Jumatatu, Mei Mosi, 2017
Leo ni Jumatatu tarehe 4 Shaaban 1436 Hijria mwafaka na tarehe Mosi Mei mwaka 2017.
Siku kama ya leo miaka 1412 iliyopita, yaani tarehe 4 Shaaban mwaka 26 Hijria, alizaliwa Abbas bin Ali bin Abi Talib mashuhuri kwa lakabu ya Abul Fadhl. Mama yake ni Ummul Baniina, ambaye aliolewa na Imam Ali bin Abi Twalib (A.S) baada ya kufariki dunia bibi Fatima Zahra AS. Alikulia katika familia ya watu adhimu kama baba yake Ali (as) kaka zake Imam Hassan na Hussein na dada yake mukufu Zaunab (as). Alimpenda sana kaka yake Hussein Bwana wa mashahidi kiasi kwamba alisabilia roho na nafsi yake katika ardhi ya karbala akimtetea yeye na risala yake. Abbas alifahamika mno kutokana na elimu, ukweli na uchaji Mungu wake. Kutabahari kwake kielimu kuliwafanya watu wengi warejee kwa ajili ya kutatuliwa masuala mbalimbali ya kielimu. Siku ya kuzalwia Abul Fadhl Abbas inatambuliwa hapa nchini kama Siku ya Vilema wa Vita.

Siku kama ya leo miaka 128 iliyopita yaani tarehe Mosi Mei 1889, ilitangazwa rasmi kuwa 'Siku ya Wafanyakazi Duniani'. Tarehe Mosi Mei 1886, zaidi ya wafanyakazi elfu 40 walifanya maandamano katika mji wa Chicago nchini Marekani kwa shabaha ya kudai haki zao. Wafanyakazi hao walitaka nyongeza za mishahara, kuboreshwa suhula za maeneo yao ya kazi na uadilifu kazini. Maandamano hayo yaliingiliwa na askari polisi, na matokeo yake yakawa ni idadi kadhaa ya wafanyakazi hao kuuawa na wengine kujeruhiwa.
Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, sawa na tarehe Mosi Mei 1915, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia yalitokea mapigano makali kati ya majeshi ya Urusi na Ujerumani katika eneo la Krakow lililoko nchini Poland. Jeshi la Ujerumani lililoyashinda majeshi ya Urusi kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia mwaka 1914, katika vita hivyo kwa kutumia mizinga liliyashinda majeshi ya Urusi na hatimaye kulidhibiti eneo la Poland. Kushindwa kwa majeshi ya Urusi katika Vita vya Kwanza vya Dunia na hali kadhalika hali mbaya iliyokuwemo nchini humo, ni miongoni mwa sababu muhimu za kujiri mapinduzi ya Kikomonisti nchini humo mwaka 1917, na hatimaye nchi hiyo kujiondoa kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia.
Na miaka 12 iliyopita katika siku kama hii, tarehe Mosi Mei 2004, nchi nyingine 10 za Ulaya zilijiunga na Umoja wa Ulaya na kufikisha jumla ya nchi 25 wanachama wa umoja huo. Nchi hizo ni Estonia, Latvia, Lithuania, Poland, Jamhuri ya Czeck, Slovakia, Hungary, Slovenia, Cyprus, na Malta. Licha ya kuwa kujiunga nchi hizo kulihesabiwa na jumuiya hiyo kuwa moja ya mafanikio, lakini kuna ufa wa kisiasa, kiuchumi na kijamii kati ya nchi wanachama wa zamani na wapya. Vilevile mwaka 2007, nchi za Romania na Bulgaria zilijiunga na umoja huo na jumla ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kufikia 27.