Mar 27, 2017 23:26 UTC
  • Jumanne, 28 Machi, 2017

Leo ni Jumanne 29 Jamadithani 1438 Hijria sawa na Machi 28, 2017.

Siku kama ya leo miaka 149 iliyopita, alizaliwa mwandishi mashuhuri wa Russia Alexei Maximovich Peshkov aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Maksim Gorky. Gorky alilazimika kusoma na wakati huo huo akifanya kazi ili kuweza kukidhi mahitaji yake ya maisha kutokana na umaskini mkubwa uliokuwa ukimkabili. Alianza kuandika riwaya haraka sana na kufanikiwa kuchapisha riwaya yake ya kwanza katika gazeti la Tbilisi wakati alipokuwa akifanya kazi katika sekta ya reli. Miaka miwili baadaye mwandishi Gorky alipata mafanikio makubwa ambapo alichapisha riwaya yake katika kitabu na taratibu akaanza kuingia katika safu ya waandishi wakubwa na mashuhuri duniani.

Alexei Maximovich Peshkov

Katika siku kama leo miaka 78 iliyopita, baada ya kupita karibu miaka miwili na nusu ya vita vya ndani huko Uhispania, wapigania usultani chini ya uongozi wa Jenerali Francisco Franco waliwashinda wapigania jamhuri na kudhibiti Madrid, mji mkuu wa nchi hiyo. Machafuko yalianza huko Uhispania wakati Alphonso wa 13 mfalme dikteta wa nchi hiyo alipolazimika kujiuzulu kufuatia mashinikizo ya wapigania jamhuri na baadaye mfumo wa jamhuri ukaasisiwa huko Uhispania.

Jenerali Francisco Franco

Na siku kama ya leo miaka 76 iliyopita mwandishi wa Kiingereza, Bi Virginia Woolf aliaga dunia kwa kujiua. Woolf alizaliwa mwaka 1882 na alianza kufaidika na maktaba binafsi ya baba yake ambaye alikuwa mwandishi na mkosoaji wa fasihi, akiwa bado mtoto. Virginia Woolf alianza kuandika vitabu mapema na miongoni mwa vitabu hivyo ni Mrs. Dalloway, The Waves na To the Lighthouse. Hata hivyo maradhi ya kiakili na kinafsi yaliyompata akiwa bado kijana yaliendelea kumuandama na hatimaye mwandishi huyo wa Uingereza aliamua kujiua katika siku kama hii ya leo.

Virginia Woolf