Nov 17, 2016 04:28 UTC
  • Alkhamis, Novemba 172016

Leo ni Alkhamisi tarehe 17 Safar 1438 Hijria sawa na 17 Novemba 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 147 iliyopita ulifunguliwa Mfereji wa Suez unaounganisha Bahari ya Mediterania na Bahari Nyekundu. Uchimbaji wa mfereji huo ulisimamiwa na mhandisi wa Kifaransa Ferdinand de Lesseps katika kipindi cha miaka 10 huku ukiwa na urefu wa kilomita 168 na upana wa mita 120 hadi 200. Karne kadhaa kabla yake, Mfalme Daryush wa Iran na baadhi ya wafalme wa Misri walichukua hatua kadhaa za kuanzisha mfereji baina ya bahari hizo mbili, suala ambalo linaonyesha umuhimu wa Mfereji wa Suez unaopunguza kwa kiasi kikubwa masafa ya kutoka Asia kuelekea Ulaya, safari ambayo zamani ilikuwa ikifanyika kupitia Afrika Kusini.

Tarehe 17 Novemba siku kama ya leo miaka 34 iliyopita Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiislamu la Iraq liliasisiwa kutokana na vyama na makundi mbalimbali yaliyokuwa yakiupinga utawala wa dikteta Saddam Hussein. Lengo la kuasisiwa baraza hilo lilikuwa ni kuwaokoa wananchi wa Iraq na dhulma pamoja na ukandamizaji wa utawala wa Chama cha Baath. Kufuatia mashambulio ya kijeshi ya Marekani nchini Iraq na kuangushwa utawala dhalimu wa Saddam, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiislamu la Iraq, lilihamishia harakati zake za kisiasa ndani ya ardhi ya Iraq na kuwa na nafasi muhimu katika uwanja huo.

Siku kama ya leo miaka 183 iliyopita, alizaliwa Sheikh Abdulrahim Sultanul Qurraa Tabrizi, msomaji mashuhuri wa Qur'ani Tukufu na mmoja wa walimu wakubwa wa qiraa ya Qur'ani. Alizaliwa katika mji wa Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran. Baadaye Sheikh Abdulrahim Sultanul Qurraa aliasisi shule ya kutoa mafunzo ya Qur'ani Tukufu huko Tabriz na ni wakati huo ndipo alipopewa lakabu ya Sultanul Qurraa kwa maana ya mfalme wa maqari na wasomaji Qur'ani Tukufu. Msomaji huyo mkubwa wa Qur'ani ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha Risala katika Elimu ya Tahwidi. Mwanazoni huyo alifariki dunia mwaka 1336 Hijria katika mji wa Tabriz nchini Iran.

Na Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita wiki mbili tu baada ya wanafunzi wa vyuo vikuu hapa nchini kuteka ubalozi wa Marekani mjini Tehran ambao ulitambuliwa kuwa pango la ujasusi la nchi hiyo, mateka wanawake na weusi wenye asili ya Afrika waliokamatwa katika ubalozi huo waliachiwa huru kwa amri ya hayati Imam Ruhullah Khomeini. Ubalozi huo ulikuwa kituo cha ujasusi na kupanga njama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa sababu hiyo wafanyakazi wake walishikiliwa mateka kama majasusi wa Marekani hapa nchini. Hata hivyo Imam Khomeini na kwa sababu za kibinadamu na vilevile kwa kutilia maanani kwamba, wanawake na Wamarekani weusi wanadhulumiwa na kubaguliwa nchini kwao, alitoa amri waachiwe huru. Sehemu moja ya barua ya hayati Imam Khomeini kwa wanafunzi wa vyuo vikuu waliokuwa wakiwashikilia mateka wamarekani hao inasema: Uislamu umetunga sheria makhsusi kwa ajili ya wanawake, na watu weusi kwa miaka mingi wamekuwa chini ya mashinikizo na dhulma za Marekani na pengine wamelazimishwa kuja Iran. Kwa msingi huo wapeni tahfifu iwapo haitathibitika kwamba wamefanya ujasusi", mwisho wa kunukuu. Kwa utaratibu huo mateka 13 wa kike na wale wenye asili ya Afrika waliachiwa huru.

 

 

 

Tags