Apr 05, 2025 02:39 UTC
  • Jumamosi, tarehe 5 Aprili 2025

Leo ni Jumamosi tarehe 6 Shawwal 1446 Hijria sawa na Aprili 5 mwaka 2025.

Siku kama ya leo miaka 660 iliyopita, alifariki dunia Ibn Bardes, malenga na mpokezi wa Hadithi wa Kiislamu.

Ibn Bardes alizaliwa huko Baalbek moja kati ya miji ya Lebanon na kuelekea katika mji wa Damascus Syria baada ya kukamilisha masomo yake ya awali, ambapo alinufaika na elimu ya maulamaa maarufu wa zama hizo.

Msomi huyo wa Kiislamu alisafiri katika nchi mbalimbali za Kiislamu na akaanza kufundisha baada ya kukamilisha masomo yake. Alikuwa mashuhuri baina ya watu kwa kushikamana na dini, kutakasa nafsi na maadili mema. Miongoni mwa vitabu vya Ibn Bardes ni al Iilamu fii Wafayatil Aalam.

Siku kama ya leo miaka 440 iliyoyopita yaani 5 Aprili 1585, yalifanyika mauaji ya halaiki katika mji wa Harlem nchini Uholanzi, ambacho kilikuwa kitovu cha wapigania uhuru nchini humo.

Mauaji hayo yalifanyika kwa amri ya Mfalme wa Uhispania. Jumla ya watu elfu sita wanaaminika kuwa waliuawa kwenye shambulio hilo. Hatimaye Uholanzi ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Uhispania hapo mwaka 1609. 

Harlem, Uholanzi

Katika siku kama hii ya leo miaka 437 iliiyopita alizaliwa mwanafalsafa wa Uingereza, Thomas Habbes. Alihitimu masomo katika Chuo Kikuu Oxford nchini Uingereza na alifanya utafiti mkubwa kuhusiana na falsafa.

Habbes aliathiriwa sana na fikra za mwanafalsafa Mtaliano Niccolò Machiavelli na alijifunza mengi kutokana na yaliyokuwa yakijiri duniani. Aliamini kuwa mfalme alipaswa kuwa na utawala usio na mipaka na kwamba watu hawapaswi kulalamikia mtawala hata kama malalamiko yao ni sahihi na kwamba walalamikaji walipaswa kukandamizwa.

Mwanafalsafa huyo wa Kiingereza alifariki dunia tarehe 4 Desemba mwaka 1679 akiwa na umri wa miaka 91. 

Thomas Habbes

Tarehe 5 Aprili miaka 231 iliyopita, aliuawa Georges Danton mmoja kati ya viongozi wa mapinduzi ya Ufaransa.

Danton licha ya kusomea taaluma ya sheria, alikuwa mhamasishaji mzuri katika kipindi cha mapinduzi ya Ufaransa. Danton alikuwa akiamini kuwa, sanjari na kuzuia machafuko na maafa ya kibinadamu, utawala wa kifalme nchini Ufaransa ulipaswa kutokomezwa. Amma Robes Pierre mmoja kati ya vinara wakubwa wa mapinduzi ya Ufaransa ambaye pia alikuwa mshindani wa Danton alichukua uamuzi wa kumtia mbaroni Danton na hatimaye kumuuwa.

Georges Danton

Na siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Aprili 1956, yalimalizika mashambulizi ya kinyama ya majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina katika eneo la Ukanda wa Gaza.

Majeshi hayo, tarehe 4 Aprili, yalianza kufanya mashambulio makubwa na kuwauwa watu 56 na kuwajeruhi wengine 30 wengi wao wakiwa wanawake, watoto na wazee katika kipindi cha siku mbili.

Nchi za Magharibi na jamii ya kimataifa hazikutoa radiamali yoyote kuhusiana na jinai hizo za Wazayuni. 

Gaza