Jumamosi, Machi 4, 2017
Leo ni Jumamosi tarehe 5 Mfunguo Tisa Jamad Thani 1438 Hijria sawa na tarehe 4 Machi 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1010 iliyopita, inayosadifiana na tarehe na tarehe 5 Mfunguo Tisa Jamadi Thani mwaka 428 Hijria, alifariki dunia Abul Hassan Mahyar Deilami, mshairi na mwandishi mashuhuri wa Kiirani. Awali msomi huyo alikuwa mfuasi wa dini ya Kizartoshti, hata hivyo kutokana na kupata elimu na miongozo kutoka kwa wasomi mashuhuri katika zama zake, hatimaye alisilimu na kuingia katika dini ya Kiislamu. Kwa muda mrefu Deilami alisoma kwa mwalimu wake Sayyid Radhi.***
Katika siku kama ya leo miaka 818 iliyopita, aliaga dunia huko Damascus Syria Ibn Qudamah Moqaddasi fakihi na mpokezi hadithi wa Kiislamu. Ibn Qudamah alihitimu masomo yake ya awali na ya utangulizi huko Damascus ambapo alijifunza Qur'ani na hadithi. Baadaye alifanya safari huko Baghdad katika Iraq ya leo na kuhudhuria masomo ya maulama na wanazuoni wakubwa katika zama hizo. Ibn Qudamah hakuwa nyuma pia katika uwanja wa uandishi wa vitabu na amevirithisha vizazi vilivyokuja baada yake vitabu vyenye thamani kubwa. Kitabu cha Raudhatun Nadhir ni moja tu kati ya vitabu hivyo.***
Miaka 766 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Maulana Jalaluddin Balkhi maarufu kwa jina la Moulavi mmoja wa malenga na washairi mahiri wa Iran. Moulavi alikuwa mshairi mkubwa na mwenye uwezo na kipaji kikubwa katika karne ya 7 Hijria. Alizaliwa mwaka 604 Hijria katika mji wa Balkhi kaskazini mwa Afghanistan ya leo. Miongoni mwa athari kubwa za Maulana au Jalaluddin Balkhi ni kitabu cha mashairi cha Masnavi Manavi.***
Na siku kama ya leo miaka 49 iliyopita sawa na tarehe 14 Esfand mwaka 1346 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, alifariki dunia Dakta Muhammad Musaddiq, Waziri Mkuu na mmoja wa wanasiasa mashuhuri wa Iran. Alizaliwa mjini Tehran mwaka 1261 Hijria Shamsia. Mwaka 1299 Hijria Shamsia ikiwa ni baada ya kuhudumu kama Waziri wa Fedha na Waziri wa Mambo ya Nje, Musaddiq alichaguliwa kuwa mwakilishi wa watu wa Tehran bungeni. Alifanya jitihada kubwa za kutaifishwa sekta ya mafuta nchini Iran na mwaka 1329 Hijria Shamsia alifanikiwa kupasisha kanuni ya kutaifishwa mafuta bungeni kwa himaya ya makundi ya Kiislamu chini ya uongozi wa Ayatullah Kashani. Baadaye aliondolewa madarakani katika mapinduzi yaliyoongozwa na Marekani tarehe 28 Mordad mwaka 1332 Hijria na kufungwa jela miaka mitatu. Baada ya kutumikia kifungu hicho Musaddiq alibaidishiwa katika kijiji kimoja huko magharibi mwa Tehran na alifariki dunia miaka kadhaa baadaye katika siku kama ya leo.