Jan 31, 2017 01:10 UTC
  • Jumanne, tarehe 31 Januari, 2017

Leo ni Jumanne tarehe Pili Jamadil Awwal 1438 Hijria inayosadifiana na 31 Januari, 2017.

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita Imam Khomein (MA) Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, alirejea nchini na kupokelewa kwa shangwe kubwa na wananchi baada ya kuishi uhamishoni kwa kipindi cha miaka 15. Mapokezi hayo makubwa ya wananchi wa Iran kwa Imam Khomeini hayajawahi kushuhudiwa mfano wake katika historia ya sasa ya dunia. Baada ya kutoa hotuba fupi katika uwanja wa ndege wa Mehrabad, Imam Khomein alielekea moja kwa moja kwenye makaburi ya mashahidi waliouawa katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya kutoa heshima kwa mashahidi hao ambako pia alitoa hotuba katika umati mkubwa wa wananchi. Kwa mara nyingine Imam aliitaja serikali ya Shapour Bakhtiar kuwa kibaraka wa Shah sanjari na kutangaza nia yake ya kuunda serikali mpya kwa msaada wa wananchi. Siku kumi baada ya kurejea nchini Imam, Ruhullah Khomeini Mapinduzi ya Kiislamu yalipata ushindi kamili na kipindi hicho cha siku kumi za baina ya kurejea Imam nchini hadi kupata ushindi kamili Mapinduzi ya Kiislamu, kinajulikana hapa nchini kama "Alfajiri Kumi".

Imam Khomeini akirejea nchini kutoka uhamishoni Ufaransa

Siku kama ya leo miaka 167 iliyopita, ilianzishwa harakati kubwa ya wananchi wa China iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Taiping. Harakati hiyo ilitokana na hali mbaya na umasikini uliokuwa ukiwasumbua wananchi wa nchi hiyo na hasa matabaka ya watu wa vijijini, iliyosababishwa na ukoloni wa kigeni na utawala wa familia isiyofaa ya Manchu. Lengo kuu la harakati hiyo iliyodumu kwa muda wa miaka 14 lilikuwa ni kuwepo usawa katika kugawana ardhi kati ya wanawake na wanaume.

uasi wa Wataiping

Siku kama ya leo miaka 418 iliyopita, ilianzishwa kampuni ya kwanza ya Uingereza ya India Mashariki nchini India, kwa amri ya Malkia Elizabeth wa Kwanza wa Uingereza. Kampuni hiyo, iliimarisha ukoloni wa Uingereza katika maeneo yenye utajiri, huko kusini mwa Asia na baada ya hapo shughuli za ukoloni zikaimarika zaidi katika mataifa ya kusini mwa Asia kupitia kampuni hiyo. Baada ya kuasisiwa kampuni hiyo, nchi nyingine kama vile Uholanzi, Ureno na Ufaransa zilielekeza nguvu zao katika bara Hindi kwa lengo la kuhudumia ukoloni wao. Aidha baada ya karne 3 za kuanzishwa shirika hilo, ushawishi na kuimarika utawala wa Uingereza nchini India vilisababisha nchi hiyo kutangazwa kuwa sehemu ya Uingereza na Malkia Viktoria kuvikwa taji la kuwa mtawala wa India na Uingereza.

 Kampuni ya kwanza ya Uingereza ya India Mashariki nchini India

Na miaka 1047 iliyopita siku kama hii ya leo, alifariki dunia malenga wa Kiirani Abu Is'haq Kesa-i Marvazi. Alizaliwa mwaka 341 Hijria katika mji wa Marv, moja kati ya miji ya Iran ya zamani, ambao kwa sasa unapatikana katika ardhi za Turkmenestan. Malenga huyu aliishi katika zama za mwisho za utawala wa Kisaman na mwanzoni mwa zama za utawala wa Maghaznavi. Marvazi alitunga beti kadhaa za mashairi kukisifu kizazi cha Mtukufu Mtume Muhammad (saw) hasahasa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Malenga huyu mkubwa wa Kiirani ameacha diwani kadhaa za mashairi.

Malenga Abu Is'haq Kesa-i Marvazi