Sep 08, 2016 09:48 UTC
  • Maafa ya Mina (6)

Huu ni mfululizo wa makala hizi maalumu ambazo zinaangazia maafa ya kusikitisha yaliyojiri katika eneo la Mina mwaka jana wakati wa Ibada ya Hija.

Katika makala zilizopita tumekuwa tukisimulia kisa cha kweli cha Haji Mohammad ambaye alishiriki katika ibada ya Hija mwaka jana na amekuwa akisimulia yale aliyoyaona kwa macho yake katika maafa ya Mina mwaka jana. Kisa chake kimefika katika sehemu muhimu na ya mwisho.. Karibuni kusikiliza.

"Mahujaji walikuwa wamebanana sana kutokana na kuwepo idadi kubwa ya watu na joto kali. Mmoja baada ya mwingine walianza kuzimia na kupoteza fahamu huku wengine wakiaga dunia. Nilikuwa nimechoka sana na hapo nikatamka shahada mbili na kujitayarisha kuaga dunia. Katika fikra yangu ilinijia taswira ya mama yangu, mke na watoto wangu na nilikuwa na matumaini kuwa watanisamehe. Wakati nilipotafakari kuhusu ibada yangu ya Hija ambayo sikuwa nimefanikiwa kuikamilisha, nilipata masikitiko makubwa kuwa sikuwa nimeweza kukamilisha tamanio langu kubwa katika maisha. Nilikuwa na matumaini kuwa Mwenyezi Mungu ataikubali Hija yangu yenye nakisi na awaadhibu waliohusika na jinai hii.

Maafa ya Mina

 

Katika lahadha hii ya kutokuwa na matumaini, nilifungua macho yangu kwa muda mfupi na nikaona Mahujaji kadhaa wakija upande niliokuwa. Hapo moyo wangu ulipata matumaini. Walikuwa wakiwachukua kwa kasi watu waliokuwa wakionekana kuwa hai miongoni mwa Mahujaji waliokuwa wamekanyagana na kuanguka. Kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, niliweza kuinua mkono wangu juu ili waokoaji wanione na waninusuru katika hali hiyo. Nilijitahidi kadiri nilivyoweza kubakia hai. Nilijitahidi kujikwamua kutoka miongoni mwa watu wengi waliokuwa wamerundikana katika eneo hilo. Katika lahadha hiyo ndugu yangu miongoni mwa Mahujaji waokoaji alininyanyua na kunikumbatia. Nilimshukuru sana kwa msaada wake, lakini hakuwa na wakati wa kuzungumza nami kwani alikuwa akiharakisha ili awanusuru Mahujaji wengine. Hapo muokoaji mwingine miongoni mwa Mahujaji alinipa maji ya kunywa. Katika hali hiyo ya jua kali na msongamano mkubwa niliweza kutambua umuhimu wa maji katika maisha. Nikiwa nimekaa pembeni baada ya kunusuriwa, sikuona hata afisa mmoja muokoaji kutoka mashirika ya Saudia."

Mnaendelea kusikiliza kipindi cha maafa ya Mina ambapo tunaangazia kisa cha kweli cha Haji Mohammad kutoka Iran aliyeshiriki katika ibada ya Hija mwaka uliopita na anayeendelea kusimilua yaliyomsibu katika maafa hayo na namna alivyoshuhudia watu wakipoteza maisha.

Mohammad anaendelea kusema: "Waokoaji kutoka nchi mbali mbali walifika katika eneo la maafa ya Mina na kwa mbali nilishuhudia namna walivyokuwa wakijitahidi  kuwaokoa mahujaji waliokuwa wamerundikana. Kwa hakika jitihada za waokoaji wa kigeni katika maafa ya Mina ni zenye kustahiki pongezi. Hatimaye baada ya kupita masaa mawili tokea yajiri maafa ya Mina, waokoaji wa Saudi Arabia walijitokeza. Pamoja na kuwa, walikuwa karibu sana na eneo la tukio na walikuwa na vifaa vinavyofaa ili kukabiliana na maafa kama hayo, lakini hawakufanya lolote la maana kuwasaidia waathirika. Masaa matatu baada ya tukio maafisa wa usalama wa Saudia walifika katika eneo hilo na kuwazuia waokoaji kutoka nchi ziginezo kuwasaidia waathirika. Baada ya kutimuliwa waokoaji wa kigeni, maafisa wa Saudia walitumia fursa hiyo kufanya kila wawezalo  kuficha mengi kuhusu maafa hayo."

Maafa ya Mina

 

Haji Mohammad kutoka Iran anaendelea kusimulia yaliyomsibu katika maafa ya Mina mwaka jana wakati wa ibada ya Hija kwa kusema:" Nilianza kupata nafuu kidogo na kutokana na msaada niliokuwa nimeupata, nilijiunga na msafara wangu. Baada ya wenzangu tuliokuwa nao katika msafara kuniona walifurahi sana na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuninusuru na kisha wakaendeleza jitihada za kuwatafuta wengine waliokuwa wametoweka.

Qarii Muhsin Haj Hassani

 

Lakini kutokana na idadi kubwa ya watu na mkanyagano uliokuwepo,  ilikuwa vigumu sana kuwatafuta wenzetu. Msafara wetu na misafara mingine 50 ya Wairani ilikuwa katika mbano mkubwa sana na hali ilikuwa ya kuogofya na kusikitisha. Majonzi yalikuwa yameenea kutokana na kuwa wanawake walikuwa wamewapoteza waume, watoto wao wa kiume au ndugu zao. Kila wakati tulikuwa tunapokea habari mpya.

Maafisa wa Saudia walijaribu kuficha ukubwa wa maafa na hivyo walifanya kila waliloweza kuhakikisha hali inarejea kuwa ni ya kawaida hapo Mina. Kwa msingi huo walianza kukusanya miili iliyokuwa imetapakaa ardhini. Kutokana na haraka waliyokuwa nayo na pia kwa vile hawakuwa wakijali kuokoa maisha, watu wengi waliokuwa hai lakini ambao hawakua na fahamu walichukuliwa na kurundikwa pamoja na maiti katika malori na makontena yaliyokuwa yakielekea katika vyumba vya kuhifadhia maiti. Hivyo idadi kubwa ya Mahujaji ambao walikuwa hai waliuawa na maafisa wa Saudia ambao waliwachanganya na waliokuwa wamefariki katika maafa ya Mina.

"Katika maafa ya Mina mwaka jana, kulikuwa na Mhujaji wawili mwaka jana ambao majina yao yalikuwa mashuhuri zaidi kuliko wengine wote katika msafara wa Iran. Wa kwanza ni Ghazanfar Ruknabadi, balozi wa zamani wa  Iran nchini Lebanon. Alikuwa mtu ambaye Wasaudi walimchukia sana. Wa pili alikuwa Muhsin Haji Hassani, qarii wa Qur'ani Tukufu  ambaye alikuwa mashuhuri kitaifa na pia katika ngazi za kimataifa.

Ghazanfar Ruknabadi

 

Katika kipindi hicho cha maafa ya Mina mwaka jana, Mahujaji walikuwa katika hali ya huzuni, majonzi na hofu kubwa kwani kila wakati kulikuwa na uwezekano wa miili zaidi ya Mahujaji, hasa Mahujaji Wairani kupatikana. Hali ilifanywa kuwa mbaya zaidi kutokana na kuwa maafisa wa Saudia walikuwa na chuki sana dhidi ya Mahujaji Wairani. Katika hali hiyo, kutokana na msimamo imara wa Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na pia maafisa wengine wa ngazi za juu nchini, viwiliwili vya Mahujaji Wairani vilirejeshwa nyumbani

Miili ya Mahujaji Wiarani waliopoteza maisha Mina ilirejeshwa nyumbani katika mazingira yaliyotawaliwa na majonzi makubwa. Kwa kawaida Mahujaji hurejea nyumbani na kusimulia kumbukumbu nzuri za ibada ya Hija, lakini mwaka jana wale walionusurika maafa ya Mina walirejea nyumbani wakiwa katika hali ya majonzi  huku wakiwasimiulia jamaa na marafiki kuhusu masaibu machungu ya maafa makubwa yaliyowakumba."

Katika sehemu kadhaa za mfululizo wa makala zetu kuhusu Maafa ya Mina tumesikiliza kumbukumbu ya Hajj Mohammad kutoka Iran ambaye alishuhudia kwa macho yake mwenyewe yaliyojiri katika maafa hayo ya mwaka jana. Makala yetu ya leo inatutamatishia kumbukumbu ya Hajj Mohammad. Katika makala ijayo tutajadili Maafa ya Mina kwa mtazamo mwingine.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Tags