Mar 07, 2017 23:51 UTC
  • Jumatano, 8 Machi, 2017

Jumatano tarehe 9 Jamadithani 1438 Hijria sawa na Machi 8, 2017

Tarehe 8 Machi imetangazwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Mwanamke.

Siku hii awali ilianza kama tukio la kisiasa na kisoshalisti lakini baadaye liliunganishwa na tamaduni za nchi nyingi duniani. Siku ya Kimataifa ya mwanamke imepoteza sura yake ya kisiasa katika maeneo mengi ya dunia na kuwa mnasaba wa wanaume kuonesha na kueleza mapenzi yao kwa wanawake. Tangu mwaka 1977 Umoja wa Mataifa umeliitambua rasmi siku hii ya leo kuwa ni Siku ya Haki za Wanawake na Amani ya Kimataifa.

Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, inayosadifiana na 8 Machi 1968 ilianza Harakati ya Ukombozi ya Moro dhidi ya utawala wa dikteta Ferdinand Marcos nchini Ufilipino. Dikteta Marcos alikuwa mshirika na muitifaki mkubwa wa Marekani na katika utawala wake wa kidikteta, maelfu ya Waislamu wa Ufilipino waliuawa au kufungwa jela. Harakati ya Ukombozi ya Moro ilipambana kwa ajili ya kupigania haki za Waislamu, na ilihesabiwa kuwa harakati kubwa zaidi iliyopinga utawala wa Marcos nchini Ufilipino. Baada ya Marcos kuondoka madarakani mwaka 1986, harakati ya Moro ilikubali kutia saini makubaliano ya amani na serikali ya Manila.

Ferdinand Marcos

Na siku kama ya leo miaka 739 iliyopita yaani tarehe 9 Mfunguo Tisa Jamadi Thani mwaka 699 Hijria, Ibn Farah Eshbily malenga, mshairi na mtaalamu wa elimu ya hadithi katika karne ya saba Hijria alifariki dunia. Alizaliwa katika Andalusia ya zamani ambayo leo ni eneo la kusini mwa Uhispania. Alitiwa mbaroni baada ya majeshi ya Uhispania kuushambulia mji huo. Hata hivyo baada ya kushikiliwa kwa muda, alitoroka na kukimbilia nchini Misri. Akiwa nchini Misri Ibn Farah Eshbily alifanikiwa kuchota elimu na maarifa kwa maulama mashuhuri wa zama hizo mjini Cairo. Baada ya muda alielekea Damascus Syria na kujiendeleza zaidi kielimu. Alimu na msomi huyu wa Kiislamu ameacha athari nyingi za kielimu hususan katika uga wa mashairi.