May 26, 2024 04:38 UTC
  • Jumapili, 26 Mei, 2024

Leo ni Jumapili tarehe 17 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1445 Hijria sawa na tarehe 26 Mei 2024 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1266 iliyopita Imam Mussa al Kadhim (as) ambaye ni miongoni mwa Ahlubait wa Mtume wetu Muhammad (saw) alibaidishwa na kupelekwa uhamishoni nchini Iraq kutoka Madina kwa amri ya mtawala dhalimu, Haroun Rashid. Mtukufu huyo aliwasili Iraq tarehe 7 Dhilhija 179 Hijria na kufungwa katika jela mji huo. Kwa muda, Imam aliwekwa katika jela ya Issa bin Ja'far aliyekuwa mtawala wa Basra, lakini mtawala huyo alimwandikia barua Haroun Rashid akimuomba amkabidhi Imam kwa mtu mwingine, kwa sababu hakupata ushahidi wowote dhidi ya mtukufu huyo. Haroun Rashid alimpeleka tena uhamishoni Imam mjini Baghdad na akamtaka waziri wake, Fadhl bin Rabi' amuue mjukuu huyo wa Mtume. Waziri huyo alikataa na hivyo Haroun alimtaka mtu aliyejulikana kwa jina la Yahya bin Khalid Barmaki atekeleze amri hiyo. Hatimaye Imam Kadhim (as) aliuuliwa shahidi na muovu huyo kwa amri ya mtawala Haroun Rashid. ***

Siku kama ya leo, miaka 225 iliyopita, alizaliwa Alexander Pushkin, malenga na mwandishi mkubwa wa Urusi mjini Moscow. Pushkin, alipata umaarufu mkubwa mwaka 1820, baada ya kusambaza majmui ya kitabu kilichosheheni mashairi. Muda mfupi baadaye malenga huyo akatunga shairi lililohusu uhuru, suala lililopelekea kubaidishwa kwake. Katika shairi hilo Alexander Pushkin alielezea kwa kina umuhimu wa uhuru. ***

Siku kama ya leo miaka 144 iliyopita Charles Louis Alphonse Laveran, daktari wa Kifaransa aligundua chanzo cha ugonjwa wa malaria duniani. Baada ya kupata shahada yake ya uzamifu, Daktari Alphonse Laveran alisafiri Algeria kwa lengo la kuhudumia watu wa nchi hiyo kuhusiana na masuala ya afya na tiba. Akiwa huko alipata fursa ya kuchunguza na kufanya utafiti wa kina kuhusiana na malaria, ugonjwa ambao ulikuwa ukiangamiza watu wengi katika pembe tofauti za dunia, ambapo mwaka 1880 alifanikiwa kupata chanzo cha ugonjwa huo. Aligundua kuwa ugonjwa huo ulisababishwa na mbu waanaoitwa Anopheles ambao huishi katika sehemu za unyevunyevu na zilizo na maji yaliyotuama. Mwaka 1907 Alphonse Laveran alitunukiwa tuzo ya Nobel kutokana na juhudi kubwa alizofanya katika uwanja wa tiba na ugunduzi wake wa chanzo cha ugonjwa wa malaria.***

Siku kama ya leo miaka 143 iliyopita sawa na tarehe 26 Mei 1881 Ufaransa iliikoloni rasmi nchi ya Kiafrika ya Tunisia. Kabla ya hapo Wafaransa waliingia nchini humo kama wafanyabiashara. Kwa miaka mingi nchi hiyo ilikuwa chini ya himaya ya Ufaransa, lakini katika muongo wa 1930 wananchi wa Tunisia wakaanzisha harakati za ukombozi chini ya uongozi wa Habib Bourguiba, ambapo mwaka 1975 waliung'oa madarakani utawala wa kifalme na kumtawaza Bourguiba kuwa rais wa nchi hiyo. Baada ya kuingia madarakani, Bourguiba alianza kuitawala nchi hiyo kidikteta hadi mwaka 1987 ambapo alipinduliwa na Zein al-Abedeen bin Ali, afisa mkuu wa polisi wakati huo. Zein al-Abedeen pia aliitawala nchi hiyo kwa mkono wa chuma na ukanadamizaji hadi Januari 2011 ambapo alipopinduliwa na wimbi la mwamko wa Kiislamu katika nchi za Kiarabu na kulazimika kukimbilia Saudi Arabia. ***

Katika siku kama ya leo miaka 126 iliyopita, Naser al-Din Shah Qajar, mfalme wanne wa ukoo wa Qajar nchini Iran aliuawa na hivyo kuhitimisha kipindi cha giza cha miaka 50 cha historia ya Iran. Tukio hilo liliandaa uwanja wa kutokea Mapinduzi ya kupigania katiba. Naser al-Din Shah Qajar aliauawa kwa kupigwa risasi katikak Haram ya Abdil-Adhiim kusini mwa Tehran na Mirza Reza Kermani mpigania ukombozi. Reza Kerman alikuwa mmoja wa wafuasi wa Sayyid Jamal al-Din Asadabadi. Kipindi kirefu cha utawala wa Naser al-Din Shah Qajar kinahesabiwa kuwa kipindi muhimu cha historia ya Iran katika zama za utawala wa ukoo wa Qajar. ***