May 01, 2025 02:18 UTC
  • Alkhamisi, tarehe Mosi Mei, mwaka 2025

Leo ni Alkhamisi tarehe 3 Dhulqa'dah 1446 Hijria, inayosadifiana na tarehe Mosi Mei, mwaka 2025.

Siku kama ya leo miaka 136 iliyopita yaani tarehe Mosi Mei 1889, ilitangazwa rasmi kuwa 'Siku ya Wafanyakazi Duniani'.

Tarehe Mosi Mei 1886, zaidi ya wafanyakazi elfu 40 walifanya maandamano katika mji wa Chicago nchini Marekani kwa shabaha ya kudai haki zao. Wafanyakazi hao walitaka nyongeza za mishahara, kuboreshwa suhula za maeneo yao ya kazi na uadilifu kazini. Maandamano hayo yaliingiliwa na askari polisi, na matokeo yake yakawa ni idadi kadhaa ya wafanyakazi hao kuuawa na wengine kujeruhiwa.   

Siku kama ya leo miaka 110 iliyopita, sawa na tarehe Mosi Mei 1915, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia yalitokea mapigano makali kati ya majeshi ya Urusi na Ujerumani katika eneo la Krakow lililoko nchini Poland.

Jeshi la Ujerumani lililoyashinda majeshi ya Urusi kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia mwaka 1914, katika vita hivyo kwa kutumia mizinga liliyashinda majeshi ya Urusi na hatimaye kulidhibiti eneo la Poland. Kushindwa kwa majeshi ya Urusi katika Vita vya Kwanza vya Dunia na hali kadhalika hali mbaya iliyokuwemo nchini humo, ni miongoni mwa sababu muhimu za kujiri mapinduzi ya Kikomonisti nchini humo mwaka 1917, na hatimaye nchi hiyo kujiondoa kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia.  

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, tarehe 3 Dhulqa'dah 1419 Hijria, Ayatullah Sayyid Muhammad Sadr, mmoja wa wanazuoni wakubwa wa Kiislamu na viongozi wa kidini aliuawa shahidi na utawala wa Saddam Hussein nchini Iraq. 

Sayyid Muhammad Sadr alizaliwa tarehe 17 Rabiu'l-Awwal mwaka 1362 Hijiria. Alijiunga na safu ya wanazuoni wa kidini akiwa na umri wa miaka 11. Alibobea katika sayansi za Kiislamu, lugha ya Kiingereza, sosholojia, saikolojia na historia.

Sayyid Sadr alikamatwa na kufungwa jela mara kadhaa na serikali ya Baath ya Iraq mwaka 1972, 1974, na 1991, lakini baada ya matukio ya 1991 nchini Iraq, alitambulishwa kama marejeo rasmi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia wa Iraq na kukabidhiwa usimamizi wa chuo cha kidini cha Najaf.

Ayatullah Sayyid Muhammad Sadr, ambaye alikuwa akipambana dhidi ya utawala wa Baath wa Saddam kwa miaka mingi, hatimaye aliuawa kishahidi na maajenti utawala wa Baathi tarehe 3  Dhulqa'dah 1419.

Encyclopedia ya Imam Mahdi katika juzuu 4; tafsiri ya Qur'ani ya Minnatul Mannan yenye ya juzuu tano, Fiqhul-Akhlaq, na Maa Wara al-Fiqh ni baadhi ya kazi za msomi huyo wa Kiislamu.     

Ayatullah Sayyid Muhammad Sadr

Na miaka 20 iliyopita katika siku kama hii, tarehe Mosi Mei 2004, nchi nyingine 10 za Ulaya zilijiunga na Umoja wa Ulaya na kufikisha jumla ya nchi 25 wanachama wa umoja huo.

Nchi hizo ni Estonia, Latvia, Lithuania, Poland, Jamhuri ya Czeck, Slovakia, Hungary, Slovenia, Cyprus, na Malta. Licha ya kuwa kujiunga nchi hizo kulihesabiwa na jumuiya hiyo kuwa moja ya mafanikio, lakini kuna ufa wa kisiasa, kiuchumi na kijamii kati ya nchi wanachama wa zamani na wapya.

Vilevile mwaka 2007, nchi za Romania na Bulgaria zilijiunga na umoja huo na jumla ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kufikia 27.