Mar 12, 2017 16:29 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (3)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi, la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa, umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu, pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya tatu.

Katika kipindi kilichopita tulieleza kuwa katika zama za ujahilia, wakati jamii za Waarabu zilikuwa zimetawaliwa na mifarakano, hasama na uadui wa kikaumu na kikabila ambayo kila mara ilikuwa ikizitumbukiza jamii hizo kwenye lindi la mapigano na umwagaji damu, Uislamu ulipodhihiri uliweza kuwaunganisha wafuasi wake na kuwafanya kitu kimoja kwa kufuata kauli mbiu ya “umoja na udugu kulingana na msingi wa kalima ya tauhidi ya Lailah illa Allah, na kujiepusha na mfarakano na uadui baina yao.” Tukabainisha kwamba kuanzia mwanzo wa kubaathiwa kwake na kupewa Utume hadi wakati anaaga dunia, Bwana Mtume Muhammad SAW alizitumia aya za Qur’ani katika kuwafunza watu mafundisho ya dini; na kwa mwenendo na sira yake mwenyewe alifanya kazi kubwa ya kupiga vita hitilafu na mifarakano na kuchukua hatua za kuimarisha misingi ya umoja, mshikamano, udugu na kuwa kitu kimoja baina ya Wislamu na kujenga maelewano hata baina ya Waislamu na Ahlul Kitab wasio na uadui na Waislamu.

Bwana Mtume Muhammad SAW alikuwa akiutaja umoja na maelewano baina ya Waislamu na kujiepusha na unafiki na kuzusha mfarakano baina ya Waislamu kuwa ni moja ya alama za imani. Katika Hija yake ya kuaga maarufu kama Hijjatul-wida'ah Bwana Mtume SAW aliwakumbusha Waislamu kwa mara nyingine tena kuwa kipimo cha ubora katika Uislamu ni taqwa na kumchaMungu na akatamka bayana kwamba: "Hakuna Mwarabu aliye mbora kuliko Mwajemi, wala hakuna Mwajemi aliye mbora kuliko Mwarabu isipokuwa kwa uchaMungu". Na kwa njia hiyo, akaasisi na kurasimisha hati ya umoja wa Waislamu kwa msingi wa usuli wa tauhidi wa Lailaha illa Allah. Katika sira ya kivitendo ya Bwana Mtume Muhammad SAW pia kuna matukio kadhaa yanayoonyesha kuwa umoja ni moja ya mihimili mikuu ya wito wa Uislamu. Kwa kutoa mfano, hatua ya tadbiri na hekima aliyochukua mtukufu huyo ya kujenga mapenzi na upendo baina ya Muhajirina na Ansar, sio tu iliepusha kutokea fitna bali iliimarisha zaidi mafungamano ya nyoyo na ya kisiasa kati ya Waislamu na kuzima njama za Mayahudi na wanafiki za kutaka kuzusha hitilafu baina ya Waislamu. Kwa mujibu wa mkataba huo, Muhajirina na Ansar kila mmoja alitakiwa ajione ndugu kwa mwenzake na kuwa na dhima na mas-ulia juu yake. Kwa msingi huo Ansar wakachukua hatua ya kugawana sawa kwa sawa mali zao na Muhajirina na hata kuwapatia maskani katika majumba yao ndugu zao hao. Kwa kuzingatia tofauti ya uwezo wa kiuchumi iliyokuwepo baina ya Muhajirina na Ansar hatua hiyo ilikuwa na taathira na umuhimu mkubwa mno na kuvunja njama na hila za maadui.

Kamisheni maalumu ya Mkutano wa Wahda wa Kiislamu

 

Hata wakati Bwana Mtume SAW alipokuwa katika siku za mwisho za uhai wake alifanya jitihada za kung'oa mizizi ya ujahili na taasubi za kikabila, za asili na za kikoo na ndiyo maana katika kipindi hicho alitoa hotuba maalumu ya kukemea mfarakano na kubainisha hofu aliyokuwa nayo, ya Waislamu kurejea kwenye mila za shirki na mifarakano, za zama za ujahilia. Vilevile katika Hija yake ya kuaga, ili kuepusha kutokea hitilafu baina ya Waislamu baada ya kuondoka kwake alimtangaza dhahiri shahir Imam Ali (as) kuwa Khalifa wake na kiongozi wa umma baada yake. Hata hivyo licha ya wasia alioacha Bwana Mtume SAW kwa umma wake wa kulinda na kudumisha izza na adhama ya Waislamu, na pamoja na kwamba alisha mchagua na kumtangaza Khalifa wa baada yake, mara baada ya yeye kutawafu, baadhi ya Waislamu walikusanyika mahala panapoitwa Saqifah na kupitisha uamuzi kuhusiana na kumchagua Khalifa wa Mtume. Kwa masikitiko, kadhia ya Saqifah ilipanda mbegu ya hitilafu na mifarakano na kusababisha kutokea mzozo na mabishano juu ya kumuainisha Khalifa. Na kwa njia hiyo, baada ya kutawafu Bwana Mtume Muhammad SAW, Saqifah pakawa mahala pa kuchipua na kumea mmea wa sumu za hitilafu na migogoro ndani ya jamii ya Kiislamu. Katika kipindi hicho, wakati kadhia ya Saqifah ingeweza kugeuka mahala pa kuripuka tena moto uliokuwa ukifukuta chini ya jivu, kwa hekima ya Imam Ali (as) ya kuzingatia maslahi na mustakabali wa umma, mkusanyiko huo ulihatimishwa pasina kutokea mgogoro; na umoja wa Waislamu ukaendelea kuwepo pasina kuathiriwa na kiu za madaraka ya kisiasa.

Katika kipindi hicho muhimu cha historia Imam Ali (as) alisamehe haki yake ya wazi kabisa na akajizuia kuchukua msimamo dhidi ya makhalifa ili kulinda na kudumisha umoja na mshikamano wa Waislamu. Baada ya kadhia ya Saqifah na kuanza Ukhalifa wa Abubakar, Imam Ali (as) aliamua tangu mwanzo kujipambanua na wakosoaji wengine wa Ukhalifa; na kinyume na wengi wao ambao walipingana na Khalifa kwa sababu ya kutaka madaraka, yeye aliamiliana na suala hilo kwa namna ya kutousababishia madhara Uislamu wenyewe na umoja wa Waislamu. Wakati upinzani dhidi ya Abubakar ulipokuwa umeshtadi, huku zikifanyika jitihada za watu kutaka kum'bai Imam Ali na kumuunga mkono yeye kuwa Khalifa, mtukufu huyo aliwatahadharisha watu waliokuwa wakimpinga Khalifa juu ya "fitna" na hatua za kuleta mifarakano kwa lengo la kufufua taasubi za kikaumu. Imam Ali alisema: "Mawimbi ya fitna yamepanda na merikebu ya Uislamu imezungukwa na mkondo wa maji; kutokea kila upande na kila pembe ya anga ya Waarabu imeibuka fitna, na kutoka kwenye kila fitna kuna wimbi lililopanda. Madina, ambayo ni kitovu cha Uislamu imo kwenye dhoruba za mawimbi hayo; leo kila harakati inashadidisha tufani hii na kugharikisha pia zilikoanzia harakati zenyewe. Inapasa kuzikhalifu njia zinazozidisha hitilafu na kuyaweka kando mambo ya kutafakhari, taasubi za kikaumu na utangulizi binafsi wa mtu (katika Uislamu). Kwa sababu, haya yanayofanyiwa fakhari, ni mithili ya mataji yatengezwayo na watu, na hayana thamani katika Uislamu".

Mkutano wa Umoja wa Kiislamu jijini Tehran

 

Wakati baadhi ya watu wa Madina walipokuwa wakimwendea na kumwomba mara kwa mara achukue hatua dhidi ya Khalifa wa Waislamu, Imam Ali alikuwa akiwausia kuwa watulivu na kuwakumbusha kwamba kuilinda na kuihifadhi dini ibaki salama ni muhimu zaidi kuliko kitu chochote. Katika zama za uongozi wa Khalifa wa kwanza, Imam Ali (as) alimpa msaada katika mambo mengi; na yeye Khalifa akitaka ushauri kwa Imam Ali katika mambo mbalimbali ya uendeshaji utawala ikiwemo kutuma jeshi kwa ajili ya vita vya Jihadi.

Mwenendo wa Imam Ali (as) wa kutoa ushauri, miongozo na fikra kwa makhalifa na kujishughulisha na masuala ya kisiasa na kijamii ya jamii ya Kiislamu kwa madhumuni ya kuendeleza na kudumisha muelekeo wa umoja uliendelea pia katika zama za makhalifa waliofuatia. Katika zama za Ukhalifa wa Omar, mara kadha wa kadha Imam Ali alitoa ushauri na msaada kwa Khalifa, kwa sababu kama angeacha kufanya hivyo yamkini hukumu na maamuzi ya kiutawala ambayo yangepitishwa yangesababisha madhara makubwa na ya kusikitisha kwa jamii ya Kiislamu na Uislamu wenyewe. Kiwango cha huduma na ushauri ambao Ali (as) alikuwa akiutoa kwa Omar kilikuwa kikubwa na chenye umuhimu kiasi cha kumfanya Khalifa huyo wa pili atamke mara kadhaa kwamba: Laiti kama si Ali, Omar angeangamia.

Mpenzi msikilizaji, sehemu ya tatu ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Hivyo tusite hapa kwa leo hadi juma lijalo panapo majaaliwa ya Mola katika siku na saa kama ya leo ili kuendelea na sehemu ya nne ya mfululizo huu…/

Tags