Feb 04, 2017 00:30 UTC
  • Jumamosi, Februari 4, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 6 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1438 Hijria sawa na tarehe 4 Februari 2017 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 1024 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alifariki dunia Abu Saeed Muhammad bin Abdul-Jalil Sistani, mwanahisabati mashuhuri wa Kiislamu. Alibobea na kutabahari katika elimu za hisabati, jiometri na nujumu. Abu Saeed Muhammad bin Abdul-Jalil Sistani alikuwa akiandika kitabu katika kile elimu aliyokuwa akiisoma na hivyo kuwafikishia wengime elimu na maarifa yake. ***

Abu Saeed Muhammad bin Abdul-Jalil Sistani

Miaka 490 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Ghiyathudeen Mansur mwanahisabati mashuhuri wa Kiirani. Ghiyathudeen Mansur alitumia sehemu kubwa ya umri wake kufundisha na kualifu vitabu. Mwanzuoni huyo amezikwa huko Shiraz moja ya miji ya Iran. Ghiyathudeen alisoma elimu za kiakili na nakili kwa baba yake na kisha kwa maulamaa wengine. Alimu huyo hakuwa nyuma pia katika uwanja wa uandishi wa vitabu. Hujjatul Kalaam na al-Haqaiq ni miongoni mwa vitabu mashuhuri wa Ghiyathudeen Mansur. ***

Ghiyathudeen Mansur

Siku kama ya leo miaka 329 iliyopita, Pierre Marivaux mwandishi wa riwaya na michezo ya kuigiza wa Kifaransa alizaliwa huko Paris nchini Ufaransa. Pierre alianza kujishughulisha na kazi ya sanaa tangu akiwa kijana na kwa muda fulani alishiriki pia katika michezo ya kuigiza hadi pale alipoanza kuandika michezo hiyo. Marivaux alipata umashuhuri mkubwa kutokana na ukosoaji wake katika uandishi wa riwaya. Marivaux ameacha athari nyingi za kimaandishi zikiwemo riwaya na michezo ya kuigiza. ***

Pierre Marivaux

Katika siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, kulifanyika mkutano uliojulikana kwa jina la Yalta katika peninsula ya Crimea huko kusini mwa Urusi ya zamani kwa kuzishirikisha Uingereza, Marekani na Shirikisho la Urusi ya Zamani. Mkutano huo ulifanyika baada ya kudhihiri dalili za kushindwa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia. Lengo hasa la mkutano wa Yalta lilikuwa kujadili hali ya kisiasa na kijeshi ya nchi zilizokuwa zikipigana vita hivyo, ikiwa ni pamoja na kuainisha hatima ya ardhi zilizokuwa chini ya madola waitifaki. ***

Viongozi walioshiriki mkutano wa Yalta

Miaka 69 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Sri Lanka ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza. Nchi hiyo ambayo ni kisiwa kilichoko kusini mashariki mwa India, ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu wakoloni wa Kireno katikati mwa karne ya 16 na baadaye wakoloni wa Kiholanzi, na kuanzia mwaka 1798 ikaunganishwa rasmi na makoloni ya Uingereza. Mapambano ya kupigania uhuru wa Sri Lanka yalianza mwanzoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia. Mwaka 1931 Uingereza ililazimika kutoa haki ya kutoa maoni kwa wananchi wa Sri Lanka na kuasisi baraza la kutunga sheria na baraza la utekelezaji. Hata hivyo nchi hiyo ilikuwa bado haijapata uhuru kamili katika masuala ya kigeni. Kwa msingi huo mapambano ya wananchi yaliendelezwa hadi kisiwa hicho kilipopata uhuru kamili mwaka 1948 katika siku kama ya leo. *** 

Bendera ya Sri Lanka

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, Imamu Ruhullah Khomeini alitoa amri ya kuundwa serikali ya muda ya Mapinduzi ya Kiislamu; hatua ambayo ilichukuliwa muda mfupi kabla ya ushindi Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Katika amri yake hiyo, mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza malengo na mipango ya Mapinduzi ya Kiislamu na akaitaka serikali ya muda ifanye hima kwa ajili ya kufikiwa malengo hayo. Aidha katika amri hiyo, aliainisha jukumu kuu la serikali ya muda ambalo lilikuwa kuitisha kura ya maoni kwa ajili ya kuainisha mfumo wa kisiasa utakaotawala hapa nchini, kuandaa uchaguzi na kuunda Baraza la Waasisi kwa ajili ya kutunga Katiba na kufanyika uchaguzi wa kwanza wa Bunge.***

Kuundwa serikali ya muda Mapinduzi ya Kiislamu

Na siku kama ya leo mwaka mmoja uliopita, aliaga dunia Raghib Mustafa Ghalwash qarii na msomaji Qur'ani mahiri wa Kimisri. Ghalwash alizaliwa Julai 5 mwaka 1938 huko nchini Misri na kukulia katika familia iliyokuwa na mapenzi makubwa na Qur'ani. Raghib Mustafa Ghalwash alipofikia rika la ubalobaro tayari alikuwa amehifadhi Qur'ani yote na alipokuwa na umri wa miaka 16 alianza kusoma Qur'ani katika hafla mbalimbali. Sheikh Raghib Mustafa Ghalwash alikuwa miongoni mwa wasomaji wa Qur'ani waliofanya safari nchini Iran baada ya vita vya kulazimishwa vilivyoanzisha na Iraq dhidi ya Iran. Hatimaye baada ya kuugua aliaga dunia katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 77. ***

Raghib Mustafa Ghalwash