Feb 05, 2025 05:44 UTC
  • Jumatano, tarehe 05 Februari, 2025

Leo ni Jumatano tarehe 06 Shaabani 1446 Hijria, sawa na Februari 5 mwaka 2025.

Katika siku kama ya leo miaka 144 iliyopita alifariki dunia mwanahistoria, mwanafalsafa na mtaalamu mashuhuri wa masuala ya mashariki wa Scotland, Thomas Carlyle.

Mwanafalsafa huyo alizaliwa mwaka 1795 katika familia ya watu wa kijijini  na mbali na lugha ya Kijerumani, alijifunza pia lugha ya Kiarabu na baadaye alianza kufunza lugha hiyo katika Chuo Kikuu cha Cambridge,London. Katika safari zake nyingi katika nchi za Kiislamu, mwanahistoria huyo alijifunza utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu na kuathirika mno na dini hiyo.

Thomas Carlyle anasema kuhusu Qur'ani kwamba: "Qur'ani ni sauti isiyokuwa na wasita kutoka kwenye roho ya ulimwengu, na wanadamu wanapaswa kuisikiliza, la sivyo hawapaswi kusikiliza maneno mengineyo."

Mwanafalsafa huyo wa Scotland anasema kuhusu Mtume Muhammad (SAW) kwamba: Mwenyezi Mungu amemfunza hikima na elimu shakhsia huyu adhimu. Alijiepusha na kupenda jaha na ni miongoni mwa watu waliotakaswa na kupendwa mno na Mola Muweza.   

Thomas Carlyle

Miaka 121 iliyopita katika siku kama ya tarehe 6 Shaaban 1325 aliuawa shahidi Allama Ibrahim Khui alimu na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu.

Alifanikiwa kupata daraja ya Ijihadi baada ya kusoma kwa miaka mingi kwa walimu mahiri wa zama hizo kama Sheikh Murtadha Ansari. Allama Ibrahim Khui alikuwa na umahiri wa aina yake katika elimu za Kiislamu hususan falsafa.

mwanazuoni huyo wa Kiirani alifanya harakati na juhudi kubwa katika zama za kupigania utawala wa katiba, kupinga dhulma na kupigania uhuru. Hatimaye katika siku kama ya leo aliuawa shahidi akiwa nyumbani kwake na makachero wa Muhammad Ali Shah, mmoja wa watawala madikteta wa ukoo wa Qajar. 

Allama Ibrahim Khui

Siku kama hii ya leo miaka 46 iliyopita mamilioni ya wananchi Waislamu na wanamapinduzi wa Iran waliandamana katika miji mbalimbali hapa nchini baada ya kutangazwa serikali ya muda ya Mapinduzi.

Wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano ili kuunga mkono uamuzi huo uliotolewa na Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu.

Katika siku hiyo pia wananchi wa Iran na kwa sauti moja walitaka kuondoka madarakani serikali ya Bakhtiyar ambayo ilikuwa kibaraka wa madola ya kibeberu.

Siku hiyo pia Jenerali Robert Ernest Huyser, mjumbe maalumu wa Marekani aliyekuwa Tehran kwa ajili ya kusaidia juhudi za kuubakisha madarakani utawala wa Shah Pahlavi na kutangaza uungaji mkono wa Washington kwa makamanda wa jeshi la Shah, alifunga virago na kurejea Marekani baada ya kushindwa kusitisha wimbi la Mapinduzi ya Kiislamu.

Jenerali Robert Ernest Huyser

Katika siku kama ya leo miaka miwili iliyopita Pervez Musharraf, Rais wa kumi wa Pakistan, alifariki dunia.

Musharraf alizaliwa mnamo Agosti 11, 1943, huko Naharwali Haveli, katika wilaya ya Daryaganj karibu na Delhi, katika India iliyokuwa ikitawaliwa na Uingereza. Baada ya kugawanywa India, alihamia Pakistan na wazazi wake na kuishi Karachi. Aliingia Chuo cha Kijeshi cha Pakistani huko Kakul mnamo 1961 na baada ya kuhitimu, alijiunga na jeshi na akapanda safu za juu za uuongozi.

Mwaka 1998, Pervez Musharraf aliteuliwa kuwa Amiri Jeshi Mkuu na Waziri Mkuu Nawaz Sharif, na Oktoba 12, 1999, akawa kiongozi wa serikali ya Pakistani baada ya kumwondoa madarakani Nawaz Sharif katika mapinduzi yasiyo na umwagaji damu.

Musharraf alikuwa jenerali wa nne wa Pakistan kutawala nchi hiyo kwa miaka tisa kupitia njia ya mapinduzi. Hatimaye alitangaza kujiuzulu wadhifa wake wa urais katika hotuba yake kwa njia ya televisheni mnamo Agosti 18, 2008, baada ya mirengo ya upinzani katika Bunge la Pakistan kutia kumfungulia mashtaka na kumuondoa madarakani.

Musharraf aliaga dunia tarehe 5 Februari 2023, katika hospitali huko Dubai akiwa na umri wa miaka 79 baada ya kustahamili ugonjwa kwa muda mrefu.