Alkhamisi, 20 Aprili, 2017
Leo ni Alkhamisi tarehe 22 Rajab 1438 Hijria sawa na 20 Aprili, 2017
Siku kama ya leo tarehe 20 Aprili miaka 215 iliyopita mawahabi wa Hijaz walishambulia mji mtakatifu wa Karbala nchini Iraq na kuua mamia ya Waislamu wa madhehebu ya Shia. Baada ya mawahabi kushika hatamu za uongozi huko Hijaz mwanzoni mwa karne ya 19 walianzisha mashambulizi ya mara kwa mara ya kundi hilo lenye misimamo na fikra za kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wengine husan wafuasi wa Watu wa Nyumba ya Mtume wetu Muhammad (saw) na miongoni mwa mashambulizi ya mawahabi hao ni yale ya kushambulia miji mitakatifu ya Karbala na Najaf nchini Iraq tarehe 20 Aprili mwaka 1802. Miji hiyo ambayo ni mitakatifu hususan kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia kutokana na kuwa na makaburi ya watu wa Kizazi cha Mtume wetu Muhammad (saw) imekuwa ikilengwa na mawahabi. Katika mashambulizi hayo mawahabi walishambulia haram ya mjukuu wa Mtume, Imam Hussein bin Ali mwana wa Bibi Fatima (as) huko Karbala na kuvunja quba na kaburi na mtukufu huyo na kisha wakapora mali iliyokuwa hapo. Waislamu zaidi ya elfu mbili waliuawa katika shambulizi hilo la mawahabi. Mashambulizi hayo yaliwakasirisha sana Waislamu katika maeneo mbalimbali ya dunia na kuzidisha chuki yao dhidi ya mawahabi na mafundisho ya kundi hilo potofu. Mawahabi walidumisha mauaji ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na madhehebu nyinginezo baada ya kuanzishwa dola la watawala wa kizazi cha Aal Saud huko Saudi Arabia na walishambulia na kuharibu Haram ya wajukuu wa Mtume Muhammad (saw) na za masahaba zake wakubwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina.
Katika siku kama ya leo miaka 210 iliyopita, aliaga dunia Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa msomi na fakihi mtajika wa Kishia. Alizaliwa mjini Najaf huko Iraq na kuanza kujihusisha na masomo ya dini tangu katika kipindi cha utoto wake. Awali alisoma masomo ya utangulizi kwa baba yake na kisha baadaye akahudhuria masomo kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama sayyid Mahdi Bahr al-Uluum. Baadaye Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa alianza kufundisha na kuandika vitabu na kufanikiwa kuwalea wanafunzi wengi na vile vile kuandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali.
Miaka 18 iliyopita inayosadifiana na 20 Aprili 1999, kulitokea maafa makubwa ya mashambulizi yaliyofanywa na wanafunzi wawili wa Kimarekani kwenye shule moja ya sekondari. Wanafunzi hao waliwamiminia risasi na kuwaua wanafunzi wenzao 12 na mwalimu wao na kuwajeruhi wengine 21. Wanafunzi hao waliovamia shule ya Columbine High School iliyoko Denver, jimbo la Colorado, walijiua wenyewe baada ya kufanya mauaji hayo. Mauaji kama hayo ya kutisha yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika maeneo ya umma nchini Marekani. Wataalamu wanasema uhuru wa kununua na kumiliki silaha ni miongoni mwa sababu za maafa hayo yanayotokea kila mwaka nchini Marekani.

Miaka 7 iliyopita katika siku kama ya leo, mlipuko uliotokea kwenye mtambo wa kuchimba mafuta wa Deepwater Horizon na kuzamisha mtambo huo mali ya Shirika la Mafuta la Uingereza (British Petroleum) kulikosababisha kuvuja mafuta katika Ghuba ya Mexico. Wafanyakazi 11 wa mtambo huo waliuawa na mafuta mengi yaliyokuwa yakivuja kutoka katika kisima hicho yalisababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira kuwahi kutokea katika karne moja ya hivi karibuni huko Marekani.
