Jul 10, 2016 06:36 UTC

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Katika Makala iliyopita tulisema dunia ni utangulizi wa Akhera na wenzo wa kupata saada na ufanisi wa milele. Dunia ni sehemu ya kazi na amali na Akhera ni mahala pa kuchuma na matokeo ya kazi na amali. Vilevile tulisisitizia kuwa, kutadabari na kufikiria daima suala hilo la ufufuo huwa na taathira kubwa katika maisha ya kidunia ya mwanadamu. Hata hivyo hapana budi kuzingatia njia ya kati na kati na kutochupa mpaka katika suala hili.

Mwanadamu mwenye imani ya Maadi na Siku ya Mwisho anaelewa kwamba, hatimaye itakuja siku ambapo atapewa malipo na jazaa ya amali na matendo yake. Katika siku hiyo wanadamu wataanza safari ya uhai wa milele ama katika saada na raha ya kudumu au katika adhabu na mashaka ya kudumu. Amali, mienendo na matendo yote ya waja yanaandikwa na kusajiliwa hapa dunia na mwanadamu ataona sura na picha ya amali na matendo hayo huko Akhera. Amali na matendo mema yataonekana katika sura nzuri na ya kuvutia, na matendo na mienendo miovu itakuwa katika sura mbaya na ya kutisha inayoambatana na adabu. Kutambua jambo hilo daima humfanya mtu anayeamini Maadi na Siku ya Malipo awe mwangalifu sana kuhusu matendo, mienendo, maneno na hata fikra zake. Mwanadamu kama huyu hutambua kuwa, hayo yote yatakuwa mtaji na masurufu yake katika ulimwengu mwingine.

Swahaba Qais bin A'sim anasimulia kwamba: Siku moja tulikwenda kwa Mtume (saw) katika kundi la Bani Tamim. Nilimwambia Mtume kwamba: Yaa Rasulallah! Tunaishi mbali jangwani na tunakutana na wewe mara chache sana. Tupe mawaidha ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mtume alitupa mawaidha na alisema: Ewe Qais! Utakuwa na mwenza atakayezikwa na wewe kaburini akiwa hai na utazikwa pamoja na yeye ukiwa maiti. Kama atakuwa mwema utaanisika na kubuudika kwake, na kama atakuwa mbaya utaadhibika kutokana na yeye. Kisha alisema: Ewe Qais! Hatafufuliwa pamoja na wewe isipokuwa mwenzi wako huyo na hutafufuliwa wewe isipokuwa ukiwa pamoja naye, na hutaulizwa isipokuwa kuhusu mwenzako huyo; hivyo basi mfanye mwema, kwa sababu akiwa mwema utaanisika na kupata saada, na kama atakuwa mbaya utaadhibika. Qais na wenzake waliuliza: Ni nani huyo tutakayezikwa na kufufuliwa naye ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Alisema: Ni amali na matendo yenu.

Uhusiano na mfungamano wa kiroho wa mwanadamu na Mola Muumba na kudumu katika kutekeleza amri na kujiepusha na makatazo yake huwa bima inayomkinga mwanadamu kutumbukia katika mitego ya shetani. Muumini wa kweli wa maadi na ufufuo anajua kwamba, rehma za Mwenyezi Mungu ni pana na kubwa lakini suala hilo halina maana ya kukana adhabu na malipo ya mja kwa makosa na madhambi yake. Rehma na huruma ya Mwenyezi Mungu haina maana ya kufumbia macho dhulma, ufuska na uonevu unaofanywa na wanadamu dhidi ya wenzao kiasi cha kuwaona dhalimu na anayedhulumiwa kuwa wako sawa mbele ya Mwenyezi Mungu. Uadilifu wa Mola Muumba unahukumu kwamba, kila mtu atachuma alichopanda na kupata jazaa na malipo ya matendo na minendo yake. Hii ndiyo kanuni kuu ya Mwenyezi Mungu inayotawala mambo yote. Aya za 53 na 54 za Suratu Yunus zinasema: Na wanakuuliza: Je! (Adhabu ya Siku ya Mwisho) Ni kweli? Sema: Ehe! Naapa kwa jina la Mola wangu Mlezi! Hakika hayo ni kweli, na wala nyinyi hamshindi. Na lau kama kila nafsi iliyodhulumu inamiliki kila kiliomo duniani, bila ya shaka ingelitoa vyote kujikombolea. Na watakapoiona adhabu wataficha majuto. Na patahukumiwa baina yao kwa uadilifu, nao hawatadhulumiwa.            

Uadilifu na hekima ya Mwenyezi Mungu haitakuwa na maana ila pale madhalimu na watenda maovu watakapopewa jazaa na malipo ya amali na matendo yao. La sivyo inawezekana vipi kuona Mwenyezi Mungu SW akiwapokea na kuwakirimu peponi madhalimu, wauaji na makatili waliochafua sura ya historia ya mwanadamu kwa jinai na uhalifu wao mkubwa? Kwa hakika tunaweza kusema kuwa, adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa madhalimu na wauaji hao ndiyo uadilifu halisi. Kwa sababu haiwezekani kumuita Mwenyezi Mungu kuwa ni muadilifu na mwema isipokuwa akiwaadhibu na kuwapa jazaa na malipo yao watu waovu na makatili. Huu ndio uadilifu wa Mola Muumba ambaye hapuuzi au kufumbia macho jema au ovu hata likiwa dogo kama punje na haradali. Imam Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as) anasema: Wallahi kulazwa usiku kucha kwenye miba au kufungwa na kuburutwa kwa minyororo ni bora kwangu mimi kuliko kukutana na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Siku ya Kiyama nikiwa nimedhulumu baadhi ya waja wa Mwenyezi Mungu au nimeghusubu na kunyakua mali.." (Nahjul Balagha, hotuba:223)      <<<<    >>>

Miongoni mwa mambo yanayosisizwa sana na mawalii wa Mwenyezi Mungu ni kuwa na hofu na kumuogopa Mwenyezi Mungu au kwa maneno sahihi zaidi, kuogopa matendo yetu sisi wenyewe. Hofu na woga huo hudhibiti amali na matendo yote ya mwanadamu. Hofu na woga wa hatima na mwisho mbaya wa madhambi na dhulma humfanya mwanadamu azidishe uangalifu wake na kudhibiti ghariza na matamanio yake. Humfanya aishi baina ya hofu ya Siku ya Mwisho na matarajio ya rehma zisizo na kikomo za Mwenyezi Mungu.

Msingi wa wito wa Mitume na viongozi wa dini ulisimama juu ya hofu na matarajio. Katika upande mmoja watukufu hao waliwabashiria wafausi wao neema na saada ya milele katika ulimwengu wa Akhera, na katika upande mwingine waliwatahadharisha na dhambi na kuasi amri za Mwenyezi Mungu na hatimaye kupatwa na adhabu ya milele. Qur'ani Tukufu inasema katika aya 28 ya Suratu Sabai kwamba: Na hatukukutuma ila kwa watu wote, uwe mtoa bishara njema, na mwonyaji. Lakini watu wengi hawajui

Hivyo mwanadamu anapaswa kuishi baina ya hofu ya adhabu ya Mwenyezi Mungu na matarajio ya rehma na huruma yake. Imepokewa kutoka kwa Imam Jafar Swadiq (as) kwamba amesema: Muumini anapaswa kumuogopa Mwenyezi Mungu kana kwamba amesimama kandokando ya moto wa Jahannam, na awe na matarajio na rehma zake kana kwamba ni mtu wa peponi." (Tafsiri ya al Amthal, juzuu 20)

Sahaba mwema wa Mtume Muhammad (saw), Abu Dharr al Ghifari baada ya kuaga dunia mwanaye alikuwa na wasiwasi na woga mkubwa kuhusu hatima yake, je ni miongoni mwa watu waliopata ufanisi wa milele au watu waliotumbukia katika adhabu na mashaka ya kudumu? Alizongwa sana na suala hilo.  Alikwenda kwenye kaburi la mwanaye na kuweka mkono wake juu ya kaburi na kusema: Mwanangu mpenzi! Mwenyezi Mungu SW akupe rehma zake zisizo na kikomo..  Ghamu na majonzi kuhusu hatima yako yameniondolea makiwa na huzuni ya kifo chako. Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba, silii kutokana na huzuni ya kifo chako bali kutokana na hofu ya awamu mbalimbali zilizoko mbele yako. Laiti kama ningejua baada ya kufikwa na mauti umesema nini na umeambiwa nini".

Baadaye kidogo alielekeza moyo wake kwa Allah na kusema: Mola wangu Mlezi! Nimemsamehe mwanangu wajibu wote uliomfaradhishia kwa baba yake. Mola wangu! Msamehe uliyomuwajibishia wewe kwa sababu Wewe ni Mwingi wa kusamehe na Mkarimu zaidi kuliko mimi.

Wassalam alaykum warahmatullahi warakatuh.     

      

  

Tags