Jul 12, 2025 02:36 UTC
  • Jumamosi, 12 Julai, 2025

Leo ni Jumamosi 16 Mfunguo Nne Muharram 1447 Hijria sawa na 12 Julai 2025 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1314 iliyopita, kwa mara ya kwanza katika historia ya mapambano ya Waislamu, akiwa na jeshi kubwa la Kiislamu Twariq bin Ziyad aliweza kuingia Uhispania. Ushindi huo ulikuwa mwanzo wa maendeleo ya Waislamu barani Ulaya ambapo uliendelea hadi Ufaransa ya sasa. Twariq bin Ziyad aliwasili Uhispania baada ya kuvuka lango bahari kati ya Morocco na Uhispania linalojulikana kwa jina lake mwenyewe yaani "Jabal Tariq." Mlango bahari huo unatumika kama njia ya mawasiliano kati ya Bahari za Atlantic na Mediterranean. Waislamu walitawala kwa karne nane huko Uhispania na kueneza mafunzo na utamaduni wa Kiislamu barani Ulaya baada ya kutekwa Andalusia, moja ya maeneo ya hispania ya leo. 

Twariq bin Ziyad

 

Miaka 792 iliyopita katika siku kama ya leo, bandari ya kihistoria ya Alexandria huko Misri ilizingirwa na meli za kivita za Jeshi la Msalaba. Wakati huo Salahuddin Ayyubi alikuwa gavana wa Alexandria na hakuweko katika mji huo wakati maadui walipofanya mashambulizi. Hata hivyo wapiganaji wa Kiislamu walikabiliana kwa nguvu na Jeshi la Msalaba hadi gavana Salahuddin alipowasili. Wanajeshi wa Uholanzi waliokuwa katika safu ya mbele walipigwa vibaya na kulazimika kurudi nyuma. 

 

Siku kama ya leo miaka 20۸ iliyopita, alizaliwa Henry David Thoreau, msomi na mwanaharakati wa Kimarekani. David alikuwa akiheshimu mazingira asilia kama viumbe vya Mwenyezi Mungu na alisifika kwa kuwa na akhlaqi na maadili mema. Henry David alikuwa akisisitiza kuwa, haifai kuangamiza maisha ya wanadamu kwa tamaa ya kufikia mali na fedha nyingi. Aidha mwanaharakati huyo, aliamini kuwa kama vile ambavyo serikali inavyomuadhibu mtu mkosefu, kadhalika inapotokea serikali hiyo ikashindwa kutekeleza wadhifa wake wa kiuongozi, basi wananchi nao wanatakiwa kuipa adabu serikali hiyo sanjari na kuiondoa madarakani. Miongoni mwa athari muhimu za Henry David Thoreau ni pamoja na kitabu cha 'Uasi wa Kiraia' na alifariki dunia mwaka 1862. 

Henry David Thoreau

 

Siku kama ya leo miaka 90 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, ilianza harakati ya Waislamu wa Mashhad, moja ya miji ya kidini ya Iran, inayojulikana kama Harakati ya Msikiti wa Goharshad. Katika siku hii, Waislamu na watu wapiganaji wa Mashhad, wakiongozwa na maulama waliojitolea na wanamapambano wa Mash'had wakiongozwa na viongozi wa kidini walisimama dhidi ya ukandamizaji wa Reza Khan Pahlavi na hatua zake za kuharibu utamaduni wa Kiislamu nchini Iran na kulazimisha utamaduni wa kigeni. Miongoni mwa hatua hizo ilikuwa ni amri ya Reza Khan ya kuondoa hijabu kwa nguvu kwenye vichwa vya wanawake wa Kiislamu, lakini watu walipinga mipango ya Reza Khan ya kupinga dini na wakasimama dhidi yake. Harakati hii ilifikia kilele chake katika Msikiti wa Goharshad karibu na kando ya haram takatifu ya Imam Ridha (AS), na maajenti wa Reza Khan walikandamiza harakati hiii kwa kuwapiga na kuwaua watu.

 

Tarehe 12 Julai miaka 79 iliyopita, Hoteli ya Mfalme Daud huko Baitul Muqaddas iliripuliwa kwa bomu na kundi la Kizayuni la Irgun. Hoteli hiyo ilikuwa ikitumiwa sana na raia wa Palestina. Bomu lililokuwa limetegwa ndani ya hoteli hiyo liliripuka na kuuawa watu zaidi ya 200. Kuweko Wayahudi watano miongoni mwa waliouawa katika mlipuko huo kunabainisha wazi namna Wazayuni wasivyothamini hata maisha ya Wayahudi ili kufikia malengo yao ya kujitanua na kuzusha hofu miongoni mwa Wapalestina.   

Hoteli ya Mfalme Daud baada ya mlipuko

 

Siku kama ya leo miaka 19 iliyopita Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine tena lilifanya mashambulizi ya anga na baharini huko Lebanon. Utawala wa Kizayuni ulifanya mashambulizi hayo kwa kisingizio cha kukamatwa mateka wanajeshi wake wawili na wapiganaji wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon kupitia oparesheni yake ya kujilinda. Tel Aviv ilifanya mashambulizi hayo ya kijeshi huko Lebanon ikiungwa mkono na Washington lengo lake kuu likiwa ni kuvunja uwezo wa kijeshi wa Hizbullah na kuipokonya silaha harakati hiyo inayohesabiwa kuwa nguvu kuu ya mapambano huko Lebanon mbele ya jeshi ghasibu la utawala wa Kizayuni.