Alkhamisi, 26 Januari, 2017
Leo ni Alkhamisi tarehe 27 Rabiuthani, 1438 Hijria, sawa na Januari 26, 2017.
Miaka 194 iliyopita, yaani mwaka 1749 alifariki dunia Edward Jenner tabibu wa Kiingereza aliyegundua chanjo ya ndui yaani (small pox). Jenner alizaliwa mwaka 1749 Miladia. Tabibu huyo alifanikiwa kugundua chanjo ya ndui akiwa na umri wa miaka 45 wakati alipoelekea nchini India. Kuanzia hapo ugonjwa huo wa ndui uliweza kutibiwa kwa kutumia chanjo hiyo. Na ilipofika mwaka 1979 maradhi hayo yaliweza kutokomezwa kabisa duniani.
Miaka 67 iliyopita na katika siku kama ya leo, mfumo wa utawala wa serikali ya Jamhuri ulishika hatamu za uongozi nchini India, baada ya nchi hiyo kujitangazia rasmi uhuru wake mwaka 1947 toka kwa mkoloni Muingereza na Rais wa kwanza wa nchi hiyo akawa Dakta Rajendra Prasad. Rais huyo aliingoza India kwa muda wa miaka 7. Hata hivyo kwa mujibu wa mfumo wa kisiasa wa India, rais wa nchi hana nguvu na madaraka ya utendaji, bali Waziri Mkuu ndiye mwenye nguvu na mamlaka ya utendaji.
Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari, faqihi na marjaa mkubwa wa Kishia. Akiwa na umri wa miaka 20, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Najaf, Iraq na kustafidi na elimu kutoka kwa wasomi wakubwa kama vile Muhaqqiq Khorasani, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, Shariat Isfahani na Muhaqqiq Naaini. Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari alielekea mjini Arak, Iran katika kipindi cha kuasisiwa chuo cha hauza cha mji huo na kujishughulisha na ukufunzi. Baadaye msomi huyo alishirikiana na Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi katika shughuli za tablighi na baada ya kuasisiwa hauza ya Qum, chini ya usimamizi wa Ayatullah Hairi Yazdi, Ayatullah Ahmad Khansari alikuwa imamu wa Swala ya jamaa katika chuo cha Faiziya mjini humo. Alishirikiana bega kwa bega na wanazuoni wa Kiislamu wakiongozwa na hayati Imam Ruhullah Khomeini katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala muovu wa Shah. Msomi huyo amelea na kufunza wasomi wakubwa kama Ayatullah Murtadha Mutahhari, Imam Musa Sadr na Sayyid Ridha Sadr. Mwaka 1370 Hijiria, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Tehran na kuwa imamu wa Swala ya jamaa katika msikiti maarufu wa ‘Sayyid Azizullah’. Ameandika vitabu vingi katika taaluma za sheria na teolojia ya Kiislamu.
Na siku kama ya leo miaka 14 iliyopita, alifariki dunia mtaalamu wa masuala ya Kiislamu wa Ujerumani, Bi Annemarie Schimmel. Bibi Schimmel alipendelea mno kutalii na kupata maarifa kuhusu ustaarabu wa Kiislamu na alipata shahada ya uzamivu katika taaluma ya masuala ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Berlin akiwa na umri wa miaka 19. Prf. Annemarie Schimmel alifundisha kwa miaka mingi historia ya dini na irfani ya Kiislamu katika vyuo vikuu vya Marekani, Ujerumani na Uturuki. Mbali na kujua lugha za Kijerumani na Kiingereza, Bi Schimmel alijifunza pia lugha za Kiarabu, Kifarsi, Kiurdu, Kibengali na Kituruki kwa ajili ya kupata maarifa zaidi kuhusu masuala ya Kiislamu.
Prf. Annemmarie Schimmel ameandika vitabu kadhaa kuhusu masuala ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na kile cha "Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu" na "Mwanamke katika Irfani ya Kiislamu".
