Jumamosi 18, Machi, 2017
Leo ni Jumamosi 19 Jamadithani 1438 Hijria sawa na 18 Machi, 2017
Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, hatimaye mapambano ya wananchi Waislamu wa Algeria yaliyoanzishwa kwa lengo la kuikomboa nchi hiyo na kukomesha uvamizi wa kikoloni wa Ufaransa yalipata ushindi baada ya miaka minane ya vita vikali. Watu milioni moja waliuawa katika vita hivyo. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa pili wa Evian, Ufaransa ilitambua uhuru wa Algeria na kuwaondoa wanajeshi wake nchini humo. Hata hivyo jeshi la siri la Ufaransa liliendeleza operesheni za kigaidi kwa muda nchini Algeria. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Algeria wakati huo ilikuwa ikiongozwa na Yusuf bin Khada na baadaye nchi hiyo ikawa chini ya utawala wa Ahmad bin Bella.

Miaka 95 iliyopita katika siku kama ya leo, Mahatma Gandhi, kiongozi mpigania uhuru wa India aliyekuwa akifanya jitihada za kuiondoa nchi hiyo katika ukoloni wa Uingereza kwa njia ya amani alikamatwa na baadaye kuhukumiwa kifungo cha miaka 6 jela. Kutiwa mbaroni Gandhi kulizidisha hasira na chuki za wananchi wa India dhidi ya Waingereza na kutia nguvu azma yao ya kupambana kwa ajili ya kuikomboa nchi yao. Katika mapambano yake Gandhi alitumia mbinu iliyoitwa 'Satyagraha' ambayo inamaanisha kutafuta hakika na kweli. Mbinu hiyo isiyotumia mabavu na ghasia, ilikusudiwa kudhihirisha makosa ya adui na kumlazimisha abadili mwenendo wake.
Miaka 159 iliyopita siku kama leo, alizaliwa mvumbuzi mashuhuri wa Kijerumani, Rudolf Diesel, ambaye alibuni injini ya diseli. Diesel alifanya utafiti na uhakiki mkubwa kuhusu injini za mitambo mbalimbali na akafanikiwa kuvumbua chombo ambacho kinaweza kuzalisha nishati kubwa zaidi bila ya kuhitaji umeme lakini kwa kutumia nishati ya kawaida na rahisi zaidi. Chombo hicho ambacho kilipewa jina lake mwenyewe la Diesel kilileta mabadiliko makubwa katika sekta ya viwanda na usafirishaji kwa kadiri kwamba licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia lakini injini za diseli zingalia zinatumika kwa kuwa ni zenye nguvu kubwa na zinazotumia nishati ndogo. Rudolf Diesel alifariki dunia mwaka 1913.