Apr 06, 2017 22:04 UTC
  • Ijumaa, 07 Aprili, 2017

Leo ni Ijumaa tarehe 09 Rajab 1438 Hijria sawa na Aprili 7, 2017.

Siku kama ya leo miaka 95 iliyopita, alizaliwa mtaalamu wa masuala ya Kiislamu wa Ujerumani Bi Annemarie Schimmel. Bibi Schimmel alipendelea mno kutalii na kupata maarifa kuhusu ustaarabu wa Kiislamu na alipata shahada ya uzamivu katika taaluma ya masuala ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Berlin akiwa na umri wa miaka 19. Prf. Annemarie Schimmel alifundisha kwa miaka mingi historia ya dini na irfani ya Kiislamu katika vyuo vikuu vya Marekani, Ujerumani na Uturuki. Mbali na kujua lugha za Kijerumani na Kiingereza, Bi Schimmel alijifunza pia lugha za Kiarabu, Kifarsi, Kiurdu, Kibengali na Kituruki kwa ajili ya kupata maarifa zaidi kuhusu masuala ya Kiislamu.

Prf. Annemmarie Schimmel ameandika vitabu kadhaa kuhusu masuala ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na kile cha "Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu" na "Mwanamke katika Irfani ya Kiislamu". 

Annemarie Schimmel

Miaka 70 iliyopita muafaka na leo, aliaga dunia msomi na mvumbuzi maarufu wa Kimarekani Henry Ford akiwa na umri wa miaka 84. Ford alizaliwa mwaka 1863 katika familia ya kimasikini katika kijiji cha Greenfield nchini Marekani. Akiwa bado barobaro Henry Ford alijishughulisha na utengenezaji wa saa na alipokuwa kijana alifanya kazi ya umakanika. Henry Ford anatambuliwa kuwa mmoja wa wavumbuzi wa magari.

Henry Ford

Miaka 69 iliyopita katika siku kama hii ya leo Shirika la Afya Duniani (WHO) lilifanya baraza la kwanza la dunia la afya na kuandika hati ya kwanza ya mkutano wa kimataifa wa afya. Baraza hilo pia lilichukua uamuzi kwamba tangu mwaka 1950 tarehe 7 Aprili itakuwa Siku ya Kimataifa ya Afya. Tangu mwaka huo tarehe 7 Aprili kila mwaka huadhimishwa kama Siku ya Kimataifa ya Afya.

Siku ya Kimataifa ya Afya

Miaka 52 iliyopita mwafaka na tarehe 18 mwezi Farvardin mwaka 1343 Hijria Shamsiya, Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu Kiongozi na mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliachiwa huru kufuatia malalamiko na mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran. Usiku wa tarehe 15 Khordad mwaka 1342 Hijria Shamsia vikosi vya usalama vya utawala wa Shah vilimtia mbaroni na kumfunga jela Imam Khomeini baada ya kutoa hotuba iliyokuwa ikifichua maovu ya utawala wa Shah. Wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano makubwa kote nchini wakitaka kuachiwa huru kiongozi wao. Radiamali kali ya wananchi wa Iran iliulazimisha utawala wa Shah kumwachia huru Imam Khomeini na baadae kumpeleka nyumbani kwake, ambako huko aliwekwa chini ya uangalizi maalumu.

Hayati Imam Ruhullah Khomeini