Mar 19, 2017 03:34 UTC
  • Jumapili 19 Machi

Leo ni Jumapili tarehe 20 Jamadu th-Thani 1438 Hijria mwafaka na tarehe 19 Machi 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1446 iliyopita yaani sawa na tarehe 20 Jamadu th-Thani mwaka wa nane kabla ya Hijiria, alizaliwa Bibi Fatwimat Zahraa (as) Binti ya Mtukufu Mtume Muhammad (saw). Tangu utotoni mwake, Bibi Fatwimah alikulia katika nyumba ya wahyi na chini ya malezi bora ya baba yake Nabii wa Allah na hivyo kufikia daraja la juu la ukamilifu katika elimu na ubora. Aidha Bibi Fatwimah (as) alikuwa na nafasi muhimu katika kupunguza machungu na tabu zilizokuwa zikimkumba baba yake katika harakati za kueneza mafundisho ya dini ya Uislamu, kutoka kwa washirikina. Mwaka wa pili Hijiria binti huyo mtukufu wa Mtume alifunga ndoa kwa sherehe nyepesi sana na Imamu Ali Bin Abi Twalib, ambaye naye ni dhihirisho la haki, uadilifu na uchaji-Mungu. Akiwa na Imamu Ali (as) Bibi Fatwimah aliishi kwa Amani na furaha ya juu huku akitekeleza majukumu ya mke na mama mwema kwa watoto wake watukufu, yaani Imamu Hassan, Imamu Hussein na Bibi Zainab (as.) mbali na majukumu hayo ya nyumbani, mwanamke huyo ambaye ni kiigizo chema, alikuwa akitekeleza pia majukumu ya kijamii katika kutumikia dini tukufu ya Kiislamu kiasi kwamba, muda mfupi baada ya kufariki dunia baba yake yaani mwaka wa 11 Hijiria, huku akiwa mwenye huzuni na machungu mengi kutokana na jamii kwenda kando na njia sahihi, alisimama na kuwaelekeza Waislamu kunako kufuata njia sahihi hadi alipofariki dunia. Sehemu moja ya hotuba za mtukufu huyo, inasema: "Mwenyezi Mungu amekupatieni Imani ambayo ni njia ya kukusafisheni kutokana na ushirikina na swala kuwa njia ya kukutakaseni na kiburi na kututi sisi kuwa sababu ya kuhifadhiwa mfumo wa dini na kutufuata kuwa kinga ya mfarakano na kutupenda kuwa sababu ya izza ya Uislamu." Kufuatia siku kama yaleo, Redio Tehran inatoa mkono wa kheri na fanaka kwa Waislamu na wapenzi wote wa familia ya Mtume Muhammad (saw.)

Siku kama ya leo miaka 1119 iliyopita alifariki dunia Muhammad Bin Abdu s-Swamad Baghdadi, mtaalamu wa hadithi wa Waislamu. Abdu s-Swamad Baghdadi alifanya juhudi kubwa katika kutafuta elimu tofauti za Kiislamu hususan elimu ya hadithi. Katika uwanja huo alinakili hadithi zenye itibari kutoka kwa wapokezi kadhaa wanaoishia kwa Mtume na Imamu Ali Bin Abi Twalib (as.) Baadhi ya athari za msomi huyo ziko mikononi mwa maulama wa Kiislamu.

Muhammad Bin Abdu s-Swamad Baghdadi

Siku kama ya leo miaka 118 iliyopita, alizaliwa Imam Ruhullah Musawi Khomein (MA) Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko mjini Khomeyn katikati mwa Iran. Imam Khomein (MA) alianza kusoma masomo ya kidini akiwa na umri mdogo mjini hapo kabla ya kuelekea mjini Qum kwa ajili ya masomo ya daraja ya juu katika uwanja huo.  Akiwa mjini Qum Imam Ruhullah Musawi Khomein alipata kusoma kwa maulama wakubwa na kutokana na maandalizi makubwa ya kielimu aliyokuwa nayo, haraka akafikia daraja ya ijtihadi. Mbali na fiq’hi, Imam Khomein (MA) alitabahari pia katika elimu za falsafa, irfan huku akiwa pia mahiri katika fani ya mashairi. Licha ya kuwa mwanazuoni huyo, alianza harakati zake za kisiasa akiwa kijana, lakini mapambano yake makubwa dhidi ya utawala wa Shah yalishtadi zaidi mnamo mwaka 1342 Hijiria Shamsia sawa na 1963 Miladia. Mapambano ambayo yalipelekea kubaidishwa kwake nchini Uturuki na kisha Iraq. Katika kipindi chote cha kubaidishwa kwake Imam Khomein (MA) situ kwamba alijishughulisha na malezi ya wanafunzi, bali pia aliendeleza mapambano na kufichua njama mbalimbali za utawala wa wakati huo nchini Iran.

Ruhullah Musawi Khomein (MA) Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Siku kama ya leo miaka 134 iliyopita alizaliwa Sir Norman Haworth, mtaalamu wa kemia wa Uingereza. Sir Haworth alifanya utafiti na uhakiki mwingi wa kisayansi kuhusu haidrokaboni na akafanikiwa kubuni mpango mpya kwa ajili ya muundo wa molekuli ya sukari. Vilevile Sir Haworth alifanya utafiti na majaribio kuhusu vitamini C ambayo muundo wa molekuli yake unashabihiana na sukari na akatayarisha aina yake ya kutengenezwa viwandani kwa jina la asidi askobiki. Mwaka 1937 Sir Norman Haworth alitunukiwa tuzo ya kemia ya Nobel kutokana na uhakiki na utafiti wake mkubwa. Alifariki dunia mwaka 1950.

Sir Norman Haworth, mtaalamu wa kemia wa Uingereza

Siku kama ya leo miaka 117 iliyopita, alizaliwa mjini Paris, Ufaransa Frederic Joliot, mwanafizikia na mkemia. Baada ya kuhitimu masomo yake ya chuo kikuu, alikuwa msaidizi wa Marie Curie, mtaalamu wa fizikia na mvumbuzi wa radium (elementi ya kemikali.) Akiwa kwa Curie alifunga ndoa na mtoto wa mwalimu wake huyo ambapo kwa msaada wa mke wake akafanikiwa kuvumbua mpandano wa mionzi nunurishi. Frederic Joliot alifariki dunia mwaka 1958 Miladia.

Ufaransa Frederic Joliot, mwanafizikia na mkemia

Na siku kama ya leo miaka 30 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Machi 1987 alifariki dunia Louis de Broglie, ambaye alikuwa wa mwisho katika kizazi cha waasisi wa fizikia ya kisasa akiwa na umri wa miaka 95. Louis de Broglie alizaliwa mwaka 1892 na baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia alianza utafiti wa elimu ya fizikia. Mtaalamu huyo wa fizikia wa Ufaransa alitatua masuala mengi ya elimu hiyo kwa nadharia yake mashuhuri ya Wave Particle Duality. Mwaka 1929 alitunukiwa tuzo ya fizikia ya Nobel.

Louis de Broglie,