu, lakini alifanikiwa kuwashinda wote. Baada ya ndugu zake Yusuf (as) kusafiri Misri kwa ajili ya kununua ngano, alijiarifisha kwao nao wakawa wametubia makosa waliyofanya. Pamoja na hayo kafara ya dhambi zao ilikuwa kwamba Yusuf aliwataka warejee Kanaani na kuwaleta Misri familia yao wote. Kwa njia hiyo, kwa hakika Bani Israel walihamishiwa Misri ili wapate kusamehewa dhambi yao ya makusidi waliyotenda baada ya kukaidi amri ya Mwenyezi Mungu. Kutokana na irada na mapenzi ya Mwenyezi Mungu na baada ya kuaga dunia Nabii Yusuf (as), Bani Israel waliishi nchini Misri kwa miaka 400 huku wakipitia matatizo na mashaka makubwa hadi ilipotimia ahadi ya Mitume wao wa zamani ya kuteuliwa miongoni mwao Mtume Musa bin Imran (as).

Musa bin Imran ambaye ni mmoja wa wajukuu wa Ya'qoub ni mmoja wa Mitume Ulul Azm (as). Jina la Nabii Musa (as) na muhtasari wa maisha yake umezungumziwa katika kitabu kitakatifu cha Qur'ani kuliko Mtume mwingine yeyote ambapo limetajwa katika Sura tofauti za kitabu hicho mara 136. Alizaliwa katika kipindi ambacho Firauni alikuwa akitawala Misri ambapo aliamuru watoto wote wa kiume wa Bani Israel wauawe na kukamatwa mateka mabinti zao. Baadhi ya watu wanasema kuwa Firauni alitoa amri hiyo kwa ajili ya kuwadhoofisha Bani Israel na wengine kusema kuwa alitoa amri hiyo kutokana na ndoto aliyoota. Wanasema aliota ndoto ambapo aliona kwamba mtoto mmoja wa kiume angezaliwa katika kabila la Bani Israel na kisha kuutokomeza ufalme wake. Kwa hiyo, wakati Musa (as) alipozaliwa, Yokhabid, mama yake Musa (as), kwa mujibu wa wahyi wa Mwenyezi Mungu, alimweka mwanawe kwenye kijisanduku na kisha kukiweka kwenye Mto Nile. Mtoto huyo alitolewa majini na mmoja wa watu wa karibu wa Firauni. Ndio maana akaitwa Musa kwa sababu kijitanda chake kilipatikana karibu na mti ndani ya maji. Na bila shaka Mwenyezi Mungu alitaka Musa (as) akue na kulelewa katika kasri na ukoo wa kifalme wa Firauni.

Musa (as) atupwa kwenye maji

Baada ya kuteuliwa Musa (as) kuwa Mtume na kutokana na ukandamizaji na mateso makali ambayo Firauni (Ramses II) aliwafanyia Bani Israel, alipewa jukumu la kuwakomboa watu wa Israel kutoka katika ukandamizaji wa Firauni nchini Misri na kuwapeleka Kanaani (Palestina ya leo). Kwa hivyo katika miaka karibu 3300 iliyopita, Nabii Musa (as) na Bani Israel walipitia jangwa na kusafiri hadi karibu na ardhi ya baba na mababu zao (Nabii Ya'qoub). Wakati huo, Musa alimchagua mjumbe wake (wasii), Yusha' (Joshua) na watu kadhaa na kuwatuma Palestina ili wapate kudadisi na kujua hali halisi ya mambo ilivyokuwa huko. Baada ya kurejea walitoa ripoti kwamba kulikuwa na watu wenye nguvu kubwa na madhalimu huko, jambo lililowafanya Bani Israel kuogopa na kutotii amri ya Mtume wao Musa (as) ya kwenda Palestina. Kwa hivyo Bani Israel walibakia wakitangatanga katika jangwa hilo kwa muda wa miaka 40 wasijue la kufanya. Katika kipindi hicho kirefu Nabii Musa (as) alifanya juhudi kubwa za kuwaongoza watu wake kwenye njia nyoofu na kuwataka watii amri ya Mwenyzi Mungu, lakini Bani Israel walimuasi na kukataa kumtii. Kundi moja lilianza kuabudu masanamu na jingine likakaidi amri zake na kutaka kurejeswa Misri.

Zulia lililofumwa kwa mikono linaloonyesha matukio ya Bani Israel katika jangwa la Sinai nchini Misri

Mwishowe Nabii Musa (as) aliaga dunia katika kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 120 au 126.

 

Tags