Apr 29, 2024 04:26 UTC
  • Tuujue Uislamu (13)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu. Katika kipindi chetu cha juma hili tutafungua ukurasa mwingine

 

Aina tofauti za wanyama huishi duniani, ambapo kila mmoja kati ya wanyama hawa ana jukumu maalumu na ushawishi katika ulimwengu wa asili. Kujua siri za ajabu za maisha ya wanyama hutuongoza kwenye nguvu na mpango wa Mwenyezoungu katika uumbaji.

Ulimwengu wa ajabu na maajabu wa wanyama ni mkubwa sana kiasi kwamba, umekuwa mada na mjadala wa maelfu ya vitabu na makala za kisayansi. Hata hivyo, wanasayansi wanakubali kwamba, bado kuna mambo mengi ya hakika kuhusu uhai wa wanyama ambayo bado hayajulikani.

Utafiti mdogo katika maisha ya wanyama unaonyesha ukweli kwamba, kila mmoja wao anaishi na kukua kulingana na mpango na ratiba maalumu. Samaki wakubwa na nyangumi wanaishi kwenye bahari, huanguliwa ndege wazuri wenye manyoya na mabawa ya rangi kwa rangi, na kila aina ya mamalia na hata wanyama wadogo sana, wote hukua na kukamilika kulingana na sheria fulani. Ni vyema kutambua kwamba, Muumba mwenye hekima na busara ametoa uwezo kwa kila aina ya viumbe hai ili waweze kudumisha kuwepo kwao katika hatua mbalimbali za ukuaji na kujiandalia nyenzo za maisha na kubakia kwao.

Kwa msaada wa nguvu ya ghariza, wanyama wanajua jinsi ya kuishi, jinsi ya kuandaa makazi na kujijengea viota, na namna ya kulea watoto wao. Wanawajua maadui zao na wanafahamu vyema mbinu za mashambulizi, kutoroka na kujilinda. Mwenyezi Mungu ameweka akiba na baraka nyingi sana katika ardhi ambayo inakidhi mahitaji ya wanyama, ili viumbe dhaifu kama ilivyo kwa walio na nguvu zaidi na wao wafaidike na meza pana ya asili ili kuendelea kuishi.

Utaratibu wa ulinzi wa wanyama dhidi ya vitisho pia ni suala la kufikiria. Mbinu mbalimbali za ulinzi zinazingatiwa katika ulimwengu wa wanyama. Baadhi yao hubadilika rangi na wengine hubadilisha sura wanapokabiliwa na hatari. Wengine hujilinda kwa kuonyesha nguvu na kuujitutumua na kuchukua hatua za kushangaza dhidi ya mpinzani.

 

Kundi jingine la wanyama, lina ujuzi na umahiri wa kuvutia katika kujificha. Wale wanyama walio na mwendo wa kasi hukimbia haraka na hivyo kutoroka kutoka kwenye makucha ya washambuliaji.

Mwenyezi Mungu anasema katika Qur'an katika Aya ya nne ya Surat al-Jathiyah kwamba:

Na katika umbo lenu na katika wanyama alio watawanya zimo Ishara kwa watu wenye yakini.

Moja ya ishara za Mwenyezi Mungu ni kwamba usawa umezingatiwa katika uumbaji wa wanyama. Kwa mfano, tunajua kwamba tai ni ndege walao nyama na wakati huo huo wana maisha marefu. Ikiwa kuzaliana kwa wanyama hawa kungekuwa kwa wingi kama vile shomoro na kunguru, hapana shaka kuwa, utulivu na maisha ya viumbe vingine hai yangekuwa hatarini. Lakini kwa mpango wa Mungu, uumbaji wao unadhibitiwa na kiwango chao cha uzazi ni cha chini. La kama idadi ya wanyama wakali na wawindaji kama mbwa-mwitu na simba wangekuwa wengi kama ng'ombe na kondoo, basi wangeangamiza haraka mno vizazi vya wanyama wote duniani.

Tunaashiria mfano mwingine. Mdudu kama nzi hutaga mamia ya maelfu ya mayai, lakini maisha yake hayazidi wiki mbili. Sasa, kama maisha ya nzi yangekuwa kwa miaka kadhaa, kila mahali pangeenea nzi na maisha yangekuwa magumu kwa wanadamu na viumbe wengine.

Mfano mwingine wa maajabu haya unaweza kuonekana katika maisha ya nyuki. Mdudu huyu mdogo, lakini mwenye bidii na mwenye manufaa anaonyesha hekima na nguvu za Mungu katika uumbaji. Ikiwa tutatafakarii juu ya maisha ya nyuki, tutaona ulimwengu wa ajabu. Ushirika mkubwa, maisha ya nidhamu na utaratibu, akili ya ajabu na hatimaye shughuli zisizo choka za nyuki wa asali ambao hufuata sheria za asili na kamwe hawavuki mipaka ya sheria.

 

Wataalamu wa Entomolojia (elimu wadudu) wanashangaa sheria makini zinazohusiana na maisha ya nyuki kwamba, chimbuko lake ni nini na zinatekelezwa kwa maagizo gani.

Aya za 68 na 69 za Surat al-Nahl zinasema:

Na Mola wako Mlezi amemfunulia nyuki: Jitengenezee majumba yako katika milima, na katika miti, na katika wanayojenga watu. Kisha kula katika kila matunda, na upite katika njia za Mola wako Mlezi zilizofanywa nyepesi kuzipita. Na kutoka matumbo yao kinatoka kinywaji chenye rangi mbali mbali; ndani yake kina matibabu kwa wanaadamu. Hakika katika haya ipo Ishara kwa watu wanao fikiri.

Wapenzi wasikilizaji, kama inavyoeleweka kutokana na Aya hiyo, Qur'an inavichukulia vitendo vya ajabu vya nyuki kuwa ni matokeo ya wahyi wa Mwenyezi Mungu na inazingatia kuwa hii ni moja ya ishara na dalili za Mwenyezi Mungu kwa wale wanaofikiri. Ikiwa tutazingatia mfumo wa maisha ya nyuki, tutaelewa zaidi umuhimu wa maneno ya Qur'ani katika suala hili. Kulingana na Aya hii, dhamira ya kwanza ya nyuki ni kujenga nyumba.

Nyuki wana utendaji wa ajabu ambao una hali ya ugawanaji majukumu.  Koloni la Nyuki linandwa na washirika wa aina tatu yaani Malkia, Wafanyakazi na Nyuki dume. Nyuki Malkia ana umbo kubwa kuliko Nyuki wengine wote huku mabawa yake yakiwa mafupi. Ukubwa huu unatokana na huduma za pekee anazozipata kutoka kwa wafanyakazi. Kazi yake pekee ya malkia ni kutaga mayai ambayo hupitia hatua zote za ukuaji hadi kufikia Nyuki wakubwa na kuingia kwenye majukumu ya kila siku.

Majukumu ya Nyuki wafanyakazi ni kujenga, kulinda, kufanya usafi, kuhakikisha mzunguko wa hewa ndani ya Mzinga kwa kupigapiga mabawa yao na kutafuta chakula cha kutosha kwa ajili ya Malkia na watoto. Tafiti zinaeleza kuwa kwa safari moja ya kwenda kutafuta chakula, Nyuki hutembelea takribani maua 100. Ndani ya mzinga hubaki nyuki wengine ambao kazi yao ni kupokea malighafi hizo na kuzichakata ili kukamilisha asali. Nyuki wafanyakazi ni wadudu wakorofi na wakali; hukabiliana na yeyote anayehatarisha usalama wa malkia wao bila kujali kama wanahatarisha maisha yao.

Kwa upande mwingine nyuki dume hawana kazi yao isipokuwa kuzaliana tu. Inaelezwa kuwa, wakati mwingine dume hutegemea wafanyakazi wampe chakula. Je mpangilio wote huu na maarifa haya makubwa ya nyuki ni jambo ambalo limetokea hivi hivi tu na hakuna Muumba na muendeshaji na msimamizi wa haya yote? Bila shaka, hizi zote ni ishara za wazi za muumba mbunifu na mwenye busara, na hakuna mtu isipokuwa yeye anayeweza kupanga na kudhibiti ulimwengu huu mkubwa.

 

Muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati. Asanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.