Jumatano, 12 Aprili, 2017
Leo ni Jumatano tarehe 14 Rajab 1438 Hijria sawa na 12 Aprili 2017.
Siku kama ya leo miaka 1436 iliyopita yaani tarehe 14 Rajab mwaka wa pili Hijiria, kulijiri vita vya kwanza vya Waislamu na washirikiana wa Makka mwanzoni kabisa mwa kudhihiri dini Tukufu ya Kiislamu. Mapigano hayo ya kwanza ya Waislamu baada ya kusimamisha dola mjini Madina yaliongozwa na Abdullah bin Jahsh Asadi, huku upande wa Maquraish ukiongozwa na Omar bin al Hadhrami. Katika mapigano hayo Omar bin al Hadhrami aliuawa. Mapigano hayo yanajulikana katika historia ya Kiislamu kwa jina la Sariyyatu Abdullah bin Jahsh.

Siku kama ya leo miaka 1280 iliyopita, Zaid bin Ali bin Hussein, mjukuu wa Imam wa Tatu wa Waislamu wa Kishia, alipeperusha bendera ya harakati yake huko mjini Kufa, Iraq wakati wa utawala wa Bani Umayyah. Mapambano ya Zaid ambayo wafuasi wake walitambuliwa kwa jina la Zaidiyyah, yalidumu kwa muda mrefu ambapo mwaka 739 Miladia, aliuawa na Yusuf Ibn Omar Thaqafi, mmoja wa watawala wa Bani Umayyah. Kufuatia matukio hayo, baadhi ya wafuasi wa kiongozi huyo (Zaid bin Ali) ambao hawakuwa Wairani walihamia nchini Yemen na tangu wakati huo Yemen inajulikana kama kituo kikuu cha Waislamu wa Shia Zaidiyyah. Ni bora ikafahamika kuwa, hii leo nusu ya jamii ya Wayemen inaundwa na Mashia Zaidiyyah, Shia Ithna Ashariyyah na Shia Ismailia. Maeneo ambayo wanapatikana zaidi ni kaskazini mwa nchi hiyo.

Siku kama ya leo miaka 197 iliyopita dawa ya kutibu ugonjwa wa malaria iligundulika kutoka kwenye magamba ya mti wa Cinchona. Asili ya mti huu wenye majani ya kijani kibichi ni maeneo ya Amerika ya Kusini lakini hii leo unapandwa katika ameneo mengine ya dunia. Utomvu wa mti huu hutumika kutengeneza dawa chungu sana ya Quinine. Tarehe 12 Aprili mwaka 1820 kwa mara ya kwanza kabisa madaktari Pierre Joseph Pelletier na Joseph Bienaimé Caventou wa Ufaransa walifanyika majaribio dawa hiyo ya malaria katika Maabara ya Paris na kukaanza jitihada za kuzalisha dawa ya Quinine.

Miaka 85 iliyopita sawa na tarehe 12 Aprili 1932 mfumo wa jamhuri uliasisiwa kwa muda huko Uhispania na utawala wa kisultani ukafikia ukomo. Wananchi wa Uhispania waliokuwa wakipigania mfumo wa jamhuri waliendesha mapambano dhidi ya utawala wa kimabavu na kidikteta wa Alphonce wa 13 Mfalme wa wakati huo wa Uhispania na kumlazimisha kujiuzulu.

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, kwa mara ya kwanza mwanadamu alifika katika anga za mbali na kuizunguka dunia. Siku hiyo Yuri Gagarin mwanaanga wa Urusi ya zamani aliyekuwa na umri wa miaka 27 aliizunguka dunia kwa dakika 89 kwa kutumia chombo cha anga za mbali kwa jina la Vastok 1 na kwa msingi huo kukapatikana mafanikio makubwa katika sekta ya masuala ya anga. Gagarin alifariki dunia akiwa pamoja na mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa sekta ya masuala ya anga wa Urusi ya zamani katika ajali ya ndege hapo mwaka 1968.
