Jumatatu, 24 Aprili, 2017
Leo ni Jumatatu tarehe 26 Rajab, 1438 Hijria sawa na Aprili 24, 2017.
Siku kama ya leo miaka 1465 iliyopita kwa mujibu wa mahesabu ya wanahistoria wengi, iliasisiwa kwa mara ya kwanza taasisi ya kuandika na kutarjumu vitabu duniani hapa nchini Iran. Uamuzi huo ulichukuliwa na Khosrow Anushirawan, mfalme wa Sasani nchini hapa. Taasisi hiyo iliyoenda sambamba na maktaba ya kijamii kwa pamoja vilikamilishwa kujengwa mwaka huo huo sawa na tarehe 24 April mwaka 552 Miladia. Vitabu tofauti vililetwa kutoka maeneo mbalimbali ya dunia kwa ajili ya kutarjumiwa huku mfalme huyo akimtuma pia daktari wake kwenda nchini India kwa ajili ya kuleta vitabu kwa ajili ya shughuli hiyo.

Siku kama ya leo miaka 1441 iliyopita, alifariki dunia Abu Twalib ami wa Mtume Muhammad SAW na baba wa Imam Ali AS, wakati ambapo Waislamu walikuwa chini ya mzingiro wa washirikina wa Makka. Abu Twalib alikuwa pamoja na Waislamu wengine huko katika Sha'abi Abi Twalib. Mtume Muhammad SAW alikuwa chini ya uangalizi wa Abu Twalib tangu akiwa na umri wa miaka minane, baada ya kuaga dunia babu yake Abdul Muttalib. Abu Twalib aliikubali dini ya Kiislamu baada ya kubaathiwa Mtume na alikuwa muungaji mkono na mtetezi mkubwa wa Mtume Muhammad SAW mbele ya washirikina wa Kikureish.

Siku kama ya leo miaka 746 iliyopita, Marco Polo alianza safari yake ya kitalii na ya kihistoria barani Asia. Kabla ya hapo, baba yake pamoja na ami yake walifanya safari katika baadhi ya nchi za Asia na kufika hadi Uchina. Katika zama hizo, China, Mongolia na Iran zilikuwa chini ya himaya ya Changiz Khan Mogul. Baada ya kurejea nchini kwake, Marco Polo aliandika kumbukumbu na aliyoyaona barani Asia katika kitabu alichokipa jina la Maajabu. Katika kitabu hicho alizungumzia utumiaji wa fedha za noti nchini Uchina, miundombinu kama ile ya majitaka, madaraja marefu, posta na kadhalika. Mambo haya yaliwastaajabisha watu wa Ulaya wa zama za kati ambao walikuwa wameghiriki katika hurafa.
Siku kama ya leo miaka 90 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 24 Aprili 1927 iligunduliwa chanjo ya BCG. Chanjo hiyo iligunduliwa na Calmette na Guerin madaktari bingwa wa Ufaransa, baada ya kufanya utafiti kwa miaka kadhaa. Chanjo ya BCG inatumika kwa ajili ya kuzuia maradhi ya kuambukiza ya kifua kikuu, na baada ya kugunduliwa chanjo hiyo kasi ya maradhi hayo imepungua katika pembe zote za dunia.
Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 4 Ordibehesht 1319 Hijria Shamsia, ilianzishwa Idara ya Redio nchini Iran na kurushwa matangazo ya moja kwa moja kupitia kituo cha matangazo cha Redio Tehran. Mwanzoni mwa kuanzishwa redio nchini Iran taasisi hiyo kilikuwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Posta, Simu na Telegrafu. Miaka mitano baada ya kuanzishwa kituo cha redio mjini Tehran, hatua kwa hatua huduma hiyo ilipanuliwa katika miji mbalimabali hapa nchini. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu 1979, zilianzishwa redio na televisheni kadhaa, zikiwemo zile za matangazo ya ng'ambo, zinazotangaza kwa kutumia zaidi ya lugha thelathini za dunia.
