Mar 29, 2017 21:59 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 30 Machi, 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe Mosi Rajab 1438 Hijria, sawa na Machi 30, 2017.

Leo ni tarehe Mosi Rajab, mwezi uliojaa rehema na fadhila tele. Mwezi huu na miezi miwili inayofuata yaani Sha’aban na Ramadhan ni kipindi muhimu kwa ajili ya kujisafisha mwanadamu na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kuhusiana na mwezi huu wa Rajab Mtume Muhammad (SAW) amesema: “Mwezi wa Rajab ni mwezi mkubwa wa Mwenyezi Mungu…kupigana vita na makafiri ndani ya mwezi huu ni haramu. Rajab ni mwezi wa Mwenyezi Mungu, Sha’aban ni mwezi wangu na Ramadhan ni mwezi wa umma wangu.” Kufunga Saumu katika mwezi huu kumesisitizwa sana na kuna thawabu nyingi. Baadhi ya hadithi zimesisitiza sana kufunga Saumu na kuomba maghfira na msamaha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika mwezi huu. Katika mwezi huu kuna matukio mawili muhimu. Tukio la kwanza ni kuzaliwa Imam Ali (as) katika tarehe 13 ya mwezi huu na tukio la pili ni kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad (saw) katika tarehe 27 ya mwezi huu wa Rajab.

Siku kama ya leo miaka 1381 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia alizaliwa Imam Muhammad Baqir AS mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharibu kutoka katika kizazi chake. Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na kupata umashuhuri katika uwanja wa elimu, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya Baqir yaani mchimbua elimu. Kipindi cha Uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu. Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa. 

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita kura ya maoni ya nchi nzima kwa ajili ya kuainisha mfumo wa utawala nchini Iran ilianza baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuanguka utawala wa Pahlavi hapa nchini. Kura hiyo ya maoni iliendeshwa kwa siku mbili kutokana na kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa na wananchi Waislamu wa Iran. Asilimia 98 ya wananchi walioshiriki katika kura hiyo walipiga kura ya ndio wakiunga mkono kuasisiwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran. 

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, maandamano makubwa kwa jina la "Yaumul Ardh" au Siku ya Ardhi yalifanyika huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Ni vyema kukumbusha hapa kwamba, tarehe 18 Oktoba mwaka 1975 Miladia, mkutano wa kutetea ardhi ulifanyika katika eneo la Jalil kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Katika azimio la kwanza la mkutano huo, washiriki walielezea kusikitishwa kwao na hatua ya utawala wa Kizayuni ya kupora ardhi za raia wa Kiarabu wa Palestina na kulaani vikali hatua hiyo. Mkutano wa Jalil ulisisitiza kuwa, siasa za utawala wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu zinakiuka haki za wananchi Waislamu wa Palestina katika ardhi zao na kwamba, utawala wa Kizayuni umepuuza wazi hati ya haki za binadamu na misingi ya demokrasia na usawa.

Siku kama ya leo miaka 150 iliyopita, Russia iliiuzia Marekani ardhi yenye utajiri ya Alaska inayopatikana huko kaskazini magharibi mwa Canada na katika pwani ya bahari za Pacific na Arctic kwa thamani ya dola milioni saba na laki mbili kutokana na mahitaji ya kifedha iliyokuwanayo. Alaska ina ukubwa wa kilomita mraba zaidi ya milioni moja huku likiwa jimbo la 49 la Marekani. Jimbo la Alaska pia lina thamani kubwa za kiuchumi kutokana na kuwa na maliasili nyingi za madini, hususan mafuta na dhahabu pamoja na mapato yanayotokana na uvuvi wa samaki.

Alaska

Na siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, alifariki dunia mwanachuoni mkubwa wa Iran, Ayatullahil Udhma Sayyid Hussein Tabatabai Burujerdi, mmoja wa wasomi mashuhuri wa Iran. Baada ya kumaliza masomo yake ya awali, alielekea mjini Najaf Iraq na kupata kusoma kwa walimu wakubwa wa kidini wa mji huo, kisha akarejea nchini Iran. Ayatullah Burujerdi kwa kushirikiana na wanachuoni wengine wakubwa wa Kiislamu alianzisha Umoja wa Ukurubisho wa Madhehebu ya Kiislamu. Ayatullah Burujerdi licha ya kuandika vitabu kadhaa, alijenga misikiti kadhaa ndani na nje ya Iran, ukiwemo Msikiti wa Hamburg nchini Ujerumani.

Ayatullahil Udhma Sayyid Hussein Tabatabai Burujerdi