Jumanne 7 Febuari, 2017
Leo ni Jumanne tarehe 9 Jamadil Awwal 1438 Hijria sawa na Februari 7, 2017
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, wananchi na jeshi la Iran, walionyesha utiifu wao kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Khomein (MA). Siku hiyo mamilioni ya wananchi walipiga nara zilizoonyesha utiifu na uungaji mkono wao kwa Imamu na serikali ya Mapinduzi, kupitia maandamano makubwa yaliyofanyika katika miji tofauti ya Iran huku wakisisitiza juu ya kuendelea na mapambano hadi kuung’oa kikamilifu utawala wa Shah. Kwa upande mwingingine, maafisa na askari wa jeshi la anga wakiwa wamevalia sare za kijeshi walifika mbele ya Imam Khomein (MA) na kutangaza uungaji mkono wao kwa mapinduzi ya Kiislamu. Akiwahutubia shakhsia hao, Imam alisema: “Hadi sasa mlikuwa mkimtii twaghuti, lakini kuanzia leo mmefungamana na Qur’ani. Qur’ani itawalindeni, na ninataraji kwa msaada wenu tutaweza kuweka nchini Iran utawala wa kiuadilifu wa Kiislamu.” Mwisho wa kunukuu.

Tarehe 7 Februari mwaka 1961 kiongozi wa chama cha Abako, Joseph Kasavubu aliteuliwa kuwa Rais wa konfederesheni iliyokuwa ikiungwa mkono na Umoja wa Mataifa ya Congo. Baada ya Congo kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mbelgiji, Kasavubu alichaguliwa kuwa mkuu wa Baraza la Taifa lililoanza kazi Juni 30 mwaka 1960. Nchi huru ya Congo ilikumbwa na misukosuko mingi ya kisiasa baada tu ya kupata uhuru na serikali kuu ilidumazwa na mivutano iliyotokea kati ya viongozi wake.
Siku kama ya leo miaka 18 iliyopita aliaga dunia Hussein bin Talal mfalme wa zamani wa Jordan kwa ugonjwa wa saratani. Alizaliwa mwaka 1935 huko Amman mji mkuu wa Jordan na kuhitimu masomo yake katika Chuo Kikuu cha Kijeshi cha Uingereza. Mfalme Hussein alikalia kiti cha usultani huko Jordan mwaka 1952 akiwa na miaka 17 kufuatia kuuawa babu yake mfalme Abdallah na baada ya baba yake Amir Talal kukalia kiti cha uongozi kwa miezi kadhaa tu. Mapinduzi na mauaji mengi yalitokea wakati wa zama za usultani wa mfalme Hussein bin Talal huko Jordan.
Miaka 43 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi dogo ya Grenada iliyoko katika Amerika ya Kaskazini ilijipatia uhuru. Kisiwa hicho kiligunduliwa mwaka 1498 na Christopher Columbus mvumbuzi wa Kihispania na ikaunganishwa na nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1674 Ufaransa ikaidhibiti Grenada. Baada ya takribani karne moja yaani mwaka 1783, Waingereza waliifanya Grenada kuwa koloni lao na hali hiyo ikadumu kwa takribani karne mbili. Hatimaye mwaka 1974 na katika siku kama ya leo, Grenada ikajikomboa na kujipatia uhuru.
Siku kama ya leo miaka 155 iliyopita, alizaliwa mjini Newcastle, Edward Granville Browne, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati, mtafiti na mwanafasihi wa Uingereza. Awali Browne alihitimu taaluma ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Cambridge. Hata hivyo kutokana na kupendelea kwake tamaduni za mashariki mwa dunia alifanya safiri nchini Iran akiwa na umri wa miaka 25. Mtafiti huyo aliitaja lugha ya Kifarsi kuwa chombo bora ya kunakili fikra na tamaduni za Wairan kuelekea maeneo mengine ya dunia. Ni kwa msingi huo ndio maana akaandika vitabu kadhaa kuhusiana na historia na utamaduni wa Wairani. Mwishoni Edward Granville Browne alijikita katika kufundisha lugha ya Kifarsi na Kiarabu katika Chuo Kikuu cha Cambridge na alifariki dunia mwaka 1926 akiwa na umri wa miaka 54.
Siku kama ya leo miaka 539 iliyopita, alizaliwa Thomas More, mwanafalsafa na msomi mashuhuri wa nchini Uingereza. Mwanzoni More alisomea sheria na baada ya kujiunga na Bunge alipewa mazingatio na malkia wa wakati huo na kutunukiwa hadhi ya Ulodi. Hata hivyo Thomas More alitofautiana kinadharia na mfalme wa wakati huo wa Uingereza na hivyo akatiwa jela na kuhukumiwa kifo. Hatimaye More alinyongwa mnamo tarehe sita Julai mwaka 1535 akiwa na umri wa miaka 57.
Tarehe 9 Jamadil Awwal mwaka 786 Hijria, aliuawa shahidi faqihi na mtaalamu mkubwa wa hadithi Muhammad bin Jamaluddin Makki Amili, mashuhuri kwa jina la "Shahidi wa Kwanza." Alizaliwa mwaka 734 Hijria katika mojawapo ya vijiji vya Jabal Amil nchini Lebanon. Alijifunza elimu mbalimbali kutoka kwa walimu wakubwa wa zama zake kama vile Allama Hilli. Mbali na elimu ya dini, Muhammad bin Jamaluddin pia alikuwa hodari katika taaluma za mashairi na fasihi. Katika miaka 52 ya umri wake uliojaa baraka, Shahidi wa Kwanza aliandika vitabu vingi, ikiwa ni pamoja na "Albaqiyatus-Swalihat" na "al Lumuatu Dimashqiyya." Aliuawa na wapinzani wenye taasubi katika siku kama ya leo.