Nov 20, 2023 18:17 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (35)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 35 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 35.

Katika Hikma ya 31 ya Nahjul Balagha, Imam Ali (AS) ameelezea nguzo za imani. Kwa kuzingatia umuhimu wa suala la imani na wajibu wa kuwa na ufahamu mzuri kuhusu hikma hii, tumeamua kuizungumzia na kuichambua katika vipindi sita mfululizo hii ikiwa ni sehemu ya tano ya kuichambua hikma ya 31 ya Nahjul Balagha. Leo tutazungumzia nguzo ya kufru kama ilivyotajwa na Imam Ali AS kwenye hikma hiyo.

Katika muendelezo wa hikma ya 31, Imam Ali AS anawahesabu watu makafiri kuwa ni kundi ambalo ukweli umefichwa kwao na anataja mambo manne kuwa ndiyo yaliyoficha ukweli na kuweka pazia mbele ya watu hao makafiri.

Anasema: 

 وَ الْکُفْرُ عَلَى أَرْبَعِ: دَعَائِمَ عَلَى التَّعَمُّقِ، وَالتَّنَازُعِ، وَالزَّیْغِ، وَالشِّقَاقِ

“Na ukafiri unatokana na mambo manne: Kuzama na kudadisi sana kusiko sahihi, kupiga vita haki, kufuata upotofu kwa hawa na matamanio ya nafsi na ukaidi, ubishi na taasubu.

Katika hekima hii, mbali na suala la imani, Imam Ali AS anazungumzia pia mambo yanayopelekea kwenye upotofu na kutoifikia haki na kila kitu ambacho kinasimama mbele ya fikra ya mwanadamu na kumuwekea pazia la kutojua uhakika na uhalisia wa mambo. Baadaye anatoa ufafanuzi zaidi akisema:

فَمَنْ تَعَمَّقَ لَمْ یُنِبْ إِلَى الْحَقِّ

 

Yeyote mwenye kuzama na kudadisi dadisi kusiko sahihi, hawezi kuufikia ukweli na haki.

Maana ya kuzama katika kutafakari hapa ni vile mtu kuchupa mipaka katika kudadisidisi hasa mambo ambayo ni vigumu kuyafikia. Kwa mfano sehemu moja ya aya ya 101 ya Suratul Maidah, Qur'ani Tukufu inasema: "Enyi mlioamini! Msiulizeulize mambo ambayo mkidhihirishiwa yatakuchukizeni." Kama tunavyojua, katika kisa cha ng'ombe cha Wana wa Israili yaani Bani Israil kinachosimuliwa na Qur'ani Tukufu mwanzoni mwanzoni mwa sura ya pili ya al Baqarah, Bani Israil iliwawia vigumu sana na walilazimika kugharamia sana ng'ombe kutokana na udadisi na kuuliza kwako kusiko sahihi. Wana wa Israili walijitia wenyewe kwenye matatizo wakati awali waliambiwa tu wachinje ng'ombe yoyote tu, lakini wakafanya udadisi usio na haki mwisho wakala hasara kubwa. 

Amma kuhusu suala la kutangaza na kujiingiza kwenye vita dhidi ya haki, ambalo ni moja ya vipengele vingine vinavyopelekea kwenye ukafiri, Imam Ali AS anasema,

وَمَنْ کَثُرَ نِزَاعُهُ بِالْجَهْلِ دَامَ عَمَاهُ عَنِ الْحَقِّ

Mtu ambaye inakuwa mingi mizozo yake kutokana na ujinga wake, daima huwa kipofu asiyeiona haki.

Maana ya mizozo hapa ni ile ile inayotokea kila siku na mara kwa mara katika masuala tofauti ambapo kadiri inavyoendelea nakuwa mingi, ndivyo mtu anavyozidi kupofuka na kutoona ukweli, bali huwa anashikilia misimamo yake kitaasubu na kutopenda kabisa kuikubali haki. Kila mtu anapoanza kuzozana hukwambia sina lengo la kukataa haki, lakini kadiri mzozo unavyokuwa mkubwa ndivyo anavyozidi kuwa mbali na haki na kushikamana na msimamo wake hata kama ni wa batili.  

Katika sehemu inayofuata, Imam Ali AS ametumia neno "Zigh" na kusema ni moja ya vitu vinavyomzuia mtu kuiona haki na kumtumbukiza kwenye shaka na wasiwasi. Imam anasema:

وَ مَنْ زَاغَ سَاءَتْ عِنْدَهُ الْحَسَنَهُ، وَحَسُنَتْ عِنْدَهُ السَّیِّئَهُ، وَسَکِرَ سُکْرَ الضَّلاَلَهِ

Mtu ambaye anakengeuka njia ya haki (na kufuata hawa na matamanio ya nafsi), kwa mtazamo wake jambo hilo ni baya na baya huliona ni jema na huleweshwa na kileweshaji cha upotofu

Tunajua kwamba mtu anapokengeuka njia ya haki na kuzama katika matamanio na hawa za nafsi, polepole huzoea mambo mabaya, na kwa sababu ya matamanio ya nafsi yake hufikiri kuwa jambo baya ni mzuri, na kutokana na kujiweka mbali na mambo mazuri, huyaona mambo hayo mazuri kuwa ni mabaya na ya kuchukiza.

Kisha Imam AS anazungumzia matokeo mabaya ya “shiqaq” ambao ni uadui wa mtu mtu mbishi dhidi ya haki. Anjasema:

وَمَنْ شَاقَّ وَعُرَتْ عَلَیْهِ طُرُقُهُ، وَأَعْضَلَ عَلَیْهِ أَمْرُهُ، وَضَاقَ عَلَیْهِ مَخْرَجُهُ

Mtu ambaye anapinga haki kiubishi na kiuadui, huwa nzito kwake njia ya kuifikia haki, na mambo yatakuwa magumu na tata kwake na ataingia kwenye mkamo ambao ni vigumu kwake kutoka.

Tunajua kwamba moja ya mambo yanayomzuia mtu kuijua haki na ukweli ni ukaidi, ni ubishi, ni taasubu na ni uadui wake anaoifanyia haki. Ubishi haumruhusu mtu kuachana na maamuzi yake ghalati na taasubu zisizo na maana.

Wasaalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags