Feb 21, 2017 08:27 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (2)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi, la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa, umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu, pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya pili.

*******

Mazungumzo yetu katika kipindi kilichopita yaliishia katika kujadili nukta ya msingi kuhusu umoja baina ya Waislamu, kwa kuuliza suali kwamba tunapozungumzia umoja baina ya Waislamu tunakusudia umoja wa jambo gani na wa aina ipi?  Tukajibu suali hilo kwa kuashiria kuwa kuna rai mbili zilizotolewa katika kujibu suali hili. Rai ya kwanza ni ya mtazamo wenye muelekeo ambao, tunaweza kuuita wa 'kiumakanika' juu ya umoja wa jamii ya Kiislamu, unaoitakidi kwamba ili kuwa na umoja, Waislamu wote, Mashia, Masuni na wengineo waache imani na itikadi zao za kimadhehebu na badala yake waamini na kuyatekeleza yale tu yanayoziunganisha pamoja madhehebu zote za Uislamu. Tukabainisha kwamba kwa mujibu wa mtazamo huu, Waislamu wote inapasa wafuate madhehebu moja ya pamoja, kwa namna ambayo hakutokuwapo na hitilafu wala tofauti yoyote katika itikadi na hukumu za kifiqhi katika jamii ya Kiislamu. Lakini tukaona kuwa rai ya pili ina mtazamo mwingine kuhusu umoja na kuwaunganisha Waislamu. Rai hii ina muelekeo tuwezao kuuita wa kioganiki na wenye kuzingatia maumbile na hali halisi. Kwa mujibu wa mtazamo wa rai hii, madhumuni na makusudio ya umoja baina ya Waislamu ni kwamba sambamba na wafuasi wa kila madhehebu kushikamana na itikadi na hukumu maalumu za madhehebu yao, katika uhusiano wa kijamii, kisiasa, kijeshi, kiuchumi na kiutamaduni wawe kitu kimoja na Waislamu wenzao na wazingatie maslahi makuu ya Uislamu na umma wa Kiislamu na wote kwa pamoja daima wawe mithili ya "mkono mmoja" na nguvu moja katika kukabiliana na maadui wa Uislamu.

Wapenzi wasikilizaji, ukweli ni kwamba umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu katika muelekeo wa kwanza, si jambo la dharura wala linaloyumkinika katika mazingira tuliyonayo. Umoja wa aina hiyo hauwezekani kufikiwa hata baina ya madhehebu nne maarufu za Ahlu Sunna, yaani Shafi, Hanafi, Maliki na Hanbali. Na sababu ni kwamba hitilafu katika baadhi ya masuala ya kiitikadi na hukumu za utekelezaji ni matokeo ya kimaumbile ya ijtihadi, fikra na tafakuri huru; na wala haziwi sababu ya kutengana nyoyo za Waislamu na kuwa mbalimbali. Hivyo basi, kinachopasa kuzingatiwa ni kurejea kwenye madhumuni ya aya za Qur’ani tukufu kuhusu sababu na vizuizi vinavyokwamisha kupatikana umoja na mshikamano wa Waislamu na kuzifanya aya hizo kuwa ndiyo dira ya mwenendo na matendo yetu ya binafsi na ya kisiasa na kijamii. Qur’ani tukufu ni mlinganiaji mkubwa zaidi wa umoja baina ya Waislamu na kitovu na mhimili mkuu wa jambo hilo, ambapo kwa kuwachorea Waislamu njia iliyonyooka ya kufuata, imewataka wajiepushe na mifarakano baina yao. Aya ya 153 ya Suratul An’am inasema:  Na kwa hakika hii ndiyo Njia yangu Iliyo Nyooka. Basi ifuateni, wala msifuate njia nyingine, zikakutengeni na Njia yake.

Mkutano wa Umoja wa Kiislamu

Vilevile katika sehemu ya aya ya 103 ya Suratu Aal Imran, Qur’ani tukufu inawaita na kuwalingania Waislamu washikamane na Kamba ya Mwenyezi Mungu huku ikiutaja umoja kuwa ni neema kwao kama aya yenyewe inavyosema:  Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Qur’ani tukufu inaitaja tauhidi na kumwabudu Mwenyezi Mungu kuwa ni msingi na mhimili wa mshikamano wa kisiasa na kijamii wa Waislamu na kuelezea suala la kuasisi umma mmoja wa Kiislamu kama aya ya 92 ya Suratul Anbiyaa inavyosema: Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo niabuduni Mimi. Kwa njia isiyo ya moja kwa moja, aya hii inakutaja kumwabudu Mwenyezi Mungu kuwa ni msingi wa umoja katika umma mmoja; na kumfuata asiyekuwa Yeye Mola kwamba ndio chanzo na sababu ya mfarakano. Bwana Mtume Muhammad SAW aliianza kazi yake ya kuwaita na kuwalingania watu dini ya Uislamu kwa kufuata msingi huu; na hadi lahadha ya mwisho ya uhai wake aliendelea kuwataka Waislamu wawe na umoja chini ya mhimili wa kumwabudu  Mungu mmoja na wawe kitu kimoja katika kukabiliana na maadui wa dini yao.

Wapenzi wasikilizaji, katika zama za ujahilia, wakati jamii za Waarabu zilikuwa zimetawaliwa na mifarakano, hasama na uadui wa kikaumu na kikabila ambayo kila mara ilikuwa ikizitumbukiza jamii hizo kwenye lindi la mapigano na umwagaji damu, Uislamu ulipodhihiri uliweza kuwaunganisha wafuasi wake na kuwafanya kitu kimoja kwa kufuata kauli mbiu ya “umoja na udugu kulingana na msingi wa kalima ya tauhidi ya Lailah illa Allah, na kujiepusha na mfarakano na uadui baina yao.” Dini ya Uislamu iliweza kuuthibitisha umoja kivitendo kwa kuifanya taqwa na uchaMungu kuwa mhimili na kigezo asili cha kila kitu na kukana aina zote zingine za kujitukuza na kujiona bora mtu, kama taasubi za ukaumu, ukabila, damu, asili au lugha yake. Kuanzia mwanzo wa kubaathiwa kwake na kupewa Utume hadi wakati anaaga dunia, Bwana Mtume Muhammad SAW alizitumia aya za Qur’ani katika kuwafunza watu mafundisho ya dini; na kwa mwenendo na sira yake mwenyewe alifanya kazi kubwa ya kupiga vita hitilafu na mifarakano na kuchukua hatua za kuimarisha misingi ya umoja, mshikamano, udugu na kuwa kitu kimoja baina ya Wislamu na kujenga maelewano hata baina ya Waislamu na Ahlul Kitab wasio na uadui na Waislamu.

Bwana Mtume Muhammad SAW ni kiungo muhimu sana cha Umoja wa Kiislamu.

Tarikh na historia ya zama za mwanzoni mwa Uislamu ni shahidi wa ukweli huu, kwamba kwa kutegemea msingi wa “Lailaha illa Allah” katika mwenendo na matendo yake, Nabii Muhammad SAW alizuia kutokea mifarakano baina ya Waislamu na kurudi nyuma tena kwenye masuala yanayochochea hitilafu na mifarakano ya zama za ujahilia. Japokuwa Bwana Mtume SAW alipewa Utume katika jamii ya Waarabu, na Qur’ani tukufu imeteremshwa kwa lugha ya Kiarabu, lakini wito wake ulivuka nje kabisa ya uwekaji kila aina ya mipaka ya ukabila, rangi, asili na lugha ya mtu na kusimamisha uadilifu wa kupigiwa mfano katika kuamiliana kwake na Waislamu Waarabu na wasio Waarabu. Kusilimu watu waliokuja kuwa masahaba wakubwa wa Mtume SAW kama Salman al-Farsy, Bilal al-Habashi na Suhaib ar-Rumi katika zama za mtukufu huyo na hadhi ya juu na heshima maalumu waliyokuwa nayo masahaba hao mbele ya Bwana Mtume mwenyewe na masahaba wenzao, ni ushahidi wa wazi wa kuthibitisha ukweli huo. Ni kwa sababu hiyo, ndio maana baada ya Uislamu kuenea na kujizatiti katika eneo la Bara Arabu, ulivuka mipaka na kusambaa kwa kasi katika maeneo mengine mengi ya dunia. Na ili kuzuia kufufuliwa taasubi za kikaumu na kikabila na kuepusha Waislamu wa Bara Arabu kuwatendea dhulma Waislamu wa miji mingine, Bwana Mtume Muhammad SAW alikuwa akiwasisitizia Waislamu kuwa, wao kwa wao ni ndugu na kwamba Muislamu wa kweli hamdhulumu ndugu yake wa dini wala hamsalimishi kwa dhalimu.

Mpenzi msikilizaji, sehemu ya pili ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Hivyo tusite hapa kwa leo hadi juma lijalo panapo majaaliwa ya Mola katika siku na saa kama ya leo ili kuendelea na sehemu ya tatu ya mfululizo huu.

 

Tags