Feb 06, 2017 01:51 UTC
  •  Jumatatu, 6 Februari, 2017

Leo ni Jumatatu 8 Jamadi Awwal 1438 Hijria sawa na 6 Februari 2017

Miaka 81 iliyopita mwafaka na tarehe 6 mwezi Februari mwaka 1936 eneo lenye baridi zaidi duniani lilitambuliwa na jopo moja la kielimu baada ya kufanya juhudi za miaka minne na hatimaye kugundua eneo hilo. Kundi hilo la wataalamu hatimaye liligundua kuwa, mji wa Verkhoyansk huko Siberia, kaskazini mwa Russia, ndiyo eneo lenye baridi zaidi duniani baada ya kufanya utafiti wa muda mrefu. Mji wa Verkhoyansk ulikuwa ukitumika kama makazi ya uhamishoni ya wahalifu wa kisiasa wa Russia kabla ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti. Mji huo una jamii ndogo ya watu ambao kazi yao kuu ni biashara ya ngozi na kuchimba madini. Kiwango cha joto la eneo hilo majira ya baridi hufikia daraja 70 chini ya sifuri.

Siku kama ya leo miaka 95 iliyopita mkutano wa kimataifa wa kuzuia matumizi ya silaha za sumu ulimaliza kazi zake mjini Washington, Marekani kwa kutiwa saini mkataba uliopewa jina la mkataba wa pande tano kati ya nchi zilizoshiriki mkutano huo. Nchi zilizotia saini mkataba huo ni Marekani, Ufaransa, Uingereza, Italia na Japan. Mkataba huo ulipiga marufuku utumiaji wa aina yoyote ya gesi za sumu na za kemikali katika vita. Miaka kadhaa baadaye nchi nyingine zilijiunga na mkataba huo wa kuzuia utumiaji wa gesi za sumu vitani.

Siku kama ya leo miaka 115 iliyopita aliaga dunia Sheikh Muhammad Abduh ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa Kiislamu katika mji wa Alexandria nchini Misri. Alipata elimu katika Chuo Kikuu cha al Azhar na kisha akahudhuria darsa za Jamaluddin Asadabadi, mwanazuoni aliyepigania uhuru wa nchi za Kiislamu. Baada ya kupelekwa uhamishoni Sayyid Jamaluddin, Sheikh Muhammad Abduh alichukua nafasi yake ya kufundisha na kutoa elimu kwa wanazuoni na wanafikra za Kiislamu. Hata hivyo Sheikh Abduh alibaidishiwa nchini Syria baada ya satuwa ya wakoloni wa Kiingereza kuenea nchini Misri. Baada ya kufunza kwa kipindi cha miaka sita nchini Syria alihamia Paris na kusaidiana na Sayyid Jamaluddin Asadabadi katika kuchapisha gazeti la al Uruwatul Wuthqaa.

Sheikh Muhammad Abduh

Miaka 125 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia mwanazuoni wa Kiislamu, Muhammad Baqir Zainul Abidin Khansari katika mji wa Isfahan nchini Iran. Alikuwa hodri katika elimu za fiqhi na hadithi na alipewa ijaza ya kunukuu hadithi na wanazuoni wakubwa katika taaluma hiyo. Baada ya muda msomi huyo mkubwa ambaye alikuwa gwiji wa hali na shajara za maulamaa na wataalamu wa fiqhi ya Kiislamu, alishika hatamu za kuongoza chuo kikuu cha kidini cha Isfahan. Mirza Muhammad Baqir Khansari ameandika vitabu vingi na miongoni mwa vitabu vyake ni Raudhaatul Jannat na Hashiyatu Sharhil Lum'ah.

Mahala alipozikwa Sayyid Muhammad Baqir Khansari

Na siku kama ya leo miaka 400 iliyopita alifariki dunia daktari na mtaalamu wa mimea wa Italia, Prospero Alpini. Alizaliwa mwaka 1553 na baada ya kuhitimu masomo ya tiba alitunukiwa shahada ya udaktari. Katika uchunguzi na utafiti wake, Prospero Alpini aligundua kwamba, mimea kama walivyo wanyama, ina jinsia mbili za kike na kiume japokuwa hakuweza kujua kama kanuni hiyo inahusu kila kitu.

Miongoni mwa hatua nyingine muhimu za Prospero Alpini ni kuarifisha kahawa na ndizi kwa watu wa Ulaya. Biashara ya kahawa ya Mocha au al Mukha ambalo ni jina la bandari iliyoko kusini mwa Yemen, ilikuwa mikononi mwa Waislamu tangu karne ya 15, na mtaalamu huyo wa mimea wa Italia ndiye aliwajulisha watu wa Ulaya aina hiyo ya kahawa (Arabica) iliyokuwa ikioteshwa katika maeneo ya milimani nchini Yemen. 

Prospero Alpini