Alkhamisi, tarehe Pili Februari, 2017
Leo ni Alkhamisi tarehe 4 Jamadil Awwal 1438 Hijria sawa na tarehe Pili Februari 2017.
Siku kama ya leo miaka 883 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alizaliwa nchini Iraq Ibn Athir Jazari mwanahistoria na mwanafasihi mahiri wa Kiislamu. Ibn Athir alisoma mjini Mosul, Sham na Baghdad kwa maulama watajika kama Khatib Tusi. Alikuwa na mapenzi makubwa na kutwalii na kufanya uhakiki kuhusiana na historia na ni kutokana na sababu hiyo athari zake nyingi zilizoko hii leo zinahusiana na historia. Kitabu mashuhuri zaidi cha Ibn Athir ni kile kinachojulikana kwa jina la "al-Kamil Fi Taarikh." Msomi na mwanahistoria huyo wa Kiislamu alifariki dunia mwaka 630 Hijria katika mji wa Mosul huko Iraq.

Miaka 225 iliyopita katika siku kama ya leo, mkataba wa kihistoria wa Berlin, ulitiwa saini baina ya Leopold II mfalme wa wakati huo wa Austria na Frederick William aliyekuwa mfalme wa Prussia. Mkataba huo ulikuwa natija ya maafikiano baina ya viongozi hao wawili yaliyofikiwa tarehe Pili Agosti mwaka 1791 huko Pillnitz kwa ajili ya kukabiliana na mapinduzi ya Ufaransa. Hii ilitokana na kuwa, watawala wa Ulaya walikuwa wameingiwa na woga mkubwa kutokana na baadhi ya nadharia za wapigania uhuru wa Ufaransa. Licha ya kuweko mkataba huo na hata mashambulio ya pamoja ya Austria, Prussia na Uingereza dhidi ya Ufaransa na himaya yao kwa wapigania mfumo wa utawala wa Kifalme wa nchi hiyo, harakati hizo hazikuwa na natija kwani hatimaye wanamapinduzi wa Ufaransa waliibuka na ushindi.

Katika siku kama ya leo miaka 110 iliyopita, Dmitri Ivanovich Mendeleev msomi na mwanakemia wa Kirusi alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 73 huko Saint Petersburg uliokuwa mji mkuu wa Russia wakati huo. Dmitri alizaliwa mwaka 1834 na kusoma taaluma ya kemia. Msomi huyo alifanya utafiti na uhakiki mwingi muhimu katika taaluma ya kemia ambapo baadaye ulikuja kujulikana kwa jina la jedwali la Mendeleev.
Na miaka 38 iliyopita katika siku kama leo, wananchi wa Iran walipokuwa katika sherehe na shamrashamra za kurejea nchini Imam Khomeini akitokea uhamishoni nje ya nchi, Imam alizungumza na waandishi habari akieleza misimamo ya mfumo ujao wa utawala wa Kiislamu hapa nchini na kutangaza kuwa ataaunda serikali ya mpito ya mapinduzi muda mfupi baadaye. Imam Khomeini alitangaza kuwa serikali hiyo ya mpito itakuwa na jukumu la kutayarisha kura ya maoni ya Katiba mpya ya Iran. Vilevile alimtahadharisha Waziri Mkuu wa serikali ya wakati huo ya Shah kwamba, iwapo ataendelea kuwakandamiza wananchi angetangaza vita vya jihadi. Imam Khomeini vilevile alilitaka jeshi lijiunge na mapambano ya wananchi dhidi ya utawala wa Shah. Wakati huo pia ilitangazwa kwamba Wamarekani elfu 35 walikuwa wamekwishaondoka katika ardhi ya Iran na kwamba wengine elfu 10 wako mbioni kuondoka.