Mar 14, 2017 23:02 UTC
  • Jumatano 15 Machi, 2017

Leo ni Jumatano tarehe 16 Jamadithani 1438 sawa na Machi 15, 2017.

Siku kama hii ya leo miaka 28 iliyopita ardhi ya Taba huko kaskazini mashariki mwa Misri ilikombolewa baada ya kukaliwa kwa mabavu kwa miaka kadhaa na utawala ghasibu wa Israel. Utawala wa Kizayuni ulilikalia kwa mabavu jangwa la Sinai katika vita vya mwaka 1967, ambalo upande wa mashariki mwake linapatikana eneo la Taba. Utawala wa Tel Aviv ulikubali kuirejeshea Misri jangwa la Sinai baada ya kusaini mkataba wa Camp David mwaka 1987. Israel iliendelea kulikalia kijeshi eneo muhimu la Taba huko kaskazini mwa Ghuba ya Aqaba, licha ya utawala huo wa Kizayuni kuondoka katika baadhi ya sehemu za jangwa hilo.

Ardhi ya Taba, kaskazini mashariki mwa Misri

Miaka 29 iliyopita utawala wa zamani wa Iraq wa Baath uliushambulia mji wa Wakurdi wa Halabcha huko kaskazini mashariki mwa Iraq. Makumi ya ndege za kivita za utawala wa Saddam Hussein zilifanya mashambulizi ya kinyama kwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya raia wa Kikurdi wa mji wa Halabcha. Utawala wa Baath ulianzisha mashambulizi hayo katika hali ambayo kwa upande mmoja utawala huo ulikuwa umeshindwa kukabiliana na wapiganaji wa Kiislamu wa Iran na wa Kikurdi wa Iraq na kwa upande wa pili wananchi Waislamu wa Halabcha waliwakaribisha na kuwaunga mkono wapiganaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na dhulma na ukandamizaji usio na kipimo waliokuwa wakifanyiwa na Saddam Hussein. Nchi za Magharibi ambazo ndizo zilizoupatia utawala wa Saddam teknolojia na nyenzo zinazohitajika kwa ajili ya uzalishaji wa silaha hizo za kemikali, hazikuchukua hatua yoyote ya kivitendo mbele ya jinai hizo za Saddam Hussein, licha ya karibu watu elfu tano kuuawa katika maafa hayo ya kutisha ya Halabcha.

Halabcha

Siku kama ya leo miaka 163 iliyopita alizaliwa tabibu maarufu wa Kijerumani kwa jina la Emil Adolf von Behring. Behring aliendeleza utafiti wa Louis Pastor, mwanakemia wa Kifaransa wa zama hizo katika uwanja wa kutambua na kuzuia maradhi yanayoambukiza na kupata mafanikio makubwa katika suala hilo. Emil Adolf von Behring alitunukiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya fizikia mwaka 1901.

Emil Adolf von Behring

Na miaka 1017 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Ibn Darraj Qastalli mshairi na mwandishi mwashuhuri wa Andalusia. Ibn Darraj alizaliwa mwaka 347 Hijiria na alikuwa miongoni mwa washairi wakubwa wa Andalusia huko kusini mwa Uhispania ya leo. Pia alikuwa na nafasi muhimu katika kukuza mashairi ya Kiarabu mwishoni mwa karne ya 4 na mwanzoni mwa karne ya 5 Hijiria. Ibn Darraj ndiye aliyeleta mtindo mpya wa mashairi ya Kiarabu huko Andalusia na mashairi yake mbali na kuwa na thamani ya kifasihi na kisanaa pia yanahesabiwa kuwa chanzo cha kuaminika kinachoonyesha matukio ya wakati huo ya Uhispania. 

ابن دراج قسطلی