Jumapili, Februari 5, 2017
Leo ni Jumapili tarehe 7 Mfunguo Nane Jamadul Awwal 1438 Hijria, sawa na tarehe 5 Februari 2017 Miladia.
Siku kama hii ya leo miaka 38 iliyopita mamilioni ya wananchi Waislamu na wanamapinduzi wa Iran waliandamana katika miji mbalimbali hapa nchini kufuatia kutangazwa kuundwa serikali ya muda ya Mapinduzi ya Iran. Wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano ili kuunga mkono na kuidhinisha uamuzi huo uliotolewa na Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu. Katika siku kama hii miaka 33 iliyopita, wananchi Waislamu wa Iran walimiminika kwenye mitaa mbalimbali na kwa sauti moja kutaka kuondoka madarakani serikali ya Bakhtiyar ambayo ilikuwa kibaraka wa madola ya kibeberu. Aidha siku hiyo Jenerali Heizer mjumbe maalumu wa Marekani alikuwa amewasili Tehran ili kusaidia kuubakisha madarakani utawala wa Pahlavi na wakati huohuo kutangaza uungaji mkono wa Marekani kwa makamanda wa jeshi la Shah na hivyo kuandaa uwanja wa kuyapindua Mapinduzi ya Kiislamu.
Siku kama ya leo miaka 1049 iliyopita, alifariki dunia Ghalabun al-Halabi, msomi wa Qur'ani na mtaalamu mashuhuri wa elimu ya hadithi wa enzi hizo. Ibn Ghabun alizaliwa mjini Aleppo, Syria mnamo mwaka 309 Hijiria na kukulia nchini Misri. Alipata kusoma elimu ya hadithi na kisomo cha Qur'ani Tukufu kutoka kwa wasomi wengi wa zamani zake na kutokea kuwa mwalimu katika uwanja huo. Aidha aliweza kutoa maoni yake kuhusiana na visomo vya Qur'ani kupitia kitabu chake cha 'Al-Kashf.' Moja ya athari zake mashuhuri ni pamoja na kitabu cha 'Al-Irshad' ambacho kinazungumzia visomo saba vya Qur'ani.
Siku kama ya leo miaka 136 iliyopita alifariki dunia mwanahistoria, mwanafalsafa na mtaalamu mashuhuri wa masuala ya mashariki wa Scotland Thomas Carlyle. Mwanafalsafa huyo alizaliwa mwaka 1795 na mbali na lugha ya Kijerumani, alijifunza pia lugha ya Kiarabu. Katika safari zake nyingi katika nchi za Kiislamu, mwanahistoria huyo alijifunza utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu na kuathirika mno na dini hiyo. Thomas Carlyle anasema kuhusu Qur'ani kwamba: "Qur'ani ni sauti isiyokuwa na wasita kutoka kwenye roho ya ulimwengu, na wanadamu wanapaswa kuisikiliza, na wala hawapaswi kusikiliza maneno mengineyo."
Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, aliuawa kwa kunyongwa mjini Cairo, Misri Sayyid Qutb, msomi na mwanamapambano mashuhuri wa nchini Misri akiwa pamoja na wanafunzi wake wawili. Akiwa na umri wa miaka kumi, Qutb aliweza kuhifadhi Qur'ani yote na kuanza kujihusisha na masuala ya kisiasa na mapambano dhidi ya ukoloni na udikteta wa zama hizo. Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha mjini Cairo na kusoma kwa miaka 16, huku akifanya safari nchini Marekani mnamo mwaka 1948 kwa ajili ya kuendelea na masomo yake. Matukio ya ukandamizaji na ukatili aliyoyashuhudia nchini Marekani, yalimfanya awachukie sana Wamagharibi. Katika harakati za mapambano yake ya kisiasa, Sayyid Qutb alifahamiana na Hassan al-Banna, mwasisi wa Harakati ya Kiislamu ya Ikhwanul Muslimin na hatimaye naye akajiunga na harakati hiyo ambapo alitokea kuwa na nafasi kubwa. Hata hivyo kutokea tofauti baina yake na Gamal Abdel Nasser, rais wa wakati huo wa Misri, kulimpelekea atiwe mbaroni na hatimaye kunyongwa katika siku kama ya leo.
Na siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, liliasisiwa Baraza la Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu, kama taasisi kuu ya ushauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, chini ya Imamu Khomein, Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini hapa. Jukumu kuu la taasisi hiyo ni kutatua tofauti ambazo wakati mwingine zinaweza kuibuka baina ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (yaani bunge) na Baraza la Kulinda Katiba. Wajumbe wa Baraza la Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu huteuliwa na Kiongozi Muadhamu kila baada ya miaka mitano.