Jumatatu, 17 Aprili, 2017
Leo ni Jumatatu tarehe 19 Rajab 1438 Hijria, sawa na 17 Aprili, 2017.
Siku kama ya leo miaka 1429 vilitokea vita vya Tabuk baina ya Waislamu na jeshi la Roma. Vita vya Tabuk ni miongoni mwa vita vya mwisho vya Mtume Muhammad (saw). Sababu ya kutokea vita hivyo ni kwamba, msafara wa kibiashara wa Sham ulimtaarifu Mtume (saw) kwamba mfalme wa Roma ametayarisha jeshi na kulituma Madina. Kwa msingi huo Mtume Muhammad (saw) aliwaanuru Waislamu kujitayarisha kwa ajili ya kukabiliana na jeshi la mfalme wa Roma. Waislamu wengi walijitayarisha kwa ajili ya vita hivyo licha ya masafa marefu, msimu wa joto kali, mashaka ya safari hiyo ngumu na kuwadia msimu wa mavuno. Hatimaye jeshi na wapiganaji elfu 30 la Waislamu liliwasili eneo la vita lakini halikukuta jeshi la mfalme wa Roma eneo hilo.
Japokuwa hakukutokea mapigano wakati huo, lakini tukio hilo lilidhihirisha nguvu ya Waislamu, utayarifu wao wa kukabiliana na majeshi vamizi na moyo wao wa kujitolea kwa ajili ya Allah. Vita hivyo vya Tabuk pia vinajulikana kwa jina la "al Fadhiha" kwa maana ya mfedheheshaji kutokana na kwamba, vililifedhehesha kundi la Waislamu wanafiki waliokataa kujiunga na msafara huo kwa ajili ya kukabiliana na jeshi la Roma.
Miaka 964 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 19 Rajab mwaka 474 Hijria Qamaria Abul Walid Sulaiman bin Khalaf Maliki, faqihi maarufu wa karne ya Tano Hijria Qamaria aliaga dunia huko Andalusia ambayo leo inajulikana kama Uhispania. Alikuwa hafidh na mfasiri wa Qur'ani Tukufu mbali na kubobea katika fasihi na mashairi. Abul Walid awali alifunza Fiqhi na taaluma ya Hadithi za Mtume SAW huko Andalusia na kisha akaendelea kufundisha huko Makka na Baghdad. Kati ya vitabu alivyoandika ni, "Tafsirul Qur'an", "An-Nasikhu wal-Mansukh" na Al-Isharah."
Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita kwa mara ya kwanza kabisa duniani ilitumiwa gesi ya kubana pumzi ya wanadamu vitani. Hatua hiyo ya kinyama ilichukuliwa katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Ujerumani ilitumia gesi hiyo ya kubana pumzi dhidi ya askari wa Uingereza na Ufaransa na kuua askari wengi wa vikosi vya waitifaki. Wajerumani walipata ushindi katika vita hivyo vilivyokuwa mashuhuri kwa jina la Vita vya Gesi.

Siku kama ya leo miaka 91 iliyopita, raia wa Scotland kwa jina la John Logie Baird, alifanikiwa kuvumbua televisheni ambayo hii leo imekuwa na umuhimu mkubwa katika upashaji habari duniani. Baird alikuwa mmoja wa wavumbuzi wakubwa wa enzi zake. Baada ya hapo mtu wa kwanza kutengeneza televisheni iliyoimarika zaidi alikuwa ni Giovanni Caselli, raia wa Italia ambaye mnamo mwaka 1862 alifanikiwa kutengeza chombo ambacho kwa kutumia mfumo wa telegrafi kiliweza kutoa ramani na picha. Televisheni ya kwanza ambayo ilionyesha picha kwa ufasaha, ilianza kutumika tarehe 17 mwezi April mwaka 1926 kwa ajili ya klabu ya kifalme nchini Uingereza.
Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita inayosadifiana na tarehe 17 Aprili 1946, Syria ilijipatia uhuru wake kutoka kwa askari wa kigeni waliokuwa wakiitawala nchi hiyo. Syria na baadhi ya ardhi zinazoizunguka awali ilikuwa ikijulikana kwa jina la Sham, na kabla ya kudhihiri dini tukufu ya Kiislamu ilikuwa chini ya udhibiti wa Iran, Ugiriki, Misri na Rome. Ardhi hiyo ilikuwa makao ya utawala wa Ugiriki na baada ya kukaliwa kwa mabavu na Misri, baadaye ilichukuliwa na utawala wa Othmaniya. Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na baada ya kuporomoka utawala wa Othmaniya, Syria ilikoloniwa na Ufaransa. Kufikia Juni 1941, wakati wa vita vya pili vya dunia, askari wa Uingereza na Ufaransa waliikalia kwa mabavu nchi hiyo, hadi kufikia mwaka 1946 wakati ilipojipatia uhuru wake.
Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita mwafaka na leo alifariki dunia mjini Baghdad Iraq Ayatullahi Sheikh Muhammad Khalisi maarufu kwa jina la Khalisizadeh. Alipanda kwa haraka daraja za kielimu na kujishughulisha na harakati za kitamaduni na kidini, sambamba na kupambana na upenyaji wa ukoloni katika nchi za Kiislamu. Katika harakati hizo za kuwaamsha wananchi wa Iraq Ayatullahi Khalisi alikuwa na lengo la kuwashawishi wananchi wa nchi hiyo kuanzisha mapambano dhidi ya vikosi vya Uingereza vilivyokuwa vimeikalia Iraq. Hatimaye msomi huyo alikamatwa na kubaidishwa nchini Iran. Vitabu vya " Madhalim Inglis dar Baina Nahrain" na "Khodaa dar Tabiiat" ni miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa na msomi huyo.