Jumanne, 21 Machi, 2017
Leo ni Jumanne tarehe Mosi mwezi wa kwanza wa Farvardin mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia inayosadifiana na 22 Jamadithani 1438, sawa na Machi 21, 2017.
Leo ni tarehe Mosi Farvardin mwaka mpya wa 1396 Hijria Shamsia ambayo inasadifiana na siku ya kwanza ya mwaka wa Kiirani maarufu kwa jina la Sikukuu ya Nowruz. Nowruz ni moja kati ya sherehe za kale zaidi duniani na ilianza kusherehekewa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Mbali na Iran nchi ambazo husherehekea Nowruz ni pamoja na Afghanistan, Jamhuri ya Azerbaijan, Albania, Kyrgyzstan, Turkmenistan, Macedonia, India, Uturuki, Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia, Sudan na Zanzibar nchini Tanzania. Mwaka 2010 Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi tarehe Mosi Farvardin kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nowruz. Umoja wa Mataifa umeitambua Siku ya Nowruz kama siku kuu ya kale ambayo huadhimishwa wakati wa kuwadia msimu wa machipuo na kuhuishwa tena mazingira.
Tarehe 22 Jamadithani katika siku kama ya leo miaka 1047 iliyopita kwa mujibu wa nukuu za baadhi ya wanahistoria, alifariki dunia malenga mashuhuri wa Kiislamu Ibn Hajjaj. Alizaliwa huko Baghdad Iraq na akiwa kijana alianza kujifunza utunzi wa mashairi na kuwa rafiki na malenga mashuhuri Mahlabi. Moja kati ya athari za Ibn Hajjaj ni diwani yake ya mashairi yenye juzuu kumi ambayo baadhi yake yamehifadhiwa katika maktaba ya Baghdad. Vitabu vingine vya Ibn Hajjaj vimehifadhiwa katika sehemu mbalimbali za dunia kama vile katika majumba ya makumbusho ya Uingereza na katika Chuo Kikuu cha Istanbul, Uturuki.
siku kama ya leo miaka 249 iliyopita inayosadifiana na 21 Machi 1768, alizaliwa Joseph Baron Fourier mwanahisabati na mwanafizikia mashuhuri wa Ufaransa. Baron Fourier alikuwa ni miongoni mwa wahadhiri wa mwanzoni kabisa waliofundisha somo la hesabati mara baada ya kuanzishwa Chuo Kikuu cha Paris.
Miaka 49 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitokea mapigano makubwa kati ya harakati ya PLO ya Palestina na majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika mji wa Karama ulioko Jordan. Kwa uchache wanajeshi 1,230 wa Kizayuni waliangamizwa na makumi ya vifaru kutekelezwa au kuchukuliwa ngawira na wanamapambano wa Kipalestina kwenye mapigano hayo. Harakati ya PLO ilianza kupoteza hadhi yake ya kimapambano baada ya kulegeza misimamo yake ya kimapinduzi mwaka 1991 na kukubali kuketi kwenye meza ya mazungumzo ya amani na utawala ghasibu wa Israel; mazungumzo ambayo hayajawa na matunda yoyote kwa wananchi wa Palestina.

Miaka 51 iliyopita katika siku kama ya leo, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) liliitangaza siku ya mauaji ya umati dhidi ya wazalendo weusi nchini Afrika Kusini yaliyotokea mwaka 1960 kuwa "Siku ya Kimataifa ya Kufuta Ubaguzi wa Rangi". Waafrika weusi wapatao 69 waliuawa na wengine 180 kujeruhiwa katika siku kama ya leo, baada ya askari makaburu kuwafyatulia risasi watu hao waliokuwa wakiandamana kwa amani huko Sharpeville nchini Afrika Kusini kupinga siasa za ubaguzi wa rangi. Japokuwa sera za ubaguzi wa rangi zimefutwa nchini Afrika Kusini lakini ubaguzi na ukosefu wa usawa vingali vinashuhudiwa nchini humo katika sura mbalimbali.
Tarehe 21 Machi 1990, nchi ya Namibia ilipata uhuru kutoka kwa Afrika Kusini. Mwishoni mwa karne ya 19, wakoloni wa Kijerumani, Uingereza na Ureno walianza kuvutana kwa minajili ya kudhibiti na kupora utajiri na maliasili za Namibia. Uhuru wa Namibia ulipatikana kutokana na mapambano ya harakati ya SWAPO chini ya uongozi wa Sam Nujoma.