Jumatano, Februari 15, 2017
Leo ni Jumatano 17 Rabiul Awwal 1438 Hijria sawa na Februari 15, 2017.
Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, Jeshi Jekundu la Shirikisho la Urusi ya Zamani lililazimika kuondoka nchini Afghanistan baada ya kuikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa miaka kumi. Majeshi hayo yaliondoka baada ya kushindwa kukabiliana na muqawama wa mujahidina wa Kiislamu. Lengo la Umoja wa Sovieti la kuivamia na kuikalia kwa mabavu Afghanistan mwaka 1979, lilikuwa ni kuizatiti na kuitia nguvu serikali kibaraka ya Kabul iliyokuwa ikiungwa mkono na Moscow na kueneza satua yake upande wa maeneo ya kusini mwa Asia. Hatua hiyo iliyoyatumbukiza hatarini maslahi ya Marekani, ilikabiliwa na radiamali kali ya Washington ambapo Ikulu ya Marekani (White House) ilianzisha operesheni za kuyatoa majeshi ya Umoja wa Sovieti huko Afghanistan. Hatimaye baada ya miaka 10 wananchi wa Afghanistan wakisaidiwa na Mujahidina walifanikiwa kuhitimisha uvamizi huo na kuyatoa majeshi ya Urusi katika ardhi yao.

Miaka 235 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Miladia, vilianza vita vya majini kati ya Ufaransa na Uingereza katika pwani ya India. Vita hivyo vilivyodumu kwa muda wa miezi saba, vilikuwa ni mlolongo wa vita kati ya nchi mbili hizo vilivyokuwa na lengo la kuikoloni India na kupora utajiri wake. Ijapokuwa Ufaransa ilishinda vita hivyo, lakini nchi hiyo haikuweza kurejea India na kuikoloni nchi hiyo, na badala yake Uingereza ilibaki na kuendelea kuwa mkoloni mkuu huko Bara Hindi.

Siku kama ya leo miaka 453 iliyopita alizaliwa msomi mashuhuri, mnajimu na mtaalamu wa fizikia wa Italia, Galileo Galilei katika mji wa Pisa. Alisoma fasihi hadi alipokuwa na umri wa miaka 19 na baadaye akajishughulisha na fizikia na hisabati. Galileo alitumia lenzi iliyovumbuliwa na msomi na mnajimu mashuhuri wa Kiislamu Ibn Haitham kutengeneza darubini ya elimu ya nujumu kwa ajili ya kutazamia nyota na sayari. Galileo alitumia chombo hicho kuthibitisha kwamba sayari ikiwemo ya ardhi, zinazunguka jua. Utafiti huo wa Galileo Galilei ulithibitisha nadharia ya msomi Muislamu wa Iran ambaye karne kadhaa kabla yake alithibitisha kwamba ardhi inazunguka jua. Baada ya kusambaa nadharia hiyo ya Galileo kuhusu mzunguko wa ardhi na sayari nyingine kando ya jua, kanisa la Roma lilimtuhumu kuwa kafiri na kupelekea kuhukumiwa kifungo cha maisha cha nyumbani. Baadaye msomi huyo alilazimika kukanusha nadharia hiyo kwa ajili ya kuokoa maisha yake.
Siku kama ya leo miaka 988 iliyopita, alizaliwa Muhammad Ghazali msomi wa fiq'hi na mwanafalsafa mashuhuri wa Kiislamu wa Iran. Ghazali alisoma elimu ya fiq'hi kwa Abu Nasri Ismail na alikuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu katika elimu hiyo akiwa na umri wa miaka 28. Umaarufu wa Imam Muhammad Ghazali ulipelekea kiongozi wa Iraq wakati huo Khawaja Nidham al-Mulk kumualika msomi huyo kwenda mjini Baghdad kwa ajili ya kufundisha. Hatimaye alirejea Iran na kujishughulisha na masuala ya ualimu. Imam Muhammad Ghazali aliandika kitabu chake maarufu cha "Ihyau Ulumud-Din," mwaka mmoja kabla ya kurejea Iran. Vitabu vingine mashuhuri vya msoni huyo ni "Kemia ya Saada" na "Nasaha za Wafalme."
Siku kama ya leo miaka 1147 iliyopita, yaani mwaka 291 Hijiria, alifariki dunia Abul-Abbas Ahmad bin Yahya, mtaalamu maarufu wa lugha na nahau. Abul-Abbas katika masomo yake alibobea katika ulingo wa fasihi ya Kiarabu na baada ya miaka kadhaa ya kufanya utafiti wa kina, akatokea kuwa mtaalamu mkubwa katika uwanja huo. Miongoni mwa athari zilizobakia kutoka kwa mtaalamu huyo, ni pamoja na kitabu maarufu kiitwacho 'I'raabul-Qur'an'.