Mar 31, 2017 22:03 UTC
  • Jumamosi, Aprili Mosi, 2017

Leo ni Jumamosti tarehe tatu Rajab mwaka 1438 Hijria Qamaria sawa na tarehe Mosi Aprili 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1184 iliyopita yaani mwaka 254 Hijria, Imam Ali Naqi al-Hadi AS mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad SAW aliuawa shahidi. Alizaliwa mwaka 212 katika mji mtakatifu wa Madina. Alikua na kulelewa chini ya uangalizi wa baba yake, yaani Imam Jawad AS. Imam Ali al-Hadi alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake. Imam Ali al Hadi alitumia sehemu kubwa ya umri wake kufundisha, kulea wanafunzi na kueneza mafunzo sahihi ya dini tukufu ya Uislamu. Mapenzi ya watu kwa Imam Hadi kwa upande mmoja na elimu aliyokuwa nayo kwa upande wa pili, ni mambo yaliyowafanya watawala wa wakati huo wa ukoo wa Bani Abbas waingiwe na husuda, na ndio maana wakapanga njama za kumuua shahidi Imam huyo na kuitekeleza katika siku kama ya leo.

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, sawa na tarehe 12 Farvardin mwaka 1358 Hijiria Shamsia, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wananchi Waislamu wa Iran walishiriki katika kura muhimu ya kihistoria ya maoni ya kuamua mfumo uliotakiwa kutawala hapa nchini. Kura hiyo ya maoni ilifanyika kwa muda wa siku mbili. Katika kura hiyo ya maoni asilimia 98.2 ya wananchi Waislamu wa Iran waliunga mkono kuanzishwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini. Kuanzia hapo, kila mwaka ifikapo tarehe 12 mwezi Farvardin, Iran huadhimisha siku hii inayojulikana hapa nchini kwa jina la "Siku ya Jamhuri ya Kiislamu." Matokeo ya kura hiyo ya maoni mbali na kuwatenga wapinzani wa utawala wa Kiislamu, yaliwaonesha walimwengu kwamba Wairani wanataka mfumo wa utawala wa wananchi na demokrasia inayotegemea mafundisho ya dini tukufu ya Uislamu. 

Wananchi Wairani wakishiriki aktika kura ya maoni ya kuunga mkono Jamhuri ya Kiisalmu, Aprili 1, 1979

Miaka 72 iliyopita mwafaka na siku kama ya leo, vikosi vya jeshi la Marekani vilifanya mashambulizi makubwa katika kisiwa cha Okinawa huko Japan. Mashambulizi hayo yaliyofanywa na wanajeshi wa Marekani mwishoni mwa vita vya Pili vya Dunia yanahesabiwa kuwa vita vikubwa zaidi vya baharini na nchi kavu kuwahi kushuhudiwa kati ya Marekani na Japan. Meli 1300 na karibu ndege za kivita za Marekani elfu 10 zilishiriki kwenye vita hivyo vilivyodumu kwa muda wa siku 83. Baada ya hapo Marekani ilitoa amri ya kushambuliwa kwa mabomu ya atomiki miji ya Hiroshima na Nagasaki nchini Japan ili kuilazimu nchi hiyo isalimu amri. Hivi sasa baada ya kumalizika vita na kuja serikali mpya, Marekani iliruhusiwa kuwa na vituo vya kijeshi huko Okinawa jambo ambalo Wajapani wengi wanalipinga.

Wajapani katika kisiwa cha Okinawa wakipinga uwepo wa wanajeshi wa Marekani

Miaka 439 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa nchini Uingereza William Harvey tabibu na msomi wa elimu ya tiba. Harvey alianza kufundisha katika chuo kikuu baada ya kuhitimu mafunzo ya tiba na baadaye akaendelea kufanya utafiti katika uga huo. Mwaka 1616 tabibu Harvey aligundua namna damu inavyozunguka mwilini na kuandika makala kuhusu utafiti huo. William Harvey alifariki dunia mwaka 1657.

William Harvey

Na siku kama ya leo miaka 202  iliyopita Otto Von Bismarck mmoja kati ya shakhsia waliokuwa na nguvu na ushawishi mkubwa katika karne ya 19 barani Ulaya na Kansela wa Ujerumani aliyepewa lakabu ya 'Kansela Madhubuti', alizaliwa. Alisoma sheria katika Chuo Kikuu cha Gottingen na baada ya hapo kuhudumu kama mwanadiplomasia wa Ujerumani huko New York na Paris hadi mwaka 1862 alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Wairi wa Mambo ya Nje. Alishiriki katika vita kadhaa na mwaka. Mfalme Kaiser Wilhelm II aliyekuwa mfalme wa wakati huo wa Ujerumani mwaka 1871 alimteua Bismmarck kuwa kansela wa nchi hiyo na alibakia katika nafasi hiyo kwa muda wa miaka 20. Lakini baada ya kushadidi hitilafu kati yake na Mfalme Wilhelm II, Bismarck alilazimika kujiuzulu. Bismarck alifariki dunia Agosti 24 mwaka 1898.

Otto Von Bismarck