Mar 12, 2017 23:09 UTC
  • Jumatatu 13 Machi, 2017

Leo ni Jumatatu 14 Jamadithani 1438 sawa na 13 Machi, 2017

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, inayosadifiana na 13 Machi 1983, Joshua Nkomo kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe alikimbilia nchini Uingereza akihofia usalama wa maisha yake. Nkomo ambaye alikiongoza chama cha Zimbabwe African People's Union (ZAPU) alisema kuwa, alilazimika kutoroka nchini Zimbabwe na kukimbilia Uingereza kwa kuwa maisha yake yalikuwa hatarini. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Brigedi ya Tano ya jeshi la Zimbabwe kuizingira kambi yake iliyoko katika mji wa Bulawayo.

Nkomo kulia, na Mubabe kushoto

Tarehe 13 Machi miaka 69 iliyopita Wazayuni waliokuwa na mfungamano na kundi la kigaidi la Haganah, walishambulia kitongoji cha Wapalestina cha Husseiniyah katika eneo la kaskazini mwa Jalilah. Wazayuni hao waliua shahidi zaidi ya Wapalestina 60 na kuharibu nyumba zao kadhaa. Katika siku hiyohiyo, wanajeshi wa Israel walizilipua kwa mabomu nyumba za Wapalestina katika eneo la 'Qatmuun' lililoko Baitul Muqaddas. Mauaji ya Waislamu wa Palestina yaliyofanywa na makundi ya kigaidi ya Israel, yalitekelezwa kwa lengo la kutaka kutangaza uwepo wa utawala huo bandia kwenye ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina baada ya kuondoka vikosi vya majeshi ya Uingereza katika eneo hilo.

Siku kama ya leo miaka 284 iliyopita, inayosadifiana na 13 Machi, 1733 alizaliwa Joseph Priestley, mkemia na mwanafizikia wa Uingereza. Priestley alikuwa mashuhuri mno hasa katika taaluma ya kemia. Katika uchunguzi na utafiti wake, aliweza kuvumbua uvutaji pumzi katika mimea na hewa za oksijeni na nitrogen. Joseph Priestley alifariki dunia mwaka 1804.

Joseph Priestley

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita sawa na tarehe 23 Esfand 1340 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abul Qassim Kashani, mwanachuoni na shakhsia maarufu wa kisiasa katika historia ya Iran. Ayatullah Kashani alifanikiwa kupata daraja la ijtihadi akiwa bado barobaro huko Najaf nchini Iraq lakini baadaye alifukuzwa nchini humo kutokana na misimamo yake ya kupinga ukoloni wa Uingereza. Aliporejea nchini Iran, Ayatullah Kashani aliendelea na misimamo yake ya kupambana na ukoloni wa Uingereza na kufungwa jela mara kadhaa. Baada ya kutoka jela wananchi wa Tehran walimchagua kuwa mwakilishi katika bunge la Taifa.

Ayatullah Sayyid Abul Qassim Kashani

Miaka 933 aliyopita katika siku kama hii ya leo, alifariki dunia msomi na mtaalamu wa fiq'hi wa Kiiran Abu Hamid Muhammad Ghazali Tusi, maarufu kwa jina la Imam Muhammad Ghazali. Baada ya kuaga dunia baba yake, yeye na kaka yake, Ahmad walilelewa na Ahmad bin Radkani. Ghazali alisoma elimu ya fiq'hi kutoka kwa Abu Nasri Ismail na baada ya kufikia umri wa miaka 28 alikuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu katika elimu hiyo. Umaarufu wa Imam Muhammad Ghazali ulipelekea kiongozi wa Iraq wakati huo Khoja Nidham al-Mulk kumwalika msomi huyo kwenda mjini Baghdad kwa ajili ya kufundisha. Hatimaye alirejea Iran na kujishughulisha na masuala ya ualimu. Kabla ya kurejea Iran, Imam Muhammad Ghazali alipata kuandika vitabu vya thamani kama "Ihyau Ulumud Din," "Kemia ya Saada" na "Nasaha za Wafalme."

Imam Muhammad Ghazali