Mar 12, 2017 16:32 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (4)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi, la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa, umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu, pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya nne.

Katika kipindi kilichopita tulieleza kuwa katika enzi za uongozi wa Khalifa wa kwanza Abubakar, Imam Ali (as) alimsaidia katika mambo mengi; na yeye Khalifa alikuwa akitaka ushauri kwa Imam Ali katika mambo mbalimbali ya uendeshaji utawala ikiwemo kutuma jeshi kwa ajili ya vita vya Jihadi. Tukaashiria kuwa mwenendo wa Imam Ali (as) wa kutoa ushauri, miongozo na fikra kwa makhalifa na kujishughulisha na masuala ya kisiasa na kijamii ya jamii ya Kiislamu kwa madhumuni ya kuendeleza na kudumisha muelekeo wa umoja uliendelea pia katika zama za makhalifa waliofuatia. Katika zama za Ukhalifa wa Omar, mara kadha wa kadha Imam Ali alitoa ushauri na msaada kwa Khalifa, kwa sababu kama angeacha kufanya hivyo yamkini hukumu na maamuzi ya kiutawala ambayo yangepitishwa yangesababisha madhara makubwa na ya kusikitisha kwa jamii ya Kiislamu na Uislamu wenyewe. Kiwango cha huduma na ushauri ambao Ali (as) alikuwa akiutoa kwa Omar kilikuwa kikubwa na chenye umuhimu kiasi cha kumfanya Khalifa huyo wa pili atamke mara kadhaa kwamba: Laiti kama si Ali, Omar angeangamia. Aidha licha ya malalamiko na upinzani aliokuwa nao kuhusiana na jinsi alivyochaguliwa Othman, Imam Ali (as) alimbai na kushirikiana naye kwa kujitolea kwa hali zote kwa sababu ya kulinda umoja wa Waislamu. Wakati muelekeo wa kisiasa na kijamii wa Othman ulipokabiliwa na malalamiko ya kila upande, Imam Ali alimpa nasaha na ushauri kiungwana na kwa heshima kamili na kumtaka ajiepushe na ufufuaji taasubu za zama za ujahilia na kutoa upendeleo wa kisiasa na kijamii kwa jamaa zake. Hata wakati Waislamu walipokuwa wamechoshwa na kuishiwa na uvumilivu kutokana na utaratibu wa uendeshaji utawala wa Othman na licha ya ukosoaji mkubwa na lawama chungu nzima zilizotolewa dhidi ya mfumo wa uongozi wa Khalifa huyo wa tatu, Ali (as) hakuunga mkono uasi ili kuepusha kutokea mfarakano kati ya Waislamu; na hata akawatuma watoto wake mwenyewe wakamlinde Khalifa.

Umoja na udharura wa kukabiliana na makundi ya kitakfiri

 

Mbali na kuzuia kupanuka wigo wa hitilafu baina ya Waislamu, Imam Ali aliitahadharisha jamii ya Waislamu na matokeo hatari ya mfarakano na mgawanyiko. Aliwaasa Waislamu kwa kuwaambia: Jihadharini na mfarakano na utengano kwa sababu mtu aliye peke yake ni windo la shetani, kama kondoo aliye peke yake alivyo windo la mbwa mwitu" (Nahjul-Balaghah, hotuba ya 127)

Wakati alipopata habari kwamba kuna baadhi ya watu wa kabila la Bani Hashim wanazozana na baadhi ya Makureishi na kubishania mambo ya ukaumu, Imam Ali (as) aliwatahadharisha na kuwapelekea ujumbe wa kuwataka waachane na mambo hayo ya kuchochea hitilafu. Katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake pia Ali (as) alifanya jitihada za kulinda na kudumisha umoja wa jamii ya Kiislamu kwa kuamiliana kwa upole na uvumilivu na wapinzani; na kwa muda ambapo hawakubeba silaha kupigana dhidi ya utawala wa Kiislamu hakuchukua hatua yoyote dhidi yao na wala hakuwazuilia haki zao katika mfuko wa hazina ya Waislamu ya Baitul-maal.

Katika wasia wake wa mwisho kwa mwanawe Imam Hassan (as) mtukufu huyo alimsisitizia kulinda umoja na kushikamana na Kamba ya Allah na kujiepusha na mifarakano, huku akimnukulia maneno aliyoyasikia kutoka kwa mtukufu Mtume SAW kwamba kulinda umoja wa Waislamu kuna fadhila zaidi kuliko hata Sala na Funga. Alimwambia mwanawe Hassan (as): "Shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu na jiepusheni na mfarakano, kwani nimemsikia Mtume wa Allah akisema, tambueni kuwa kusuluhisha mambo baina yenu kuna fadhila zaidi kuliko Funga na Sala zote".

Wapenzi wasikilizaji, kabla ya kuendelea mbele na safari hii ndefu ya kuvuka mabonde na mito na misitu na nyika ili kuchanganua yaliyojiri katika historia ya Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu tuyafanyie ufupisho na muhtasari kwanza yale tuliyoyazungumza hadi sasa katika mfululizo huu. La kwanza ni kuwa tumeashiria nukta kadhaa kuhusu nafasi yenye umuhimu mkubwa ya umoja na mshikamano baina ya Waislamu kwa mujibu wa aya za Qur'ani na vilevile mbinu aliyotumia Bwana Mtume Muhammad SAW katika kujenga na kuimarisha umoja wa Umma wa Kiislamu.  Kama ambavyo tumeeleza kuwa kwa kutumia kaulimbiu ya "umoja na udugu na kujiepusha na mfarakano na uadui kulingana na msingi wa kalima ya tauhidi ya Lailah illa Allah" Uislamu uliweza kuondoa mifarakano na hasama za kikaumu na kikabila zilizokuwepo baina ya Waarabu katika zama za ujahilia. Mizozo na mifarakano hiyo ilikuwa ikisababisha mapigano na umwagaji damu; lakini ilifutika na kutoweka chini ya kivuli cha tauhidi na imani ya Mungu mmoja. Miongoni mwa tuliyoyaashiria hadi sasa ni kadhia ya kuundwa shura baada ya kuaga dunia Bwana Mtume SAW katika mahala panapoitwa "Saqifah". Licha ya wasia ulioachwa na mtukufu huyo wa kulindwa na kudumishwa izza na adhama ya Waislamu, yaliyojiri katika tukio la Saqifah yalisababisha kutokea mlolongo wa hitilafu na mizozo katika jamii ya Kiislamu. Hata hivyo kwa hekima ya Imam Ali (as) ya kuzingatia maslahi na mustakabali wa umma, mkusanyiko huo ulihatimishwa pasina kutokea mgogoro; na umoja wa Waislamu ukaendelea kuwepo pasina kuathiriwa na kiu za madaraka ya kisiasa.

Hatukukutuma (ewe Muhammad) ila uwe rehema kwa walimwengu wote

 

Katika zama za uongozi wa makhalifa mipaka ya ardhi za Waislamu ilipanuka kwa kiwango kikubwa na hitilafu mbalimbali zilijitokeza baina yao lakini umoja wa jamii ya Kiislamu haukuvunjika. Hitilafu hizo ambazo chimbuko lake lilikuwa ufufuaji wa taasubi na ukereketwa wa kikaumu na kikabila ulifikia kiwango mpaka cha kusababisha mauaji ya makhalifa; lakini pamoja na hayo mshikamano wa Ulimwengu wa Kiislamu kama kitu kimoja uliendelea kulindwa. Baada ya kuuliwa shahidi Imam Ali (as) na Ibn Muljim Muradi, vidonda vilivyokuwa vimeanza kufanya kovu vya chuki za enzi za ujahilia vilitonesheka na kufumuka tena na cheche za moto wa utengano na mfarakano zikaripuka tena; na kufufuliwa tena hulka ya uashrafu na ubwanyenye pamoja na taasubi za kikaumu, rangi na asili za watu, ambako kuliutia doa umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu. Katika kipindi hicho, kwanza utaratibu wa kuainisha Khalifa ulibadilika, ukawa sasa ni wa kurithishana. Muawiyah bin Abi Sufyan, si kwa sababu ya sifa za kitabia, za kidini na kisiasa au hata kwa hoja ya kukubaliwa na watu wengi, alimfanya mwanawe Yazid kuwa Khalifa baada yake kwa msingi wa kumritihisha utawala. Katika zama za utawala wa Bani Umayyah siasa za mifarakano kwa sababu ya rangi na asili za watu, na utengano kwa misingi ya ukaumu ilipamba moto na kuandaa mazingira ya kujitokeza mpasuko na mgawanyiko wa kijamii.

Mpenzi msikilizaji, sehemu ya nne ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Hivyo tusite hapa kwa leo hadi juma lijalo panapo majaaliwa ya Mola katika siku na saa kama ya leo ili kuendelea na sehemu ya tano ya mfululizo huu…/

Tags