Nov 20, 2016 05:59 UTC
  • Jumapili, 20 Novemba, 2016

Leo ni Jumapili tarehe 20 Swafar 1438 Hijria, sawa na tarehe 20 Novemba mwaka 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1377 iliyopita, ilienziwa siku ya 40 tangu alipouawa shahidi Imamu Hussein (as) mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) na watu wake wa karibu. Katika tukio hilo, tarehe 10 mwezi Muharram mwaka 61 Hijiria, Imamu Hussein (as) akiwa na wafuasi wake 72 waliokuwa na imani thabiti walipambana kishujaa na jeshi la mtawala dhalimu Yazidi mwana wa Muawiya, ambapo katika makabiliano hayo jeshi la mtawala huyo liliwaua shahidi na kwa dhulma watu wa familia ya Mtume wa Mwenyezi Mungu huku waliosalia hai wakitekwa nyara. Ni kwa ajili hiyo ndio kila baada ya siku 40 kila mwaka, kukawa kunafanyika marasimu ya kukumbuka tukio hilo chungu, marasimu ambayo yanaitwa ‘Arubaini’ ambapo kwa mara nyingine huamsha hamasa ya kumbukumbu ya siku ya Ashura sanjari na kuhuisha nafasi ya juu ya Imamu Hussein (as) na sira ya Mtukufu Mtume Muhammad (saw). Aidha katika siku kama ya leo na kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, msafara wa Ahlu Bayti wa Mtume ulifika tena mjini Karbala kutoka Sham, baada ya kufichua maovu ya mtawala Yazidi na kuweka wazi njama zake chafu dhidi ya Uislamu. Kwa mujibu wa historia, msafara huo wa watu wa karibu wa Imamu Hussein, ulikutana hapo Karbala na sahaba mkubwa wa Mtume (saw) Jabir Bin Abdillah al-Answar ambaye baada ya kupata habari ya kuuawa shahidi mjukuu huyo wa Nabii wa Allah, alifika hapo kwa ajili ya kuzuru kaburi la mtukufu huyo yaani Imamu al-Hussein (as).

Siku kama ya leo miaka 123 iliyopita, alizaliwa mjini Najaf, Iraq, Ayatullahil-Udhma Mar’ashi Najafi, mmoja wa maulama wakubwa wa ulimwengu wa Kiislamu. Baba yake alikuwa Sayyid Shamsud-Din Mahmud Mar’ashi, mmoja wa wasomi wakubwa wa sheria za Kiislamu (fiqhi) katika zama zake. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali ya dini ya Kiislmu mjini hapo Najaf, Ayatullahil-Udhma Mar’ashi Najafi aliendeleza masomo yake ya juu ya fiqhi na Usulu Fiqhi kwa maulama wakubwa kama vile Agha Dhiyaau Iraqi na Sheikh Ahmad Kashiful-Ghitwaa. Akiwa na umri wa miaka 27 alifikia daraja la Ijtihadi. Kadhalika Ayatullahil-Udhma Mar’ashi Najafi, alipata kusoma elimu ya dini ya Kiislamu mjini Najaf, Kadhimiya, Karbala, Samarra, Qum, Tehran na Kermanshah. Moja ya vitu muhimu sana alivyoviacha ni maktaba kubwa iliyopewa jina lake mjini Qum aliyoianzisha mnamo mwaka 1344, ambapo ndani yake kuna vitabu vya thamani sana. Maktaba hiyo hadi sasa ina zaidi ya vitabu laki mbili na 50 elfu. Ayatullahil-Udhma Mar’ashi Najafi, alifariki dunia mjini Qum, Iran tarehe 7 Swafar mwaka 1411 Hijiria.

Siku kama ya leo miaka 118 iliyopita, alizaliwa Edwin Hubble, mtaalamu wa elimu ya nyota wa Kimarekani. Awali alijiunga na chuo kikuu kusomea sheria kwa pendekezo la baba yake, hata hivyo baada ya kuhitimu alipendelea sana kusomea masuala ya nyota. Hivyo akaamua kusomea taaluma hiyo. Katika harakati hiyo Edwin Hubble aliufanyia utafiti mkubwa mrundikano mkubwa wa mawingu na pia vumbi na gesi angani. Kadhalika alithibitisha kupishana sayari nje ya mfumo wa Milky Way, kama ambavyo pia aliamini nadharia ya kupanuka kwa dunia. Edwin Hubble alifariki dunia mwaka 1953 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 106 iliyopita alifariki dunia mwandishi mashuhuri wa Kirusi Leo Tolstoy. Mwandishi huyo alizaliwa mwaka 1828 na aliondokewa na baba na mama yake akiwa angali mdogo. Alifanya safari za kitalii na uchunguzi katika jamii nyingi za Ulaya na mambo aliyoyashuhudia katika safari hizo yalimfanya achukie ustaarabu wa kimaada wa nchi za Magharibi. Tolstoy alilipa umuhimu mkubwa suala la kuwapa elimu na malezi watoto wadogo na alikuwa akijitahidi mno kusaidia matabaka ya watu maskini na wasiojiweza. Leo Tolstoy ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha "Kiyama", "Kipindi cha Utotoni" na riwaya ya "Vita na Amani".
Siku kama ya leo miaka 96 iliyopita, yaani tarehe 20 Novemba mwaka 1920, mapambano makubwa ya wananchi wa Iraq dhidi ya wakoloni wa Kiingereza yalishindwa. Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na kusambaratika utawala wa Kiothmania, serikali za Ufaransa na Uingereza ziligawana ardhi za utawala huo Mashariki ya Kati. Kwa msingi huo Uingereza ilichukua Iraq na kukabiliwa na mapambano makali ya wananchi tangu mwanzoni. Mapambano hayo yaliongozwa na wanazuoni wa Kiislamu waliotoa wito wa kufukuzwa wakoloni wa Kiingereza na kuundwa serikali huru ambayo ingezingatia sheria za Kiislamu.
Na siku kama ya leo miaka 66 iliyopita majeshi ya Marekani na China yalipambana ana kwa ana kwa mara ya kwanza kabisa katika vita vya Peninsula ya Korea. Mapigano hayo yalitokana na himaya na uungaji mkono wa Marekani kwa Korea Kusini na uungaji mkono wa China na Urusi kwa Korea Kaskazini. Vita vya Korea vilisababisha hasara kubwa sana kwa pande zote mbili. Vita hivyo vilisimama kutokana na upatanishaji wa Umoja wa Mataifa na hadi sasa Korea Kaskazini na Kusini zimebakia nchi mbili zilizojitenga.

 

 

 

 

Tags