Maadhimisho ya Ushindi ya Mapinduzi ya Kiislamu (5)
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya mfululizo wa vipindi hivi vinavyokujieni kwa mnasaba wa Maadhimisho ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliyotokea mwaka 1979 kwa uongozi wa Imam Ruhullah Khomeini MA, hii ikiwa ni sehemu ya tano ya mfululizo huu.
Chuki dhidi ya Uistikabri na Ubeberu ni miongoni mwa misingi isiyobadilika na isiyotetereka ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hatua ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ya kupinga Ubeberu na kutoukabali Uistikabari iliupatia ulimwengu fikra mpya; na mtazamo huu wa ukombozi ulikuwa changamoto ni kubwa kwa madola makubwa ya kibeberu ulimwenguni.
Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu uliotokea Februari mwaka 1979 baada ya kuuangushwa utawala wa kifalme wa Shah uliokuwa kibaraka wa Marekani, lilikuwa tukio muhimu mno katika uhusiano wa Iran na ulimwengu wa nje na mabadiliko haya yalitosha kuisukuma Washington na washirika wake wafanye kila njama kwa ajili ya kukabiliana na mfumo wa mapinduzi uliokuwa ndio kwanza mche mchanga unaochipua nchini Iran. Jamhuri ya Kiislamu ilikuja na kumuweka kando mmiliki bandia na kukabidhi mamlaka ya nchi kwa wamimiliki wake wa asili ambao ni wananchi, ambao huchagua viongozi kupitia uchaguzi, hujitokeza katika medani mbalimbali za maamuzi, wasipotaka wanapinga jambo fulani na wakitaka kitu fulani husimama na kulithibitisha hilo. Kwa hakika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuja na kusambaratisha ngome ya adui na kufungua ukurasa mpya katika historia ya nchi hii.
Hivi sasa inapita miaka 38 tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulipopatikana nchini Iran na tukio hili muhimu lingali lina mvutano mno kwa wanafikra na waandishi mbalimbali ulimwenguni. Hii ni kutokana na kuwa, tukio hili kubwa kwa upande mmoja lilileta wimbi la shauku na matumaini baina ya Waislamu na wastaadhaafu ulimwenguni; na kwa upande mwingine lilivuruga mahesabu ya kisiasa ya Uistikbari katika mwendelezo wake wa siasa za kibeberu na ugawanyaji wa kikoloni ulimwenguni. Katika fikra na kivitendo, Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kupinga na kutoukubali Ubeberu na wakati huo huo kusimama na kutetea haki za Waislamu wote na kutokuwa na mfungamano makabala na madola makubwa ya kibeberu, ni mambo ambayo yaliufanya Uistikbari wa dunia na madola ya Magharibi kukasirika na kughadhibika mno na hatua iliyofuata ilikuwa ni kuanzisha uadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sanjari na kusisitiza juu ya kusimama kidete mkabala na dhulma na ukosefu wa uadilifu, ilitangaza bayana mpango na ramani yake ya njia ya fikra zake za kisiasa.
Tangu awali Jamhuri ya Kiislamu ilisema na kuthibitisha kwamba, haitolegeza kamba katika kukabiliana na utumiaji mabavu, dhulma, utwishaji mambo, mashinikizo na matarajio ya Waistikabri wa dunia; na kwamba katu haitaacha kutetea malengo na matukufu yake.
Kwa haki fikra hii mpya ulikuwa mwanga wenye taathira kilimwengu na kwa upande mmoja ilitoa changamoto kwa siasa za kibeberu dhidi ya mataifa dhaifu ulimwenguni na kwa upande wa pili, ilipelekea kuimarika na kupata nguvu matakwa ya kupigania uadilifu ya mataifa dhaifu duniani. Harakati nyingi ulimwenguni zilipata ilhamu ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuyafanya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kuwa kigezo na ruwaza njema kwa ajili ya kujikomboa na kufikia katika haki zilizoporwa na kukanyagwa.
Hamid al-Khalifa, mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema:
Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ni moja ya matukio makubwa kabisa yaliyotokea katika nusu ya pili ya karne ya ishirini. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliathiri mataifa na nchi nyingi na kutoa fursa mpya mbele ya harakati za mapambano ya kupigania uhuru na ukombozi.
Kwa hakika Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalikuja na kuzungumzia uwezo mkubwa na thamani za kibinadamu na kusisitiza juu ya misingi ambayo haki zake zilikuwa zimewekwa katika hifadhi ya Magharibi na kuanza kusahauliwa. Hii ni katika hali ambayo, watu waliodhulumiwa walikuwa wakitaka kutekelezwa uadilifu duniani. Hapana shaka kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaraji kwamba, misingi hii iungwe mkono na madola ya Kiistikbari. Ukweli ni kuwa, muamala wa madola hayo umedhihirisha ghadhabu na hasira zilionayo kwa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Martin Indyk mwanadiplomasia wa zamani wa Marekani anasema:
Kuyaadhibu Mapinduzi ya Kiislamu, kutakuwa funzo na ibra kwa nchi ambazo zinapiga hatua katika njia ya kutaka kujitawala na kujivua na ubeberu wa Marekani.
Ukweli wa mambo ni kuwa, uadui wa madola yanayotumia mabavu dhidi ya mfumo mchanga wa Jamhuri ya Kiislamu katika kipindi hicho ulitokana na kuwa, mfumo huo ulikuwa kigezo kipya kwa wanadamu wenye fikra huru hususan Waislamu.
Noam Chomsky mwandishi mashuhuri wa Kimarekani yeye anaamini kuwa, uadui, njama na upinzani wa Marekani na madola ya Magharibi dhidi ya Iran chimbuko lake ni fikra ya kujitawala Iran na kutokubali taifa hili kuburuzwa na Ubeberu na Uistikbari wa Magharibi.
Chomsky anasema: Madhali Iran itaendelea kuwa yenye kujitawala na kutopiga magoti mbele ya ubeberu wa Marekani, basi uadui na upinzani wa Washington nao utaendelea kushuhudiwa.
Ni jambo lisilo na shaka kuwa, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na hatua yake ya kuwa kigezo cha mwamko wa Kiislamu katika pembe mbalimbali za dunia ulipelekea kufunguliwa ukurasa mpya wa kukabiliana Uislamu na Magharibi. Mwenendo wa uadui na chuki sambamba na njama ulianza katika siku za mwanzo za ushindi wa Mapinduzi na hatua kwa hatua ukapanuka na kuenea huku ukitumia anuai kwa anuai ya mbinu na mikakakati. Marekani na utawala haramu wa Israel zilikuwa tawala zilizokuwa mstari wa mbele na zilizobeba bendera ya chuki na uhasama usio na maridhiano.
Mmoja wa Mawaziri wa zamani wa Ulinzi wa Marekani anasema:
Kwa mtazamo wangu ni kuwa, jambo ambalo ni hatari zaidi na muhimu zaidi kuliko matatizo ya kimataifa ni matokeo ya kuenea misingi ya Kiislamu ambayo jiwe lake la msingi limewekwa nchini Iran. Kama itashindikana kulidhibiti hili, basi maslahi ya madola makubwa yatakuwa katika hatari kubwa mno. Mapinduzi hayo kuwa ni ya Kiislamu ndio sababu kuu ya wasiwasi na upinzani wetu.
Kutokana na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kuleta ufahamu na mwako baina ya mataifa ya wastaadhaafu ulimwenguni hususan katika nchi za Kiislamu yaliandaa mazingira ya mabadiliko ya kisiasa ya kudumu katika uga wa kieneo na kimataifa. Ni jambo lisilo na shaka hata kidogo kwamba, kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba, ni kigezo cha wapigania uhuru na uadilifu na hatua ya mapinduzi haya ya kuwa ni mbebaji wa ujumbe na risala ya uadilifu ni mambo ambayo hayaoani kabisa na maslahi ya Waistikbari na mabeberu duniani.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mara chungu nzima imezungumzia hatima ya mataifa mengine yakiwemo yale yaliyodhulumiwa na kutwishwa vita kama Afghanistan, Iraq, Syria na kwingineko na kusema bayana kwamba, hatua hizo ni dhulma dhidi ya binadamu. Dhulma ambayo imefanywa na inaendelea kufanywa na madola ya kibeberu.
Hii leo kama katika kila nukta ya dunia kuanzia Bahrain hadi Myanmar au barani Afrika na hata Marekani na Canada, kuna watu wanadhulumiwa na ni wahanga wa uvamizi, dhulma na mauaji ya kikatili, basi natija ya hilo ni siasa za kidhulma za madola makubwa ya kibeberu.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu hiki maalumu kilichokujieni kwa mnasaba wa Maadhimisho ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu unafikia tamati.
Ninakutakieni kila la kheri.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh