Feb 07, 2017 10:54 UTC
  • Umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu (1)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi, la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Endeleeni kuwa nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya kwanza.

Kama mjuavyo, umoja na mshikamano ni jambo lililotiliwa mkazo sana katika mafundisho ya Kiislamu. Lakini tunapoangalia matukio yanayojiri leo hii katika Ulimwengu wa Kiislamu tunashuhudia mizozo na mifarakano mikubwa na iliyo nadra kuwahi kushuhudiwa baina ya nchi za Kiislamu. Kwa sababu hiyo, katika mazingira tuliyonayo, kurejea kwenye mafundisho ya Uislamu na sira ya Bwana Mtume Muhammad (SAW) kuna udharura mkubwa zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote ule, kwa sababu maadui wa Umma wa Kiislamu wanaitumia fursa ya hali ya migawanyiko na mifarakano iliyopo katika Ulimwengu wa Kiislamu kwa maslahi yao na kutosita kuchukua kila hatua kwa lengo la kuudhoofisha Ulimwengu wa Kiislamu. Kwa sababu hiyo tumeamua kuandaa kipindi hiki cha "Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu" ili kulizungumzia suala hilo na kuona umoja baina ya Waislamu una nafasi gani kwenye tanuri la fikra la Uislamu na la warekebishaji umma na wanafikra wa Kiislamu; na nini inapasa kifanyike ili kulifikia lengo hilo tukufu?

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, hivi sasa kuna Waislamu wapatao bilioni moja na milioni mia mbili wanaoishi katika maeneo tofauti ya dunia na ambao kiidadi ni wengi zaidi katika nchi zipatazo 57. Aidha katika nchi nyingine nyingi, Waislamu ni jamii ya kidini yenye wafuasi wachache lakini wenye ushawishi.

Mbali na nchi za Kiislamu kuwa na karibu theuluthi moja ya viti kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, zina utajiri mkubwa pia wa maliasili za nishati za mafuta na gesi. Nchi hizo pia ziko kwenye maeneo mengi nyeti, hasasi na ya kistratijia duniani, jambo ambalo linazifanya ziwe na uwezo wa kuwa na hali ya kipekee kiuchumi, kisiasa na hata kijeshi. Lakini licha ya nchi za Kiislamu kuwa na fursa na uwezo mkubwa wa kiuchumi, kisiasa na kijeshi, ambao kama utatumiwa na kusimamiwa kwa njia sahihi utaweza kuzifanya ziwe moja ya mihimili mikuu yenye nguvu na sauti duniani, kwa masikitiko ni kwamba kukosekana umoja na mshikamano baina ya nchi hizo kumezifanya zisiwe na hadhi na nafasi inayostahiki katika mfumo wa kimataifa; na hata ndani ya pande nne za mipaka yao pia, nchi za Kiislamu zinakabiliwa na matatizo kadha wa kadha hususan mizozo na migogoro ya ndani na hali duni za kiuchumi.

Shikamaneni na kamba ya Allah nyote wala msifarikiane

 

Suala la mfarakano baina ya Waislamu ambalo linatajwa kama sababu kuu ya kubaki nyuma kimaendeleo nchi za Kiislamu, siku zote limekuwa moja ya mambo yanayozishughulisha mno bongo za wanafikra, warekebishaji umma pamoja na wanasiasa wa Ulimwengu wa Kiislamu. Warekebishaji umma wengi wa Ulimwengu wa Kiislamu wanaamini kuwa kujiweka mbali Waislamu na tunu na thamani za asili za Kiislamu na badala yake kufufua taasubi na ukereketwa wa kikaumu, kikabila na wa asili za watu wa zama za ujahilia, ndio sababu kuu ya mfarakano na utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu. Na katika kukabiliana na hilo wamependekeza na kushauri njia mbalimbali za kuziunganisha nchi za Kiislamu na kuzifanya ziwe na umoja. Hata hivyo licha ya jitihada na uelimishaji mkubwa uliofanywa na warekebishaji umma hususan wanafikra mashuhuri kama Sayyid Jamaluddin Asad Abadi, Iqbal Lahore na Imam Khomeini (MA), kuhusu umuhimu wa kuamka Ulimwengu wa Kiislamu na kuwepo umoja kati ya nchi za Kiislamu unaotokana na misingi na itikadi zao imara na za pamoja za kidini ikiwemo imani juu ya tauhidi na upweke wa Mwenyezi Mungu, Utume wa Nabii Muhammad SAW, kuafikiana wao wote kwamba Qur'ani tukufu ni kitabu kilichotakasika na upotoshwaji wowote na pia kukielekea kwao kibla kimoja; lakini inasikitisha kuona kwamba hadi sasa Ulimwengu wa Kiislamu haujaweza kupiga hatua za maana katika njia ya umoja na kuwa mshikamano na msimamo wa pamoja. Ni kutokana na hali hiyo, ndiyo maana Waislamu walio wengi wanateseka na kutaabika kwa ukata, ufakiri na hali duni ya kiuchumi, kuwa na hadhi ya chini kisiasa katika uga wa kimataifa na kuandamwa na matatizo ya ndani yanayotokana na uingiliaji wa mara kwa mara wa kisiasa na kijeshi wa madola majabari katika nchi hizo.

Hata Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, ambayo awali ikijulikana kama Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC), ambayo lengo lake kuu lilikuwa ni kuzidisha mshikamano baina ya nchi za Kiislamu, kuunga mkono ushirikiano kati ya nchi wanachama katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, kuandaa mazingira ya kuwepo maelewano zaidi kati ya nchi hizo na kuunga mkono mapambano ya mataifa yote ya Kiislamu kwa ajili ya kulinda heshima, uhuru wa kujitawala na haki za kitaifa za nchi hizo, kwa kipindi chote hiki tangu kuasisiwa kwake haijaweza kufanikisha kupatikana umoja baina ya nchi za Kiislamu; na anga ya mifarakano na mizozano ambayo imekuwa ikitawala katika misimamo ya nchi hizo ingalipo palepale. La kusikitisha zaidi ni kwamba, katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, kujitokeza makundi ya kisalafi na kitakfiri kumeshadidisha mizozo na vita baina ya Waislamu na kuzidi kuchafua sura ya dini yao mbele ya fikra za walimwengu. Kutokana na yote hayo, wakati umewadia wa sisi wenyewe kujiuliza, kuna kweli Waislamu wanaonufaika na kufaidika na hali hii ya mizozano na mifarakano baina ya nchi za Kiislamu? Kwa nini viongozi wa mataifa ya Waislamu hawazinduki na kulifanya suala la umoja kuwa ndio dira ya sera zao katika kukabiliana na maadui waliokula kiapo cha kuudhuru Uislamu na Waislamu? Qur'ani tukufu na mafundisho ya Bwana Mtume Muhammad SAW yamelipa thamani na hadhi gani suala la umoja wa Umma wa Kiislamu? Ni vizuizi gani vinakwamisha kufikiwa umoja, maelewano na mshikamano baina ya nchi za Kiislamu?

 

Kabla ya kueleza umoja baina ya Waislamu umepewa nafasi gani katika aya za Qur'ani tukufu ni vyema kwanza tukalitolea jibu suali hili, kwamba tunapozungumzia umoja baina ya Waislamu tunakusudia umoja wa jambo gani na wa aina ipi?  Kuna rai mbili zilizotolewa katika kujibu suali hili. Rai ya kwanza ni ya mtazamo wenye muelekeo ambao, tunaweza kuuita wa 'kiumakanika' juu ya umoja wa jamii ya Kiislamu, unaoitakidi kwamba ili kuwa na umoja, Waislamu wote, Mashia, Masuni na wengineo waache imani na itikadi zao za kimadhehebu na badala yake waamini na kuyatekeleza yale tu yanayoziunganisha pamoja madhehebu zote za Uislamu. Kwa mujibu wa mtazamo huu, Waislamu wote inapasa wafuate madhehebu moja ya pamoja, kwa namna ambayo hakutokuwapo na hitilafu wala tofauti yoyote katika itikadi na hukumu za kifiqhi katika jamii ya Kiislamu. Rai ya pili ina mtazamo mwingine kuhusu umoja na kuwaunganisha Waislamu. Rai hii ina muelekeo tuwezao kuuita wa kioganiki na wenye kuzingatia maumbile na hali halisi. Kwa mujibu wa mtazamo wa rai hii, madhumuni na makusudio ya umoja baina ya Waislamu ni kwamba sambamba na wafuasi wa kila madhehebu kushikamana na itikadi na hukumu maalumu za madhehebu yao, katika uhusiano wa kijamii, kisiasa, kijeshi, kiuchumi na kiutamaduni wawe kitu kimoja na Waislamu wenzao na wazingatie maslahi makuu ya Uislamu na umma wa Kiislamu na wote kwa pamoja daima wawe mithili ya "mkono mmoja" na nguvu moja katika kukabiliana na maadui wa Uislamu.

Mpenzi msikilizaji, sehemu ya kwanza ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Hivyo tusite hapa kwa leo hadi juma lijalo panapo majaaliwa ya Mola katika siku na saa kama ya leo ili kuendelea na sehemu ya pili ya mfululizo huu.

 

Tags